BALOZI DK.ASHA-ROSE MIGORO APONGEZA HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA RAIS MAGUFULI KATIKA KUKABILIANA NA MAAMBUKIZI YA CORONA

Na Said Mwishehe, Michuzi TV
BALOZI wa Tanzania nchini Uingereza Dk.Asha-Rose Migiro amepongeza hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli katika kukabiliana na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 ikiwemo ya kutoweka nchi kwenye 'Lockdown'.
Dk.Migiro amesema katika kukabiliana na Corona kila nchi iliamua kuchukua hatua kulingana na mazingira yake huku akifafafanua kwa kina kuhusu Lockdown ingawa tayari kwa Uingereza wanafikiria kuanza kuiondoa ili wananchi warejee kwenye kuanza kufanya shughuli zao za kawaida.
Akizungumza leo Mei 11 kwa njia ya simu akiwa nchini Uingereza alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Clouds TV kwenye kipindi cha 360, Dk.Migiro amesema kwanza anafurahishwa na hatua ambazo zinachukuliwa na wananchi wa Tanzania kwani wamekuwa na muako mkubwa wa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni pamoja na kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali.
" Ujumbe kwa Watanzania wenzangu huko nyumbani nawaomba tuzingatie ushauri unaotolewa na Serikali pamoja na Wizara ya Afya.Tuendelee kutafuta riziki huku tukichukua tahadhari kwa kujikinga na virusi hivyo,"amesema Dk.Migoro.
Kuhusu Lockdown kwa nchi za Afrika, Dk.Migiro amesema mfumo huo sio rafiki kwa nchi hizo hasa kutokana na mazingira ya kiuchumi yalivyo, hivyo ametumia nafasi hiyo kumpongeza Tanzania kwa uamuzi wake wa kutowafungia wananchi ndani (Lockdown) kwani madhara yake kiuchumi ni makubwa sana.
Amefafanua kwa Uingereza athari za kuweka Lockdown imeanza kuonekana kiuchumi na hali itakuwa mbaya zaidi baada ya Corona kwisha kwani watu wengi watapoteza ajira zao .
"Kwa hapa Uingereza hii Lockdown tayari imeanza kuleta athari za kiuchumi lakini pia hata baadhi ya watu wanaonekana kuathirika kisaikolojia na wengine kupata magonjwa ya akili na huu utakuwa mzigo kwa Serikali.
"Hivyo kwa nchi zetu za Afrika lazima ziangalie kuhusu Lockdown, huku Uingireza angalau kuna mambo yanaweza kubebwa na Serikali.Kwa mfano watu wasiokuwa na kazi wanalipwa nusu mshahara lakini kwa nchi zetu za Afrika hatujafika huko,"amesisitiza Dk.Migiro.
Alipoulizwa ni hatua gani ambazo Uingereza imeamua kuchukua kukabiliana na Corona,Dk.Migiro amejibu kuwa kabla ya maambukizi kuingia nchini humo, wananchi walikuwa wakipewa elimu ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi na baada ya ugonjwa kuingia wakaongeza hatua zaidi ikiwemo ya kusitisha safari za treni, kuzuia baadhi ya watu kwenda kazi na kisha kufanyia kazi nyumbani.
Pia ilitoa maelekezo ya kuzuia safari ambazo hazina ulazima na waliotakiwa kutoka ndani basi ni kwa sababu maalumu kama kufuata chakula , kununua dawa na kwenda kuona mtu mwenye mahitaji maalumu."Hata hivyo tayari Waziri Mkuu wa Uingereza ametangaza kuwa wanatarajia kuruhusu watu kutoka na kwenda kwenye shughuli zao."
Previous article
Leave Comments
Post a Comment