ALIYEKUWA MWENYEKITI BODI YA WAKURUGENZI REA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SERENGETI
Na Mwandishi Wetu, Mpanda
WAKATI Joto la uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba Mwaka huu likizidi kupambana moto hapa nchini,aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya wakala wa umeme vijijini(REA)Michael Nyagoga pichani ametangaza rasmi kugombea ubunge jimbo la Serengeti mkoani Mara.
Nyagoga ambaye amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa taasisi mbalimbali hapa Nchini, ametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo jana kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi jana mjini Mpanda.
Nyagoga, kwa sasa ni katibu Tawala msaidizi sekretalieti ya mkoa wa Katavi alisema, anataka kuwa mbunge wa jimbo la Serengeti ili kubadilisha maisha ya wananchi wa jimbo hilo ambao kwa muda mrefu wamekosa kupata mtu sahihi .
Alisema, kwa miongo kadhaa wakazi wa Serengeti wamewapa nafasi baadhi ya watu kuwakilisha, hata hivyo wameshindwa kuisaidia Serengeti kutatua changamoto zinazo wakabili kama miundombinu ya barabara,maji, umeme wa uhakika pamoja changamoto nyingine.
Alisema,sasa ni wakati muafaka kwa wana Serengeti kuchagua mtu mpya ambaye anaweza kusaidiana nao kutatua changamoto hizo ambazo zimechangia jimbo hilo kubaki nyuma kimaendeleo.
“mtu atakayepewa dhamana hiyo anapaswa kuwa mchapakazi,mwadilifu,mweledi, na mbunifu anayeheshimu wenzake,mwenye mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo na kikubwa zaidi awe mtu anayepinga vitendo vya rushwa”alisema Nyagoga.
Nyagoga alitolea mfano kuwa, Serengeti ina watu wengi wenye sifa hizo akiwemo yeye binafsi ambaye ametaja sababu kubwa zilizomshawishi kufikia uamuzi huo wa kugombea Ubunge ni kwenda kuungana na wananchi kutatua kero zilizokuwepo kwa muda mrefu ili wilaya hiyo ipige hatua kimaendeleo kama ilivyo kwa maeneo mengine hapa nchini.
Anataja, changamoto ya kukosekana kwa barabara inayounganisha wilaya na makao makuu ya mkoa tangu Uhuru mwaka 1961,kutokuwepo kwa umeme wa uhakika na maji safi na salama ni kati ya kero kubwa ambazo zimechangia sana kudumuza maendeleo.
Aidha alisema, wabunge wote waliopewa dhamana kwa nyakati mbalimbali wameshindwa kuisaidia Wilaya ya Serengeti kutatua changamoto hizo akiwemo Mbunge anayemaliza muda wake Marwa Ryoba, ambaye awali alikuwa Chadema na baadaye kwa kulinda na kutetea maslahi yake akarejea Chama cha Mapinduzi.
Amewataka wana Serengeti kuchagua mtu mpya,mwenye mawazo mapya,maono mapya,mikakati,mipango mipya inayoendana na kasi ya sasa katika kutatua changamoto zinazokabili wilaya na jimbo la Serengeti.
Nyagoga anataja mafanikio ya miaka 28 katika utumishi wa umma akiwa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi miaka 13,wizara ya fedha na mipango miaka 13 na Ofisi ya Rais Tamisemi miaka 5 ambayo ni ishara tosha kuonyesha jinsi alivyofanikisha alama za mafanikio katika kila kituo cha kazi.
Kwa mujibu wa Nyagoga, kazi hizo ni miongoni mwa kazi nyingi ambazo ameshiriki kuzisimamia na kuziratibu kwa mafanikio makubwa kuanzia maboresho ya Sera,maandalizi ya sheria na hatimaye maandalizi ya kanuni.
Ameeleza kuwa, dhamana aliyopewa ya kutumikia ameonyesha kwa vitendo namna ya mtumishi na kiongozi anavyoweza kuishi kwa mafanikio akiheshimu wenzake,akitenda haki na kupinga rushwa kwa vitendo, hivyo kwa nyenzo hizo anaweza kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Serengeti mpya.
Nyagoga anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuwa sehemu ya mafanikio hayo kwa kutumia elimu na uzoefu wake kwa manufaa ya na maslahi ya Watanzania wote.
Next article
Leave Comments
Post a Comment