KITUO CHA AFYA CHA MAPERA KIMEPATA GARI LA KUBEBEA WAGONJWA
Picha na Mtandao.
KITUO cha Afya Mapera kilichopo katika Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, kimepata gari la wagonjwa(Ambulance) iliyonunuliwa na Halmashauri hiyo ili kurahisisha usafiri kwa wagonjwa watakohitaji na kupewa rufaa kwenda Hospitali ya wilaya Mbinga na Rufaa ya mkoa Songea.
Akikabidhi gari hilo kwa Mganga Mkuu wa kituo cha Afya Mapera,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Juma Mnwele alisema, gari hilo limetokana na ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa wananchi wa kata ya Mapera la kuwapatia gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo hicho.
Alisema, Waziri Mkuu baada ya kupata ombi hilo aliiagiza Halmashauri ya wilaya kutumia mapato yake ya ndani kununua gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha Afya Mapera ili lisaidie wananchi hasa wagonjwa watakaopewa rufaa kutoka katika kituo hicho kwenda Hospitali ya wilaya Mbinga mjini,au Hospitali ya Rufaa ya mkoa Songea kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mnwele alisema,gari hilo limenunuliwa kwa shilingi ml 138 kutokana na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo linakwenda kumaliza kero ya wagonjwa wanaopewa rufaa kukodi magari ya watu binafsi kwa gharama kubwa ikilinganisha na hali halisi ya maisha ya wananchi hao.
Alisema, katika mkoa wa Ruvuma kuna vituo vya Afya 16 lakini ni Mapera ndiyo iliyopewa upendeleo kwa kupata fedha za kujenga majengo mapya katika kituo cha Afya na kupata gari jipya la wagonjwa.
Hata hivyo alisema, kwa kuwa halmashauri ya wilaya Mbinga ni kubwa kuna wakati litahitajika kwenda kutoa huduma kwa wagonjwa wa vijiji vingine katika halmashauri hiyo, na kuwaeleza wananchi kwamba gari hilo litatumika kwa ajili ya wagonjwa na sio shughuli nyingine za kijamii.
Akizungumzia ujenzi wa majengo hayo alisema, Serikali kuu imetoa shilingi ml 500 na Halmashauri ya wilaya imeongeza milioni 80 zilizowezesha kukamilisha kazi ujenzi huo ambapo ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zimekwenda kuimarisha na kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.
Alisema, kujengwa kwa majengo mapya kutawezesha wauguzi na madaktari kufurahia mazingira bora na hivyo kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa.
Alisema, mbali na kununua gari na kuongeza majengo mapya,Serikali imepeka Madaktari wawili ambao watasaidiana na waliopo kutoa huduma za matibabu na kuwataka wananchi wa Mapera kuwapa ushirikiano ili waweze kutekeleza wajibu wao.
Baadhi ya wananchi Betram Komba,Anitha Nikata na Mganga Mkuu wa kituo hicho Dkt Charles Sanga wameipongeza Halmashauri ya wilaya Mbinga kwa kuona umuhimu wa kununua gari la wagonjwa na kutekeleza haraka agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Betram Komba Alisema, awali kulikuwa na changamoto ya gari la wagonja pale mgonjwa anapohitaji rufaa kwenda Hospitali kubwa kwa ajili ya huduma kama ya upasuaji kwani walilazimika kukodi magari ya watu binafsi kwa gharama kubwa jambo lililopelekea baadhi ya wananchi kushindwa kumudu gharama ya kukodi magari.
Alisema,hali hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi hasa akina mama wajawazito kujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha kwa kushindwa kufika kwa wakati katika Hospitali kubwa.
Leave Comments
Post a Comment