Monday, 17 March

Ads Right Header

Buy template blogger

MTI WA MNINGA, MKONGO HATARINI KUTOWEKA

MTI WA MNINGA, MKONGO HATARINI KUTOWEKA
Na Tulizo Kilaga- TFS

IMEELEZWA kuwa ongezeko la watu nchini limeongeza utegemeze wa matumizi ya mazao ya misitu hususan mbao za miti ya mninga na mkongo na hivyo kuhatarisha uwepo wa miti hiyo katika miaka michache ijayo.

Hayo yameelezwa Juni na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii, Deosdedit Bwoyo alipokuwa akifungua kikao cha kitaalamu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) na taasisi za Serikali na binafsi zinazoshughulika na ujenzi, ununuzi na utengenezaji wa samani jijini Dodoma.

Bwoyo amesema tumekutana leo ili tujadili matumizi ya mbao za miti ya misaji kama mbadala wa mbao za mti wa mninga na mkongo zilizopo hatarini kutoweka.

“Watanzania tunapenda sana kutumia mbao za mkongo na mninga lakini mninga hadi kukomaa kwake unachukua zaidi ya miaka 70, na hatujaweka utaratibu mzuri wa kuendelea kuwa na miti hii baada ya hio, miti hii inapungua sana na hivyo inatupasa kuchukua hatua,

“Sera ya Misitu inasisitiza usimamizi na matumizi endelevu ya mazao ya misitu kwa maana ya tupande lakini tufanye matumizi endelevu, lakini pia inasisitiza matumizi ya mbao nyingine kwa maana ya kwamba miti yote lazima itunufaishe sisi Watanzania,

“Bahati nzuri Serikali miongo kadhaa iliyopita ilianzisha mashamba ya mbao ngumu aina ya Misaji Katika Shamba la Miti Mtibwa na Ronguza ambayo ina sifa sawa na miti ya mninga na mkongo, mashamba haya yana uwezo wakutoka mita za ujazo 20,000 kila mwaka kwa miaka mingi ijayo, kuna haja ya kuazna kutumia miti hii kama mbadara ili kizai kijacho kiweze kuona na kutumia mninga na mkongo,” amesema Bwoyo.

Ameongeza kuwa hali ikiendelea kama ilivyo sasa katika miaka michache ijayo Tanzania haitakuwa na mti wa Mninga wala mkongo.

Kutokana na hali hiyo Naibu Kamishina Mhifadhi wa Misitu anayesimamia Masoko, Mipango na Matumizi ya Rasilimali Misitu, Mohamed Kilongo amesema waliamua kuitisha kikao hicho kwa lengo la kuangalia matumizi sahihi ya mbao zilizopo za mkongo na mninga, na mbao mbadala.

“Sisi kama wahifadhi wa rasilimali misitu na nyuki, tumeona tuanze sehemu ya mazungumzo ili tuwe na mbadala wa mbao za mninga na mkongo ambazo tumekuwa tunatumia tu bila kupanda, sasa tunamipango ya kupanda, lazima tuangalie matumizi bora na sahihi ili rasilimali hizi zisiishe,” ameongeza Kilongo.

Amesisitiza katika mpango huo wataangalia kilichopo katika soko na shambani na kuangalia wanchopendela wadau kulingana na uhitaji kwa kuzingatia kilichopo na wanachotaka kisha kuwashauri kulingana na kilichopo sokoni.

Kilongo amesema katika kikao hicho wameangalia kanuni za manunuzi zinazosisitiza matumizi ya mbao za mninga na mkongo kwenye jezi na samani za serikali jambo ambalo ni hatari kwa uwepo wa miti hio.

“Wakati tunaandaa mipango ya kupanda miti ya mninga na mkongo lazima kwenye sera na sheria na kanuni zetu tuingize matumizi ya mbao za miti mbadala yenye ubora sawa na mninga na mkongo. Hivyo leo tumeangalia sheria na kanuni zinasemaje ili sisi kama watendaji tuweke miongozo ya hawa watumiaji wa mbao ili tuwe na matumizi endelevu lakini pia tusipate shida yakupata mbao hizo,” amesema Kilongo.

Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Bodi ya Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Ujenzi nchini (AQRB), Shangwe Kambaga, Mkadiriaji Majenzi Mkuu wa AQRB kanda ya Kati aliyepewa jukumu la kufunga kikao hicho alisema wadau wa sekta ya ujenzi hawawezi kukwepa utumiaji wa mbao ngumu na kutokana na hatari ya kutoweka kwa mbao za mikongo na mninga wameona haja ya kutumia mbao mbadala.

“Tumekuwa tukiwapa kongwa wakandarasi wetu kwa kuwaandikia kwenye specification kuwa lazima watumie mbao za mninga au mkongo lakini kumbe kuna mbadala unaoweza kutumika na Serikali ikaona value for money! Nitaenda kumshauri msajili wangu tujadili hili katika kikao chetu kinachokwenda kufanyika jijini Arusha hivi karibuni ili tuazimia kuanza kutumika kwa mbao za teak kwenye ujenzi,” amesema Kambaga.

Kwa upande wake Mwakilishi Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Emanuel Isaya amesema kuwa kuna haja ya Wizara ya Ujenzi ambayo kwa mujibu wa kanuni za ununuzi wa umma imepewa mamlaka ya kuweka viwango na vigezo vya ubora wa mbao zinazofaa tumika badala ya kutaja majina.

“Kuna haja ya kutaja ubora wa mbao zinazofaa kutumika kutengenezea samani ama majengo ya Serikali badala ya ilivyo sasa kutaja majina ya mti, leo tumeelezwa kuna miti yenye bora sawa na mninga na mkongo sasa Wizara ishirikiane na TFS kutengeneza vigezo vya ubora ili wazabuni waweze tumia miti mbadala kama vile wake,” amesema Isaya.

Katika kikao hicho mashirika mbalimbali ya serikali na binafsi yalihudhuria baadhi yao ni NHC, TBI, TAFORI, TBS, PPRA, NCC na Jaffar Industries .

Naibu Kamishna Mhifadhi Wa Misitu Mohamed Kilongo akisititiza jambo kwa wadau (hawako) pichani.Picha ya pamoja ya wadau mara baada ya kumaliza kikao hicho.

Leave Comments

Post a Comment

Ads Post 4