Wednesday, 19 March

Ads Right Header

Buy template blogger

MAELFU YA WAOMBOLEZAJI WAMUAGA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA UWANJA WA UHURU, KUZIKWA KESHO

MAELFU YA WAOMBOLEZAJI WAMUAGA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA UWANJA WA UHURU, KUZIKWA KESHO
Na Said Mwishehe, Michuzi Tv
MAELFU ya waombolezaji wakiongozwa na Rais Dk.John Magufuli wameshiriki tukio la kuaga kitaifa mwili wa mzee wetu, Rais mstaafu Benjamin Mkapa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam leo Julai 28,2020.

Katika tukio hilo, mbali ya Rais Magufuli ambaye aliongozana na Mama Anna Mkapa kwenda kuaga, pia waliwepo marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Aman Karume, viongozi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, viongozi wa ngazi mbalimbali Serikali, pamoja na viongozi wastaafu.

Kabla ya kuanza kutoa heshima za mwisho, waombolezaji waliokuwepo uwanjani hapo walipata salamu kutoka kwa makundi mbalimbali ambao wameguswa na msiba huo mkubwa kwa Taifa la Tanzania kwa kuondokewa na Rais mstaasfu wa Awamu ya Tatu.

Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli hiyo baada ya Rais Dk.Magufuli kwenda kuaga akiwa ameambatana na Mama Anna Mkapa pamoja na familia yake walifuata viongozi wengine kwa utaratibu uliokuwa umewekwa. Hata hivyo Rais na familia ya Mkapa waliondoka baada ya kutoa heshima zao za mwisho na kuacha viongozi wengine wakiendelea kuaga.

Wakati shughuli hizo zikiendelea ambazo zilianza mapema asubuhi, simanzi, huzuni na majonzi zilikuwa zimetawala katika Uwanja wa Uhuru kutokana na kila mmoja kutafakari msiba huo wa kuondokewa na mzee wetu ambaye amelitumikia Taifa la Tanzania kwa uzalendo na uadilifu mkubwa alipokuwa Rais wa Awamu ya Tatu.

Mzee Mkapa ambaye katika utawala wake aliamini katika uwazi na ukweli na kuwa mbunifu katika kuhakikisha Serikali anayoingoza inatekeleza wajibu wake kwa utaratibu unaoeleweka, hivyo kumfanya afanikiwe kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo baada ya kuaga kwa mwili wa mzee Mkapa, mwili wake uliondolewa uwanjani hapo saa 11:45 asubuhi kwa ajili ya kwenda Uwanja wa Ndege kwa safari ya kwenda kijijini kwake Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara ambako atapumzishwa katika nyumba yake ya milele kesho Julai 29,2020,  saa nane mchana.

Wakati msafara huo gari iliyobeba ilikuwa inakwenda kwa mwendo wenye kasi ya spidi 35 hadi 40, kando ya barabara wananchi walikuwa wamejitokeza wakishuhudia mwili huo  ukipitishwa ambako pikipiki saba zilikuwa zikiongoza msafara na gari ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)ndio iliyokuwa   imebeba mwili ikiwa katikati.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi kitaifa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni kwamba kesho wananchi wa Lupaso na waombolezaji wengine nao watapa nafasi ya kuaga mwili wa mzee Mkapa kuanzia saa mbili asubuhi na itakapofika saa nane mchana ndio atakwenda kupumzishwa huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kuendelea kuyaenzi yale yote aliyofanywa enzi za uhai wake.

Leave Comments

Post a Comment

Ads Post 4