KESI YA MBUNGE CHADEMA KUANZA KUSIKILIZWA SEPTEMBA 7
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga, Septemba 7, mwaka huu kuanza kusikiliza utetezi wa kesi ya uchochezi, inayomkabili Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo leo Agosti 13,2020 lakini imeshindwa kuendelea kufuatia mawakili wa utetezi kushindwa kufika mahakamani hapo.
Akitoa taarifa juu wa kutokuwepo kwa mawakili wake, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,
mshtakiwa Mdee amedai kuwa mawakili wake, Peter Kibatala na Hekima Mwasipu, wameshindwa kufika mahakamani hapo kwa sababu wapo kwenye kesi nyingine katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara na Kazi.
Mapema Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kuwa shauri hilo leo liliitwa kwa ajili ya mshitakiwa kuanza kujitetea lakini kwa sababu mawakili wa mshitakiwa huyo hawapo mahakaman, aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya utetezi.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, 2020 kwa utetezi.
Katika kesi ya msingi Mdee anadaiwa kuwa Julai 3,2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, alitenda kosa la kutoa lugha chafu.
Anadaiwa kutamka maneno machafu dhidi ya Rais John Magufuli kuwa “anaongea hovyo hovyo , anatakiwa afungwe breki” na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Leave Comments
Post a Comment