SABABU YA SENZO KUBWAGA MANYANGA SIMBA NA KUIBUKIA YANGA IPO HIVI
Mhariri Mwandamizi wa Gazeti la Championi na mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Saleh Ally Jembe, akizungumza katika kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio amesema kuwa moja ya sababu kuu zilizomwondoa Senzo katika Klabu ya Simba ni kwamba alishindwana na Simba kuhusu malipo ya mkataba wake mpya, kwani kiasi alichoomba kuongezewa, Simba waligoma kutoa.
"Kwanza ni kuwapongeza Yanga SC, lakini Simba SC wamepaniki sana, wanahisi Senzo ataondoka na Chama au Simba itayumba kimafanikio, Senzo ameikuta tayari Simba ina mafanikio, imekwenda Robo Fainali (CAF Champions League), ilikuwa imebeba ubingwa (VPL) mara mbili, Senzo hakuwepo.
“Yanga SC wana haki ya kufurahi sana kwa sababu walikereka Morrison kwenda Simba SC, na ninasikia walikuwa na sherehe ya kujipongeza, lakini Yanga wanapaswa kujua kwamba Senzo siyo kocha wala mchezaji, hawezi kuleta mafanikio ndani ya muda mfupi, wampe muda.
“Simba SC wanasema kazi aliyokuwa anaifanya Senzo alikuwa ameshawatoa sehemu ambayo kuna vitu hawakuwa wanavijua, baada ya hapo hakuna mwendelezo wa vitu vipya vyote wanavijua lakini walikuwa tayari kuendelea kufanya naye kazi, inawezekana hii ndiyo sababu inayowauma.
“Senzo atasaidia vitu vingi sana Yanga kuiboresha timu. Leo nilikuwa nahesabu, sasa ni mwaka wa 21 kila inapofika wakati wa usajili Simba na Yanga inakuwa burudani na hii ndiyo raha kwetu sisi watu wa michezo. Ni lazima mmoja amuumize mwingine sijui kwa nini?
“Mo na Senzo walikwaruzana kidogo, Mo alikuwa anataka Senzo aonyeshe progress (mandeleo) ya kwamba Simba ifanye nini baada ya muda fulani, iingize shilingi ngapi, tatizo timu zetu hapa nchini hazina target (malengo) kuhusu mapato.
“Niliandika makala kwenye Championi, najiuliza usajili unaofanywa na Yanga, pesa anatoa GSM au Yanga? Kama ni GSM anatoa kama msaada au atalipwa na Yanga, kama atalipwa ni lini na kwa mfumo gani? GSM wana nia nzuri na Yanga lakini mambo hayaendi, Yanga wawe na plan (mpango wa kueleweka).
“Mwaka jana nilikuwa Anfield nikarekodi video, sikutegemea kama Liverpool wanaweza kuwa wanauza maji ya kunywa kwenye duka lao, nguo za watoto, kava za simu vitu kibao. Yanga wana jezi nzuri sana lakini hakuna scarf, jifikirie kama maji ya Yanga leo yanauzwa wangapi watanunua?
“Tatizo la klabu zetu nchini hawana pesa zao binafsi hata kama zipo ni za wakubwa, wadhamini. Yanga kulikuwa na Manji alipoondoka ishu ya mishahara ikaanza kuwasumbua, hata GSM yupo leo siku akiwa hayupo itakuwaje? Simba vilevile kuna Mo, siku akiondoka itakuwaje?” amesema Saleh Ally.
“Yanga SC kumpata Senzo ni faida, kutokana na walivyokuwa wanajiendesha walitakiwa kupata mtu kama huyu, lakini najiuliza watamuingizaje kwenye mfumo wao, sababu kwa katiba ya Yanga hawana CEO, labda wampe Senzo ukatibu mkuu ili aweze kufanya majukumu yake.
“Ukisema Senzo kachukuliwa Simba SC ni makosa, sababu yeye na Simba walikuwa wameshashindwana, alikuwa huru kuondoka, aliomba kwenye mkataba mpya aongezewe mzigo, Simba wakasema mzigo huu hatuwezi kulipa. akasema mimi nitaondoka, Yanga wakapata taarifa wakamuwahi.
“Niliongea na Engineer. Hersi nikamwambia katika move zote ulizofanya kuelekea msimu ujao hii ya Senzo ni sahihi zaidi, sababu atakuwa mshauri mzuri, ni mzoefu, ana nafasi ya kumwambia hapa tumepatia hapa tumekosea, tunahitaji kocha wa namna gani, forward wa namna gani."
Leave Comments
Post a Comment