WANACHAMA KLABU ZA KODI WATAKIWA KUWA MABALOZI BORA
Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa TRA, richald Kayombo akitoa elimu ya kodi kwa wanafunzi wa klabu ya kodi wa chuo kikuu cha Dar wakati wa mahafali ya pili ya klabu hiyo yaliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Na Ripota wetu, Michuzi TV
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema, kila mtanzania nchini anawajibu wa kulipa kodi na sio lazima awe mfanyabiashara bali ni kwa kulipa kodi kutokana na bidhaa alizonunua na kudai risiti.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa mahafali ya pili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao ni wanachama wa klabu za kodi (UDTA) ambazo zipo chini ya mamlaka hiyo.
Amesema kila pato analopata mtu anatakiwa kulilipia kodi kwa mujibu wa sheria na kwamba ili kujiridhisha kodi imefika serikalini baada ya kufanya manunuzi ya bidhaa mtu anatakiwa kudai risiti.
"Lengo la kuanzishwa kwa klabu za kodi mashuleni na vyuo vikuu ni kuwezesha vijana kuwa na elimu ya kodi na kutambua umuhimu wake ambao utawafanya kuwa walipakodi wazuri wa baadae kwani bila kulipa kodi tusingekuwa na barabara nchi nzima na kwamba miaka ya nyuma ili uweze kuifikia Bukoba ilikuwa lazima upite katika nchi mbili za Kenya na Uganda lakini sasa hivi tuna barabara nzuri zinazotuwezesha kwenda moja kwa moja bila kupita nchi za wenzetu, amesema Kayombo".
Ameongeza, vijana wote waliojiunga na klabu za kodi wapo katika njia sahihi kutokana na kuwa kodi ni moja ya sababu itakayoiwezesha Tanzania kuwa nchi zilizoendelea kama Ulaya kwani ili nchi iendelee na kuweza kupata mafanikio zaidi ya haya yaliyopo sasa ni lazima TRA ikusanye mapato na ili mapato yakusanywe mamlaka inatakiwa kutoa elimu ya kodi kwa kila mwananchi na sio kuwalazimisha kulipa kodi pasipokuwa na uelewa wa umuhimu wake.
"Siyo kwamba mfanyabiashara akilipa kodi anaonewa, analipa kwa mujibu wa sheria, TRA kazi yake ni kuhakikisha biashara za wafanyabiashara zinaimarika kwa kuwajengea uelewa wa kujua umuhimu wa kulipa kodi, kuwawekea mazingira mazuri ya kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho endelevu yatakayowezesha kutatua changamoto za walipakodi wake, amesema Kayombo.
Amesema ili klabu hizo ziweze kuendelea na kupeleka elimu ya kodi katika maeneo mbalimbali ambako wanachama hao wa klabu za kodi wanakoishi, TRA itakuwa ikiwapa elimu za mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vituo vya kazi vya mamlaka hiyo ili wajifunze kwa vitendo.
Kwa upande wake, Rais wa UDTA, Wiseman Lucas alisema kuwa uwepo wa klabu hizo za kodi mashuleni na vyuo vikuu kutawezesha vijana uelewa wa umuhimu wa kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kuifanya elimu hiyo kumfikia kila mwananchi alieko jirani naye kutokana na kuwa kila mwanachama wa klabu ni balozi ambaye anatakiwa kuipeleka elimu hiyo katika maeneo anayoishi.
Alisema katika matawi 12 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, matawi matano tayari yana wanachama wa klabu za kodi na kwamba lengo lao ni kuyafikia matawi mengi zaidi.
Mwisho.
Previous article
Leave Comments
Post a Comment