KATIBU MKUU WIZARA YA HABARI DK. ABBASI AWAONGOZA WANAHABARI, WASANII KUONJA UTAMU WA RELI YA KISASA
Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Soga.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali amewaongoza wanahabari na wasanii mbalimbali nchini kutembelea Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Dk.Abbasi amewaongoza wanahabari na wasanii hao leo Ijumaa ya Oktoba 16 mwaka huu ambapo lengo kuu la kutembelea mradi huo ni kuona maendeleo ya ujenzi huo na wakati huo huo kushuhudia kwa vitendo kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk.John Magufuli ya kuifungua nchi kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya usafiri ikiwemo ya kujenga reli hiyo ya kisasa ya SGR.
Wakizungumza mara baada ya kujionea maendeleo makubwa ya mradi huo ikiwemo kupanda treni ya kisasa ya majaribio, waandishi wa habari na wasanii hao wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. Magufuli kwa kubuni na kutekeleza mradi huo ambao pia unakwenda kuwaomboa watanzania kiuchumi.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa reli hiyo, Msanii wa muziki wa Singeli Sholo amesema "Sikuwahi kuwaza kama katika miaka yangu hii nitaona kitu cha kisasa kama hiki nilidhani ni vitu vitakuja sisi tushakuwa wazee."
Kwa upande wake msanii amesema sasa anakwenda kuongeza biashara zake zaidi reli hiyo ikianza kufanyakazi huku msanii Kala Jeremire akisisitiza hayo ndio ndio mambo waliyokuwa wakitaka na kuona yanatokea na chini ya Rais Magufuli imewezekana.
"Tunampongeza Rais Magufuli kwa kazi hii nzuri ambayo anaifanya katika nchi yetu,amefanya mambo makubwa ya maendeleo na hiyo ni kwa miaka mitano tu, tuna kila sababu ya kumpa tena miaka mitano mingine afanye makubwa zaidi na wenye akili timamu Oktoba 28 mwaka huu watampa kura kwani anachokifanya sote ni mashahidi,"amesema.
Muigizaji maarufu wa filamu nchini Monalisa amesema yale ambayo yalikuwa yanaonekana katika filamu za Ulaya hatimaye sasa chini ya Rais Magufuli yanaonekana waziwazi na binafsi amejisikia faraja kuona ujenzi wa reli hiyo ya mwendo kasi ukiendelea vizuri.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari na wasanii hao Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kasi ya ujenzi wa reli hiyo ya kisasa inakwenda vizuri na ujenzi umefikia asilimia 90 kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na hatua itakayofuata itakuwa ya kuanza kwa majaribio kwa lengo la kukagua mifumo mbalimbali.
"Yanayoendelea kwenye sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro kwa sasa ni 'finishing'.Baada ya kukamilika hatua hiyo, majaribio ya awali yataanza mara moja kama mambo yataenda vizuri tutaanza majaribio na ieleweke hatua ya kupitisha treni ni ya mwisho kabisa,"amesema Kadogosa.
Kuhusu mifumo amesema itahusisha pia makubaliano ya kisheria kati ya TRC na mamlaka mengine kama vile Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) ili kujiridhisha na kutoka na maamuzi kadhaa, ikiwemo gharama za nauli.
Pia katika kuelekea huko amesema tayari TRCimeanza mazungumzo na wakala wa serikali mtandao, (e-goverment) kwa ajili ya kuona namna gani watashirikiana kusimamia masuala yanayohusu teknolojia kwenye ukatishaji tiketi.
Kuhusu gharama za ujenzi wa mradi huo amesema utagharimu Sh.trilioni 7.026 na fedha hizo zote zinatolewa na Serikali wakati kwa upande wa ajira amesema wafanyakazi wa kada mbalimbali 14,000 wamepata ajira na kati hizo asilimia 90 ni wazawa.
Kadogosa amesema ajira nyingine zimepatikana kwenye mahitaji ya huduma mbalimbali muhimu za kijamii, vikiwemo vyakula na vinywaji, mahitaji ya malighafi za kujengea ambapo zaidi ya kampuni 1,600 zimepata zabuni za kusambaza mahitaji hayo.
Leave Comments
Post a Comment