RUVUMA YAPATIWA BILIONI 4.5 KWA AJILI YA SEKTA YA AFYA
SERIKALI imesema, inaendelea kuimarisha na kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza dawa na vifaa tiba kwenye zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zake ili kuhakikisha hakuna mwanachi atakayepoteza maisha kwa kukosa huduma ya matibabu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Jairy Khanga, wakati akiongea na wananchi wa vitongoji vitatu vya Madaba (A) Madaba(B) na Changarawe kijiji cha Liula wanaoendelea kupata matibabu baada ya kunusurika kifo kufuatia kukumbwa na mlipuko wa kuhara damu baada ya kunywa togwa inayodhaniwa kuwekwa sumu.
Dkt Khanga alisema, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuri imeupatia mkoa wa Ruvuma zaidi ya bilioni 4.5 ambazo zimetumika kuimarisha na kuboresha huduma za Afya katika maeneo mbalimbali.
Alisema, katika awamu zote serikali ya awamu ya tano ndiyo inayoongozwa kwa kupeleka fedha za kuimarisha sekta ya afya katika mkoa wa Ruvuma ambapo mbali na fedha imeleta madaktari 24 ambao wamepelekwa katika wilaya zote za mkoa huo na kuwataka wananchi kuendelea kuiamni na kuiunga mkono serikali yao iliyopo madarakani.
Aidha Dkt Khanga na wataalam kutoka Hospitali ya wilaya Songea wamekwenda katika kijiji hicho kwa lengo la kutoa elimu ya Afya,kudhibiti kuenea kwa madhara pamoja na kutoa majibu ya vipimo vilivyochukuliwa kwa ajili ya kutambua aina ya sumu iliyowekwa katika kinywaji hicho.
Dkt Khanga alisema,kimsingi mlipuko huo umetokana na uchafu katika maandalizi ya tongwa kwani hayakuzingatia kanuni za usafi ndiyo chanzo cha kupata maradhi yanayofahamika kwa kitaalam(Bacillary Dysentry).
Dkt Khanga alisema,ugonjwa wa kuhara na kuharisha damu mara nyingi usababishwa na bakteria anayefahamika kwa jina la Shigella ambaye utokea katika maeneo yenye ukosefu wa maji safi na salama,watu wasiokuwa vyoo bora,wasionawa mikono kwa sabuni mara wanapotoka kujisaidia,na kundaa chakula katika mazingira bila kuzingatia usafi.
Kwa mujibu wa Dkt Khanga, mtu(watu)wanapokosa vyoo au kujisaidia porini kinyesi uzalisha Inzi ambao uingia katika chakula na vyombo na kuacha uchafu ambao ni hatari kwa afya ya binadamu.
Alitaja dalili za kuharisha damu ni mtu kupata homa inayoambatana na baridi kali,maumivu ya kichwa,kutapika,kuharisha na kichwa kuuma ambapo madhara yake ni kuishiwa maji mwilini na kama mgonjwa hatapata dawa ni rahisi kupoteza maisha.
Adha, amewapongeza wahudumu wa Afya wa zahanati ya Matimila na Liula kwa kazi kubwa waliyoifanya kuokoa maisha ya wananchi kwani mara baada ya kutokea mlipuko huo walifanya kazi usiku na mchana bila kuchoka.
Hata hivyo,amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa na vyoo bora na kuzingatia kanuni bora za Afya ili kuepuka magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu na kuharisha.
Awali Mganga mkuu wa wilaya ya Songea Dkt Geofrey Kihaule alisema, jumla ya watu 102 walipata ugonjwa wa kichwa na kuhara damu ambapo hadi sasa hakuna aliyepoteza maisha.
Dkt Kihaule alisema, kazi iliyofanyika mara baada ya kufika katika kijiji hicho ni kutoa elimu ya afya ili wananchi waelewe namna ya kuchukua hatua pale milipuko inavyotokea na kuwaondoa hofu kuhusiana na tukio hilo na Imani ya kishirikina na kuwafuatilia wale walio karibu na wagonjwa ili nao kufahamu afya zao na kuwapa kinga ili wasipate maradhi hayo.
Baadhi ya wananchi wameipongeza Serikali kupitia mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma kwa kuchukua hatua ya haraka kukabiliana na mlipuko huo hali iliyosaidia kuokoa maisha ya watu walioathirika na ugonjwa huo.
Mmoja wa wananchi Moses Luambano alisema, kama wataalam wangechelewa kufika kwa wakati ni dhahiri kuwa madhara yangekuwa makubwa zaidi kwa watu kupoteza maisha.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Jairy Khanga akimjulia hali mkazi wa kitongoji cha Madaba B kijiji cha Liula wilaya ya Songea anayeendelea kupata matibabu baada ya kupata na ugonjwa wa kuharisha damu kutokana na kunywa togwa inayodhaniwa kuwa na sumu kwenye sherehe kijijini hapo.
Leave Comments
Post a Comment