UMAKINI NA TAHADHARI KWA SASA NI MUHIMU
BADO mambo ni magumu kwa sasa na hii ni kutokana na janga la Virusi vya Corona ambavyo vinaendelea kuitikisa dunia kiujumla.
Sio shule, soka na mikusanyiko isiyo ya lazima kwa nchi nyingi haijaruhusiwa na hii ni kutokana na janga hilo.
Kupitia mitandao ya kijamii wachezaji wengi wamekuwa wakiandika kuwa wanatamani kurejea uwanjani na hawa ni wale wa Bongo na Ulaya.
Kutokana na janga hili hapa Bongo makocha wamejitahidi kutoa program kwa wachezaji wao kuhakikisha wanaendelea kulinda viwango vyao.
Ligi Kuu Bara pamoja na ligi nyingine bado haijafahamika ni lini rasmi zitarejea kwa sasa hivyo kikubwa kuwa na subira pamoja na dua.
Wachezaji kadhaa wamekuwa wakionekana wakiendelea na mazoezi yao binafsi kama kawaida bila tatizo lolote.
Lakini tunaamini wachezaji wengi wa kibongo watakuwa wanazingatia yale ambayo wamekuwa wakielezwa kufanya na makocha wao ili kulinda viwango vyao.
Wachezaji wapo majumbani lakini sasa hivi ni wakati wao muafaka wa kujituma na kuendelea kulinda viwango vyao ili ligi itakaporejea basi mambo yaweze kwenda sawa.
Wachezaji ni watu ambao wanajielewa na wanatambua ni kitu gani wanatakiwa kufanya kipindi hiki kwa manufaa yao binafsi pamoja na klabu zao.
Huko waliko wachezaji sasa wanatakiwa kujituma kwa bidii na kuweka malengo ligi itakaporejea tunaweza kushuhudia mambo mengi ambayo hayakutarajiwa.
Wachezaji wasipokuwa makini na kuzingatia suala la kujitunza na kufanya mazoezi itakuwa ni jambo rahisi zaidi kwa makocha ligi itakaporejea kuwachuja vizuri hasa kuelekea katika msimu mpya wa ligi.
Ligi itakaporejea ni wazi klabu zitakuwa zinaelekea katika kipindi cha usajili wake na nyakati za mwisho ndiyo sehemu muafaka kwa wachezaji kuonyesha kile walichonacho ili makocha waweze kutoa uamuzi sahihi kwa ajili ya usajili mpya.
Kuna wachezaji wamekuwa na tabia ya uvivu wa kufanya mazoezi wanapokuwa na timu, lakini wakati kama huu unaweza kujiuliza je wale wachezaji kipindi hiki cha Corona wanafanya mazoezi kweli au ndiyo wanaendelea na mambo yao bila kuzingatia kazi zao.
Soka ni mchezo ambao unachezwa hadharani hivyo ligi itakaporejea kila mmoja ubora wake utaonekana pale na kipindi hiki makocha watapata wachezaji sahihi sababu Corona kwa upande mmoja au mwingine imekuwa kama kipimo kwa wachezaji kuona kweli wanaweza kuzingatia program walizopewa au ndiyo wataendelea na ratiba zao binafsi.
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment