BEFORE I DIE SEHEMU YA KWANZA
Mzee Vincent Benard akiwa ameongozana na mkewe Bi Gloria Benard pamoja na binti yao Sarah walijawa na nyuso za furaha kwa kumpokea tena mtoto wao kipenzi Innocent ambaye ni mtoto wa tatu na wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto watatu ambao bwana na bi Vincent Bernard walijaliwa kuwapata.Mtoto wa kwanza kuzaliwa alikuwa ni Edson ambaye kwa sasa ni mfanya kazi katika shirika moja lisilokuwa la kiserikali linaloshughulika na masuala ya elimu ya ukimwi kwa umma.Wa pili ni Sarah ambaye ni mwandishi wa habari katika televisheni ya Taifa na wa mwisho ni Innocent ambaye leo hii anarejea nyumbani akitokea Marekani baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza ya uchumi na fedha katika chuo kikuu cha Columbia.Familia hii ni moja ya familia ambazo tunaweza kusema kuwa ni familia bora zenye kujiweza kiuchumi.Mzee Vincent alimiliki kiwanda cha kutengeneza magodoro na kiwanda cha kutengeneza maji ya kunywa. vile vile alikuwa na hisa za kutosha katika viwanda kadhaa kikiwemo kiwanda cha sigara na saruji.
Ni vigumu kuelezea furaha waliyoipata baada ya Innocent kutokeza katika sehemu ya kusubiria wageni.Walimkumbatia kwa furaha na kumkaribisha tena nyumbani.Innocent au Inno kama walivyozoea kumwita hakukaukiwa tabasamu kama ilivyo kawaida yake.Ilikuwa ni furaha ilioje kuwasili tena nyumbani baada ya miaka kadhaa ya kuwa mbali na nyumbani.
“Karibu tena nyumbani mwanangu” Mzee Vincent akasema
“Ahsante baba nimeshakaribia.Mbona kaka Edson simuoni hapa? Nilifikiri mtakuwa naye.” Inno akasema
“Edson amepata safari ya dharura kwenda mikoani katika shughuli zao,ila alipenda sana kuungana nasi kuja kukupokea.” mama yake akasema
Saraha akamsaidia Inno kusukuma mabegi yake hadi katika gari lao halafu wote wakaingia garini na kuondoka kuelekea nyumbani.
“Ama kweli Marekani kuzuri.Inno umebadilika.Umependeza sana mdogo wangu” Sarah akasema huku akicheka kwa furaha.Innocent kijana asiyekaukiwa tabasamu akajibu.
“Na wewe Sarah bado hujaacha utani wako tu.”
“Siongei utani.Ni kweli kabisa umependeza sana mdogo wangu.Inaonekana hali ya huko imekukubali.Halafu mimi nikafikiri utakuja na wifi mzungu”
Wote mle ndani ya gari wakaangua kicheko kikubwa kwa utani ule wa Sara.
“Huyo mzungu nitampeleka wapi? Unafikiri mzee Vincent atakubali mwanae aoe mzungu na kuacha wasichana warembo wenye maadili ya kiafrika? Thubutu! “ Inno akaendeleza utani na kumfanya mzee Vincent acheke kwa nguvu.
“Ndiyo maana nakupenda mwanangu.Hapo umenena.Sioni sababu ya kuacha mamilioni ya mabinti warembo wa kiafrika wenye sifa na maadili ya kiafrika na kwenda kuoa mtu wa mbali ambaye hayuko tayari kufuata mila na desturi zetu.Hebu muangalieni mama yenu jinsi alivyo mzuri,ule uzuri asilia wa kiafrika.Ana umbo la mwanamke wa kiafrika.Sura pana yenye weusi wa kung’aa,macho makubwa yenye kurembua,miguu ambayo nyie vijana mnaiita ya bia” Kicheko kikubwa kikaanguka ndani ya gari.
“lakini baba hizi ni zama za utandawazi.Haijalishi ni mtu wa namna gani unahitaji kumuoa au kuolewa naye .Kitu cha msingi muwe mnapendana kwa dhati” Sarah akasema
“Sikatai mwanangu.Hayo unayosema ni ya kweli.Lakini pamoja na hayo ni lazima tuendelee kulinda mila na desturi zetu sisi kama waafrika.Iwapo utapata bwana wa kizungu ni wazi hautauthamini utamaduni wako tena.Malezi,makuzi ya wenzetu ni tofauti na sisi.Hebu angalia kwa sasa sijui wanashinikiza dunia nzima ihalalishe hivi vitendo vichafu visivyompendeza Mungu ambavyo ni kinyume na maadili yetu ya kiafrika.Siwakatazi na wala siwaingilii katika masuala yenu ya mahusiano lakini nisingependa mwanangu yeyote aoe au kuolewa na mtu wa mataifa ya kigeni na hasa huko Ulaya na marekani.Nitafurahi sana kama wanangu wote wataoa na kuolewa humu humu ndani ya nchi yao.”
Maongezi yalikuwa matamu na hatimaye wakajikuta wamewasili nyumbani.Giza tayari likwishatanda.Mabegi ya Innocent yakashushwa na kupelekwa ndani halafu kwa furaha kubwa Inno akakaribishwa ndani.
“Karibu nyumbani mwanangu” akasema mama yake.
“Nimeshakaribia mama.Hivi yule mbwa wangu Pura bado yupo? Inno akauliza
“Mbwa wako bado yuko tena anazidi kunawiri siku hizi.”
“Mama siwezi kuingia ndani hadi kwanza nikamsalimu Pura.Nimemnunulia sabuni nzuri ya kuogea.”
“ahahahahaaaa..mambo ya wazungu hayo yaani hadi mbwa unamnunulia sabuni ya kuogea! “ mama yake akasema huku akicheka.
“mama nampenda sana mbwa wangu ndiyo maana nikaona ni bora naye nimletee zawadi”
Innocent akaelekea katika banda la kufugia mbwa anakokaa mbwa wake ampendaye sana Pura.Japokuwa ilipita miaka takribani sita lakini mara moja Pura alimfahamu Inno akamchangamkia na kumrukia kwa furaha.Baada ya kuhakikisha mbwa wake yuko salama na mwenye afya njema akaufunga mlango na kurudi ndani.
“Shikamoo kaka” Innocent akasalimiwa na dada mmoja mwembamba mrefu wastani aliyejifunga kitambaa kichwani aliyekuwa amesimama hapo sebuleni akiwa na sinia la kubebea vinywaji alivyokuwa amewapelekea Bwana na Bi Benard.
“Maharaba dada yangu,habari za hapa? Innocent akajibu huku akitabasamu na kumuangalia yule dada ambaye hakumuacha pale nyumbani wakati anaondoka kuelekea Marekani kwa masomo.
“Habari za hapa nzuri,pole na safari”
“Nimeshapoa” Innocent akajibu huku akiunyoosha mkono ili asalimiane na yule dada.
“wewe Grace hebu haraka nenda kamuandalie Innocent maji ya kuoga halafu mwambie na sabrina muanze kuandaa meza haraka .” Ilikuwa ni sauti ya amri ya mama yake Inno
Binti yule akaondoka haraka baada ya kupokea amri ile.Innocent akamgeukia mama yake na kumtazama kwa mshangao.
“Innocent , wakati unaondoka hapa nyumbani kwenda masomoni hukuacha msichana wa kazi hapa ndani lakini kwa sasa kuna wasichana wawili tunaishi nao.Mmoja ni huyu Grace ambaye ametoka hapa sasa hivi ambaye ni binti tuliyemchukua atusaidie kazi za hapa nyumbani kama unavyojua baada ya Sarah kuanza kazi katika televisheni ya Taifa mama yako alizidiwa sana na kazi.Mwingine anaitwa Sabrina, yeye alikuwa ni mtoto wa Michael yule mfanyakazi wetu wa shambani ambaye nilikutaarifu katika simu kuwa alifariki dunia.Kwa kuwa niliishi naye vizuri sana yule bwana nikaona ni bora nimchukue binti yake wa pekee niishi naye hapa kwa sababu alihitaji uangalizi maalum kwani ni mlemavu wa ngozi yaani albino”Mzee Vincent akamfahamisha mwanae Inno.
“Ouh ! nafurahi kusikia hivyo baba.Unajua ni vizuri kuwa na familia kubwa .Familia inapokuwa na mchanganyiko mkubwa wa watu basi inakuwa na furaha zaidi.” Innocent akasema
Mrs Benard alikuwa amefura kwa hasira wakati mumewe akimfahamisha Innocent kuhusu wasichana wawili wanaoishi nao mle ndani.
“Nakwambia baba Eddy waondoe hawa wasichana humu mwangu,sitaki mwanangu akaribiane nao kabisa.Usipowatoa mimi nitawaondoa kwa nguvu” Akasema kwa hasira
“kwani mama kuna tatizo gani kuishi nao katika jumba hili kubwa? Innocent akauliza
“Baba yako ametuletea balaa humu ndani.Kaenda kamleta yule albino humu ndani.Hajui kama watu wale wana mikosi.halafu huyu mwingine ni muathirika wa ukimwi .Huoni kama nyumba yetu imeingiliwa? Mwanangu naomba ukae mbali nao kabisa hawa wasichana.”
Innocent akabaki mdomo wazi akishangaa
“mama ! kumbe hilo ndilo tatizo ? Mimi nilidhani labda ni tatizo kubwa lakini kama ni hilo tu basi hakuna tatizo lolote katika kuishi nao.Mzee Michael alikuwa ni kama ndugu yetu aliyekuwa akitulimia na kutulindia shamba letu kwa hiyo kukaa na binti yake hapa tena ambaye anahitaji uangalizi maalum ni jambo la busara sana.Tunahitaji kumuenzi yule mzee.Tunahitaji kumtunza mtoto wake bila ubaguzi wowote.Japokuwa ametoka katika familia ya kimasikini tofauti na sisi lakini hakuna sababu yoyote ya kumtenga.na hata huyu Grace ambaye unadai ameathirika na ugonjwa wa ukimwi,hatuna budi kumtunza na kumlea.Kuathirika na ugonjwa huu si sababu ya kunyanyapaliwa au kutengwa.Mama naomba tuwaonyeshe upendo wajisikie kama ni sehemu ya familia hii”
Innocent akasema na mara Grace akaingia mle sebuleni
“kaka maji ya kuoga tayari.”
“Ahsante Grace” Innocent akajibu huku akitabasamu na kumfanya mama yake anune.
“Nenda kaoge mwanangu tuje tujumuike pamoja kwa chakula cha usiku tufurahie kurejea kwako” mzee Vincent akasema
Innocent akaelekea chumbani kwake akabadili nguo na kwenda kuoga .Kisha oga akarudi tena sebuleni kujumuika na familia yake kwa chakula cha usiku.
“Mwanangu nimekuandalia sherehe kubwa ya kukukaribisha nyumbani jumamosi ijayo..”mzee Vincent akasema
“Nashukuru sana baba.Lakini sioni kama kuna umuhimu wa kufanya sherehe yoyote kwa ajili ya kurudi nyumbani na kutumia fedha nyingi wakati kuna maelfu ya watu wanazihitaji fedha hizo kwa ajili ya elimu ya watoto wao,wengine matibabu n.k.”
Huku akitabasamu Mzee Vincent akajibu
“mwanangu nalifahamu hilo.nafahamu una moyo wa kusaidia wengine toka ukiwa mdogo.lakini kuna kitu ninataka kukifanya siku hiyo ya jumamosi na ndiyo maana nikaamua kuandaa sherehe hiyo .”
“hakuna shida baba,nilikuwa najaribu tu kukumbusha kwamba tunapotumia fedha kwa mambo yasiyo ya lazima tukumbuke kuna watu masikini wanasumbuka usiku na mchana kutafuta fedha kama hizo kwa ajili ya mahitaji yao muhimu.Halafu mbona akina Grace siwaoni hapa?
Sarah na mama yake wakatazamana halafu Sarah akajibu
“Wana chakula chao jikoni”
“Ina maana wao hawajumuiki nasi hapa mezani? Innocent akauliza
“wao wanakula jikoni” mama yake akajibu
“No ! That’s not fair.Waiteni wajumuike nasi hapa,nao ni sehemu ya familia.” Innocent akasisitiza
“Waende wapi? Wao chakula chao kiko jikoni.Kwani kuna tatizo gani? Mama yake akasema kwa sauti yenye ukali kidogo ndani yake.
Innocent hakujibu kitu akachukua chakula katika sahani yake akainuka na kuelekea jikoni.
TUKUTANE SEHEMU IJAYO…………
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment