BEFORE I DIE SEHEMU YA 2
“Mwanangu nimekuandalia sherehe kubwa ya kukukaribisha nyumbani jumamosi ijayo..”mzee Vincent akasema
“Nashukuru sana baba.Lakini sioni kama kuna umuhimu wa kufanya sherehe yoyote kwa ajili ya kurudi nyumbani na kutumia fedha nyingi wakati kuna maelfu ya watu wanazihitaji fedha hizo kwa ajili ya elimu ya watoto wao,wengine matibabu n.k.”
Huku akitabasamu Mzee Vincent akajibu
“mwanangu nalifahamu hilo.nafahamu una moyo wa kusaidia wengine toka ukiwa mdogo.lakini kuna kitu ninataka kukifanya siku hiyo ya jumamosi na ndiyo maana nikaamua kuandaa sherehe hiyo .”
“hakuna shida baba,nilikuwa najaribu tu kukumbusha kwamba tunapotumia fedha kwa mambo yasiyo ya lazima tukumbuke kuna watu masikini wanasumbuka usiku na mchana kutafuta fedha kama hizo kwa ajili ya mahitaji yao muhimu.Halafu mbona akina Grace siwaoni hapa?
Sarah na mama yake wakatazamana halafu Sarah akajibu
“Wana chakula chao jikoni”
“Ina maana wao hawajumuiki nasi hapa mezani? Innocent akauliza
“wao wanakula jikoni” mama yake akajibu
“No ! That’s not fair.Waiteni wajumuike nasi hapa,nao ni sehemu ya familia.” Innocent akasisitiza
“Waende wapi? Wao chakula chao kiko jikoni.Kwani kuna tatizo gani? Mama yake akasema kwa sauti yenye ukali kidogo ndani yake.
Innocent hakujibu kitu akachukua chakula katika sahani yake akainuka na kuelekea jikoni.
ENDELEA…………………………….
“jamani .mbona hamji kujumuika nasi kule mezani?” Innocent akawauliza grace na Grace waliokuwa wamekaa wakipata chakula jikoni.
“Sisi chakula chetu huwa kinabaki huku jikoni.Haturuhusiwi kukaa mezani na mama” Grace akajibu.
Innocent akatabasamu kama kawaida yake akamsogelea Sabrina na kumpa mkono.
“Naitwa Innocent.Sidhani kama unanikumbuka kwa sababu mara ya mwisho kukuona ulikuwa mdogo nadhani ulikuwa darasa la nne au la tano.Pole sana kwa msiba wa mzee .Mzee Michael nilikuwa namchukulia kama baba yangu na nilikuwa naelewana naye sana.” Innocent akasema na kumfanya Sabrina atokwe na machozi huku akimshangaa .Toka amekuja katika nyumba ile hakuna hata siku moja ambayo ameweza kuongea na mtu wa familia hii zaidi ya mzee Vincent kwa upole na heshima ya ajabu namna hii.Siku zote imekuwa ni kugombezwa na kufokewa.
“nyamaza kulia Sabrina.Ni kazi ya Mungu ambayo sisi wanadamu hatuna budi kuikubali.” Innocent akambembeleza.Sabrina hakuwa akilia kwa sababu ya kukumbushwa kifo cha baba yake bali kwa jinsi Innocent alivyomsalimia na kuongea naye kwa upole na ucheshi huku macho na sauti yake vikionyesha upendo wa hali ya juu.
Sabrina akafuta machozi na kumtazama Inno usoni.
“Ahsante sana kaka Innocent.Pole na safari”
“Nimekwisha poa.Nashukuru Mungu baada ya miaka sita sasa nimerudi nyumbani.Nadhani tutaendelea kuwa wote hapa kwa sababu sifikirii tena kwenda kusoma nje ya nchi labda hapo baadae sana.”
“kaka Innocent kuna kitu umekuja kuchukua huku jikoni? Grace akauliza baada ya kuona Inno hakuwa na dalili za kuondoka mle jikoni.
“hapana Grace nimekuja huku tule wote. mimi sijazoea kukaa mezani na kula bila maongezi .Kule mezani tunakula kimya kimya na hata mkiongea ni kuhusu maisha binafsi.Mimi nataka kula kwa uhuru halafu nahisi chakula cha huku ni kitamu kuliko hata cha kule mezani” Innocent akasema na kuwafanya Grace na grace waangue kicheko kinachosikika hadi sebuleni na kumfanya Mrs Benard kutoka haraka na kuja kuangalia.Alipoingia jikoni akakuta Innocent amekaa na akina Grace wakiongea na kucheka kwa furaha.Mara tu alipoingia maongezi na vicheko vikakoma.Mrs benard akaukunja uso na kusonya kwa hasira halafu akaondoka.
“Msijali sana,mama yangu ndivyo alivyo.Jitahidini kumzoea na kumvumilia” Innocent akasema na kuwafanya grace na Grace kutabasamu.
“I have to change things here.Ni lazima niwasaidie wasichana hawa masikini ili wawe na maisha mazuri na yenye furaha kama tulivyo sisi.Najua wana wakati mgumu sana kuishi na mama yangu.Ninamfahamu mama yangu vizuri.Hana roho nzuri.Nitafanya kila niwezalo kuwasaidia.
Baada ya kula chakula wakaendelea na maongezi yaliyotawaliwa na utani na vicheko.Laiti kama ungewakuta wakiongea ungedhani labda ni watu waliokaa pamoja zaidi ya miaka kumi kumbe ni leo tu wameonana.Wakati wakiendelea na maongezi yao jikoni ghafla Sarah akaingia.
“ Grace mnacheka huku wakati kule tumemaliza kula chakula.Hebu nenda kaondoe vyombo haraka .Na wewe Sabrina kwa nini usianze kuosha vyombo .Inuka mara moja uanze kazi.” Sarah akasema kwa ukali.
“Sawa dada Sarah” Grace akasema na kuondoka haraka kuelekea sebuleni kukusanya vyombo walivyolia chakula.
Baada ya Grace na Sabrina kuondoka mle jikoni Sarah akamuangalia Innocent kwa macho makali .
“Vipi kuna tatizo? Mbona unaniangalia hivyo? Innocent akauliza
“Yes lipo tatizo.Hebu acha uzungu uzungu wako uliotoka nao Marekani.Hawa wasichana huwa hawachangamani na sisi hata siku moja.Tena usijaribu kuwaozea”
Huku akicheka kichini chini Innocent akasema
“Sister mnavyofanya si vizuri.Hawa ni binadamu na isitoshe wana matatizo.Tunatakiwa tuishi nao kwa upendo mkubwa.Ikiwa tutaanza kuwanyanyapaa haitapendeza” Mara Grace akaingia mle jikoni akiwa na sinia la vyombo.Innocent akamshika mkono dada yake wakatoka.
* * * *
Mlio wa saa ya ukutani ndio ulimstua toka katika usingizi mzito.Akafunua shuka na kuangalia saa.Ilikuwa ni saa mbili za asubuhi.
“Leo nimelala usingizi ambao sijaulala kwa miaka kadhaa.Kweli nyumbani ni nyumbani.” Akawaza Innocent huku akijinyoosha nyoosha pale kitandani.
“Ngoja niendelee kulala kidogo mpaka saa tatu ndipo niamke. No ! I have to wash Pura” haraka haraka akainuka akavaa na kutoka nje.Kabla hajafunga mlango akasikia kelele za kufoka.Mama yake alikuwa akifoka maeneo ya jikoni.Taratibu akapiga hatua na kuelekea huko.
“Nimekwambia mwaka huu ni lazima utaondoka tu.Sitaki uiambukize familia yangu maradhi yako.Na kama baba Edson hataki kukuondoa humu ndani nitahama na kumuachia nyumba.Siwezi kuishi na mwathirika wa ukimwi ndani mwangu” mama yake Innocent alikuwa akimfokea Grace.Maneno yale yakamchoma sana Inno na hasa pale alipomuona Grace ameinama chini akilia na pembeni yake kukiwa na sahani ya udongo iliyovunjika.Huruma ikamwingia .
“Tena naomba usinililie hapa.Inuka sasa hivi ukaendelee na kazi.Na sahani yangu uliyoivunja utailipa” Mrs Benard akaendelea kufoka kwa nguvu.
“mama its enough” Innocent akaingilia kati.Mama yake akasimama na kumuangalia kwa macho makali.
“Mama kwa nini unawafanya hivi ? this isn’t right.Hawa ni wenzetu na ni lazima tuwapende na kuwaona ni sehemu ya familia yetu.” Innocent akasema huku akiinama na kuushika mkono wa Grace akamwinua
“Inuka Grace.” Akamshika mkono na kumpeleka chumbani kwake.
“Hebu pumzika kwanza humu chumbani kwako hadi baadae.halafu usilie sana utaumwa na kichwa.Mama yangu ndivyo alivyo.Unatakiwa uwe mvumilivu sana kuishi naye”
“kaka Innocent mimi nimevumilia lakini sasa naona nimeshindwa.Mama kila siku ananitukana kupita maelezo.Au kwa vile sina wazazi? Grace akasema kwa uchungu huku akilia.
“hapana usiseme hivyo Grace.Namfahamu mama yangu ni mkorofi sana.Nitaongea na baba ili tuone tutafanya nini kuwasaidia wewe na Sabrina”
“Kaka Innocent kwa mateso ninayoyapata katika hii nyumba ni bora niende nikateseke mtaani.Ninachoomba niombee nauli kwa baba ili niondoke hapa na kwenda kokote kule nikaishi.”
Grace akaendelea kulalamika huku uso wake umejaa machozi.Aliongea toka moyoni.Ni wazi alikuwa ameumia mno na maneno aliyoambiwa na Mrs benard.
“hapana usiseme hivyo Grace.Hautaenda sehemu yoyote ile,wewe utaishi katika nyumba hii miaka yote.Jihesabu ni mmoja kati ya wana familia hii.Naomba futa kabisa mawazo ya kuondoka katika nyumba hii.Kama walikuwa wakiwanyanyasa na kuwadharau ni wakati sipo.lakini kwa sasa hakuna mtu atakayethubutu kufanya hivyo tena nikiwa hapa nyumbani.Pumzika Grace tutaongea baadae”
Innocent akatoka mle chumbani kwa Grace na mara akakutana na mama yake akiwa amefura hasira.
“Naona sasa wamepata mwokozi wao” akasema Mrs Benard kwa dhihaka.
“Mama naomba niwe wazi.Mnavyowatendea hawa wasichana si vizuri.”
Mama yake hakujibu kitu akaondoka zake.Innocent akelekea katika banda anamolala mbwa wake Pura akamtoa na kumuogesha halafu akarudi ndani akaoga akapata chai na kuamua kwenda kupumzika bustanini..Akiwa pale bustanini mara Grace akatokea.
“Ouh Grace karibu”
“kaka Innocent samahani kwa kukusumbua.Nimekuja kukuuliza kama una nguo za kufua nikakufulie.”
Huku akitabasamu ,Inno akajibu.
“Grace nashukuru lakini nitazifua mwenyewe.Tafadhali pata muda wa kupumzika”
“Usijali kaka Innocent.Kama zipo nipe nikufulie kwani mama alisema tuchukue nguo zako tufue pia”
“Ina maana hata Sarah huwa mnafua nguo zake? Inno akauliza
“Ndiyo.Hata nguo za dada Sarah pia huwa tunafua.”
Innocent akakaa kimya halafu akasema.
“Grace nenda tu kapumzike.Nina nguo chache lakini nitazifua kesho mimi mwenyewe”
Grace akaondoka na kumwacha Innocent peke yake bustanini.
“Wasichana hawa wanatumikishwa namna hii kiasi kwamba hawana hata muda wa kupumzika na bado wanaendelea kunyanyaswa na kubaguliwa.I must stop this”
* * * *
Ni siku ya nne tangu Innocent arudi toka Marekani .Siku hii ya Jumamosi baba yake alikuwa amemuahidi kumfanyia sherehe ya kumkaribisha tena nyumbani.Ni sherehe iliyoandaliwa kwa siri japokuwa yeye Innocent alidokezwa kuwa itakuwa ni sherehe ndogo tu yenye kujumuisha watu wachache.
Saa kumi na mbili za jioni akiwa ndani ya suti nzuri nyeusi akaongozana na baba na mama yake pamoja na dada yake Sarah wakaingia garini na kuondoka kuelekea mahala inakofanyikia sherehe.
Lamona palace ni ukumbi mkubwa na wa kisasa kwa ajili ya semina hafla na sherehe mbali mbali.Ni katika ukumbi huu sherehe ya kumkaribisha nyumbani Innocent inafanyikia.Tayari wageni waalikwa wamekwisha wasili na waliokuwa wakisubiriwa ni Mr benard na familia yake.Mara tu walipoingia ukumbini ukumbi wote ukalipuka kwa makofi na vigere gere.Innocent akapatwa na mshangao mkubwa.Hakutegemea kama sherehe ya kukaribishwa kwake nyumbani ingekuwa kubwa namna ile.alitegemea sherehe ndogo yenye watu wachache lakini kwa umati alioukuta mle ukumbini akasimama na kushika mdomo wake kwa mshangao.Alihisi kuishiwa nguvu .Huku akitabasamu Mr Benard akamshika mkono na kumuongoza kuelekea meza kuu iliyoandaliwa maalum kwa ajili yao.
Sherehe ikafunguliwa na watu wakaanza kuburudika kwa vinywaji na ndipo Mr benard alipopewa nafasi ya kuongea.
“Ndugu zangu,wageni waalikwa,mabibi na mabwana.Nakosa neno kubwa la kuwashukuru kwa kuacha shughuli zenu leo hii na kuja kuungana na familia yangu katika sherehe hii ya kumkaribisha nyumbani kijana wetu Innocent aliyekuwa akisoma nchini Marekani.Ujio wenu jioni hii ya leo unaonesha ni jinsi gani mlivyotuthamini sisi kama familia.Tunasema Ahsanteni sana.Sina mambo mengi sana ya kusema kwani mengi yamekwisha semwa ila ningependa nitumie nafasi hii kutangaza jambo moja kwenu wote.”
Ukumbi wote ukakaa kimya kabisa kumsikiliza mzee huyu.
“Si kitu cha kuficha kuwa kwa sasa mimi na mke wangu umri umesogea sana na kwa maana hiyo tunahitaji muda mwingi zaidi wa kupumzika baada ya kazi ngumu tuliyokwisha ifanya kwa miaka mingi.Nimekuwa na majukumu ya kusimamia miradi na kampuni zote zilizoko chini ya familia yangu.Napenda nikiri kuwa hii ni kazi ngumu na bila usaidizi wa karibu basi hakuna ufanisi utakaopatikana.Ninachotaka kukisema hapa ni kwamba kutokana na kuzidiwa mno na majukumu na hivyo kukosa hata muda wa kupumzika,nimeonelea niyagawe majukumu ili walau nipate wasaa wa kupumua.Napenda sasa nitamke kuwa kampuni ya kutengeneza maji ya kunywa ya Benardo ambayo kwa siku za hivi karibuni ufanisi wake umeshuka sana kwa sasa itakuwa chini ya usimamizi wa kijana wangu Innocent benard.”
Ukumbi wote ukalipuka kwa kelele za kushangilia.
Hizi zilikuwa ni habari njema mno kwa wafanyakazi wote wa kampuni hii.Kampuni hii ilikuwa ikiyumba baada ya kukosa usimamizi thabiti.Kupata meneja mpya tena kijana msomi kama Innocent ilikuwa ni faraja kubwa sana kwa wafanyakazi waliokuwa wana wasiwasi na ajira zao iwapo ingetokea kampuni ile kufungwa.
Innocent akapatwa na mstuko mkubwa.Hakuwa ametegemea kama angeweza kupewa kampuni kubwa kama ile aisimamie.Alipomaliza masomo yake nchini Marekani angeweza kubaki na kufanya kazi huko lakini alitambua umuhimu wa kurudi nyumbani na kusimamia miradi ya familia.Aliinama na kushika kichwa kwa mshangao.Kwa jinsi watu walivyoshangilia walizidi kumchanganya akili kwani japokuwa hawamjui lakini walionekana kuwa na imani na matumaini makubwa kwake ndiyo maana walifurahi na kushangilia
Baada ya Mr benard kumaliza kuongea akamkaribisha Innocent aweze kuwasalimu wageni na kuongea machache.Ukumbi wote ukawa kimya kumsikiliza .Huku akitabasamu akaanza kwa kusema
“Ndugu wageni waalikwa mabibi na mabwana ,nakosa neno la kuweza kuelezea furaha yangu kwa makaribisho haya makubwa.Sikutegemea kama ningeweza kupata makaribisho makubwa kama haya.Kitu kimoja ninachoweza kukisema toka moyoni mwangu ni Ahsanteni sana kwa kuja katika sherehe hii.Kuna msemo usemao nyumbani ni nyumbani na mkataa kwako mtumwa.Ni kwa kuzingatia misemo hii ndiyo maana nikachagua kurudi na kuishi nyumbani Tanzania badala ya kuishi na kufanya kazi katika nchi za kigeni.Nimerudi nyumbani kusaidiana na watanzania wenzangu katika kuijenga nchi yetu,kuinua uchumi wetu.Nitatumia ujuzi na maarifa yote niliyoyapata katika kuhakikisha tunapiga hatua kimaendeleo. Japokuwa hapa si mahala pake kulisema hili lakini kwa wale ndugu zangu wa kampuni nitakayokuja kuisimamia,naomba niseme kuwa muwe na amani na ninaahidi kushirikiana nanyi kwa moyo mmoja kwa manufaa ya kampuni yetu,jamii na nchi yetu kwa ujumla.Mabibi na mabwana sina cha kuongezea zaidi ya kuwashukuru sana kwa kuja kwenu .Naomba tuendelee na sherehe hizi kwa amani na utulivu.Ahsanteni sana”
Makofi na vigele gele vikasikika katika kila kona ya ukumbi.Watu waimshangilia Innocent kwa maneno machache aliyoyatoa.Sherehe zikaendelea hadi usiku mwingi halafu watu wakatawanyika na kurudi majumbani kwao.
TUKUTANE SEHEMU IJAYO………
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment