SEPTEMBER 1 SEHEMU YA KWANZA

_Gereza la Nyumba ya Giza, Iringa__
Ni majra ambayo baridi huelekea kumalizika kwa mkoa huu, ingawa haikufanya watu wa eneo hilo waache kuvaa makoti. Bado haikupaswa kukaa bila ya nguo ya kukinga baridi kila ikifika jioni, au asubuhi kabla ya jua haljaanza kuonesha makucha yake yanayoweza kuwafanya watu wasitamani hata kuendelea kuweka nguo nzito miilini mwao.
Hakika bado baridi ipo maeneo haya, haswa huko juu mlimani kulipo sehemu ya kuingilia ndani ya gereza la Nyumba ya giza. Hali ya hewa wasikiayo walinzi waliyopo huko juu ya milima kwenye minara yenye kurunzi kubwa za kuangazia usiku. Haikuwa yenye kustahimilika ikiwa mkaaji hatokuwa na koti lolote, hadi ukungu bado upo huko juu.
Gereza hili lililojengwa kwa ajli ya wafungwa watukutu, pamoja na wale wenye kesi nzito ikiwemo mauaji na ugaidi. Majira hayo ya asubuhi helikopta yenye rangi nyeusi na nyekundu, ubavuni ikiwa na nembo ya EASA. Ilionekana ikishuka kwa taratibu eneo la juu kabisa ambalo kuna uwanja maalum wenye herufi 'H', majira hayo maaskari wa jeshi la magereza wakiwa na nguo zao za rangi ya kahawia. Mikononi kila mmoja alishika bunduki aina ya 'shot gun', nyuma ya maafisa hawa wenye silaha za moto mikononi mwao. Walisimama Askari jela wengine wenye virungu tu mikononi mwao, wote macho yao ni juu kutazama chombo kile cha angani chenye kushuka taratibu.
Helikopta ilipotua chini tu, wazee wa kazi wenye silaha waliizunguka kwa pamoja wakiwa wapo umbali mfupi kutoka ilipo. Muda huohuo mlango wa chombo kile ulifunguliwa, watu hao ndiyo walikaa tayari kwa lolote kutokana na ujio huo.
Hali hiyo ilipelekea wale wasiyo na silaha wasogee mbele, walisimama hatua takribani mbili kutoka ulipo mlango. Mlango ulifunguka na walishuka maafisa wengine wenye magwanda meusi, ambao wana bunduki nzito mikononi mwao. Hawa waliambatana na mwanaume mwembamba aliyevaa suti nyekundu, ambaye mikono na miguu yake alifungwa minyororo huku shingoni akiwa na kitu kama bangili ya chuma.
Kuonana kwa maafisa wa sehemu mbili tofauti, kulipelekea itolewe slamu ya kijeshi miongoni mwao. Vyote viliendelea kukiwa na ulinzi mkali ili yule aliyefika mahala hapo, asiweze hata kutoroka wala kushambulwa. Kuwepo eneo hilo lenye ulinzi mkali, haikumaanisha ndiyo kunaweza kusitokee hatari, hata kama wapo ndani ya ukuta mzito uliyopo juu ya mlima. Hatari ingeliweza kutokea kwa juu, kama ukkipita chombo cha maadui.
Kuepusha hilo ndiyo kukawekwa ulinzi wa kila namna, hakika gereza hili waliyoliita shimo la majuto hawakukosea.
Kijana mwenye suti alikabidhiwa upande wa magereza, ambao walimpokea na kuanza kumpekua kila sehemu kwenye mavazi yake. Jambo hilo lilitendeka mbele ya maafisa wa EASA, hadi walipohitimisha.
"Mtu wenu ni huyo hapo, bado ni lulu muhimu mno kwa taifa. Ndiyo anaweza kutaja wenzake walipo, hivyo anahitajika kuwa hai", Afisa wa EASA alisema.
"Usijali kuhusu hilo keshafika mikononi mwetu, hatoweza kutoroka wala kupatwa na hatari yeyote", Askari jela mkubwa kuliko wenzake alijibu.
"Sisi hatuna shaka na kazi yenu, ilimradi tu aendelee kuwa hai huyo kiumbe, anahitajika apewe uangalizi mkubwa ni muuaji hatari mno"
"Duh! Kweli mnanipenda nyinyi yaani pamoja na mauaji makubwa niliyosababisha bado mnanipa ulinzi mkali kama vile ni rais wa nchi. Mnanileta hadi huku nje kupata ugali wa bure", Mtu aliyefikishwa mahala hapo aliongea kwa kejeli baada ya kusikiliza maneno ya pande mbili, kauli hiyo ilipelekea apewe teke moja la kuzunguka na Afisa wa magereza mwenye cheo kikubwa hadi akaenda chini kama gunia.
"Wewe! Haupo magereza madogo ya huko ndani, hii ni nyumba ya giza, wapo wakorofi kuliko wewe humu ndani ila ni wapole. Jifanye unajua kuongea ndiyo utajua kwanini maafisa wa humu hawahitajiki kuwepo gereza jingine nchini zaidi ya humu", Askari jela alisema kibeba.
"Dah! Afisa yaani hadi umenitoa damu mdomoni, kweli unayaweza haya mambo", Mtu yule alisema huku yupo chini. Aliamua kuwatazama watu wale waliyomleta na kuwaambia, "Ukienda mwambie N001 nikimshika atataga yai la mbuni kwa mara ya kwanza". Alipomaliza kauli hiyo alipokea teke la mgongoni kutoka upande wa EASA, alisogezwa hadi upande wa magereza ambapo aliinuliwa juu mzobamzoba.
Maafisa wa sehemu hizi mbili, waliagana na wale waliyofika mahala hapo walipanda helikopta yao wakaondoka. Walibaki wenyeji tu ambao waliondoka na mtu wao hadi eneo ambalo kuna ngazi kama za ghorofa zenye kungia chini. Walizishusha kwa umbali wa ghorofa mbili wakafika eneo ambalo kuna taa tupu tu na viyoyozi kutokana na ukosefu wa madirisha yenye kuweza kuleta walau mwangaza na hewa.
Mhalifu mpya wa gereza hilo, aliingizwa kwenye moja ya chumba. Alivuliwa nguo zote kinguvu na kupekuliwa kila sehemu kwneye mwili wake. Yote ni kuhakikisha hawezi kungiza kitu chochote hatari, zoezi hilo lilipokamilika alivalishwa nguo mpya za wafungwa kisha akaondolewa humo ndani na kwenda kupelekwa eneo ambalo kuna wafungwa wakipasua mawe ya miamba ili kupatikana kwa kokoto.
Huko aliachwa mwenyewe akakabdhiwa nyundo kubwa, alisogezwa hadi jirani na mwamba mkubwa uliyopo chini kabisa ya mlima na kuambiwa aianze kazi mara moja. Pamoja na amri hiyo, jamaa huyu aligoma kabisa na hapo akajiktua akichezea virungu vya kutosha kutoka kwa maafande watukutu.
"Pumbavu wewe Tanzania tunataka reli ya SGR hadi Mwanza ikamilike wewe unatuletea urembo wako. Pasua mawe hayo ujenzi ukendelee", Afande mmoja alimkoromea kisha akageuka nyuma na kusema, "Naenda kuchukua maji ya kunywa nikikukuta umesimama hapahapa utaenda kufungwa bendeji". Aliondoka mahala hapo akiwa na wenzake na kumwacha mfungwa huyo peke yake, naye aliinuka na kushikilia nyundo aanze kufanya kazi. Ila alijikuta akiitupa chini na kuanguka mbele, baada ya kupokea teke zito ambalo lilimfanya ajigonge kwenye jiwe.
"Utaingiaje himaya ya wapasua miamba bila kumsujudia mfalmwe wake wewe", Ilisikika sauti nzito kisha kukaambatana na vicheko vikitokea nyuma, jambo hilo lilifanya mtu huyu apande juu ya jiwe alilojigonga kwa haraka halafu akapiga sarakasi moja maridadi kurudi nyuma. Alifikia mabegani kwa jitu lililompiga, bila ya kuchelewa aliangusha mapigo mfululizo, kwa kasi kubwa mithli ya umeme.
Alipokuja kumwachia alianguka chini mithli ya mzigo, naye alirusha kwa pembeni kisha akabimbirika na kukaa sawa. Alipojiinua kila mfungwa alikaa kimya, akabaki anamtazama yeye tu.
"Nimeanza na mfalme, malkia wake yupo wapi? Waziri mkuu wake? Mawaziri wake nao hamna?", Aliuliza, alipoona kupo kimya alishika nyundo na kuanza kupasua mawe.
**
"Hapana! Hapana! Yaani kaka yangua aingie nyumba ya Giza, na wewe upo wapi Watson. Kwanini ulishindwa kuzuia hili kama uapo jirani na mheshimiwa Rais, tena mtu muhimu kwenye ushauri wa mambo ya kiusalama ulishindwa vipi wewe", Mtu mmoja aliyevaa fulana nyuesi, chini akiwa na suruali ya jeans, alilalamika akimtazama mwanaume mtu mzima anayelekea uzee akiwa amekaa kwenye kochi kuiutulivu.
"Huze relax kwanza ndiyo tuongea kuhusu hili, hebu kaa kochini kwanza", Watson ambaye alikaa kiutulivu aliongea namna hiyo ingawa alilalamikiwa.
"Nitaanza vipi kurelax Watson, unajua wazi alipoingia Gera ni sehemu ambayo ngumu kutoka hata kutoroka, yaani tuhesabie hatoki mule. Hakuna mfungwa kutoka gereza lile aliyewahi kurudi uraiani, wote wana kesi za vifungo vya maisha tena nzito"
"Hiyo ni kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini ukumbuke sisi hatupo hapa kutekeleza sheria hizo. Hatujawa wanausalama sisi, sasa ndiyo tujue tutatumia mbinu gani aweze kuachiwa, kumbuka jambo hilo lilikuwa mkononi mwa EASA nitaanza vipi kuzuia. Yaani pamoja na mheshimiwa Rais kuwa ni amiri jeshi mkuu wa amjeshi ya ulinzi na usalama, hana mamlaka kwenye EASA mpaka niseme nimshawishi achukue uamuzi fulani juu yake. EASA si jeshi ukumbuke, ile ni taasisi ya kiintelijensia ina maafisa wake tu wenye mafunzo ya kijeshi lakini sheria iliyopelekea ikatambulika kazi zake. Haihesabu ni sehemu ya jeshi", Watson alisema.
"Ohooo! Lengo lao waiweke mbali na kauli za viongozi wa kisiasa siyo, maamuz yao yaelemee kwa viongozi wenye taaluma za kiusalama siyo. Hii ni mbaya Watson, nahtaji kaka yangu awe huru na si vinginevyo, kwa gharama yeyote"
"Huze tupo wawili hapa wenye kuijua michezo yenye akili nyingi kupitiliza, afisa usalama wa taifa mstaafu pamoja na jasusi aliyeasi amri. Hizi tukikaa na kuunganisha akili zetu kwa pamoja, Gera si anaachiwa ndani ya muda wowote tu"
"Ok tujadili mimi nna wazo, ila litachukua muda mrefu kuweza kutimia. Akili yangu ilipotulia tu, limenijia", Huze alisema huku akikaa kochi jirani na Watson.
**
Muda huohuo kina Watson wakijadili kuhusu Gera, aeze kuachiwa huru. Upande mwingine ndani ya nchi ya
Tanzania. Faili la kijana aliyeshikiliwa nyumba ya giza liliwekwa mezani, kukiwa na maafisa kadhaa wa EASA pamoja na raia mmoja wa kigeni. Mjadala uliyokuwa ukiendelea mahala hapo, ni juu ya kijana yule aliyeshikiliwa kwa makosa mengi ikiwemo ugaidi.
Kuwekwa kwenye shimo hatari kwa wahalifu, haikumaanisha ndiyo mwisho wa mambo yote. Bali ni mwanzo wa mpango mwingine juu yake, hakuwa tayari amepatiwa adhabu ila ilihitajika aweze kutoa siri juu ya mhusika mkuu wa shughuli hizo ni nani. Kinara wa maovu ni yeye tayari alishatiwa nguvuni, kama vile ambavyo jasusi wa kutegemewa wa EASA alivyoagizwa kufanya. Ila bado hawakuwa wamepata kile walichokihitaji, walipompa kazi kijana wao kulingana na mpango ulivyo. Hawakutaraji kama ungeweza kwenda kinyume ulivyotarajiwa.
Ndiyo maana akaitwa raia huyo wa kigeni, tena akiwa na maafisa ngazi ya juu wa EASA pamoja na jasusi aliyesababisha kukamatwa kwake. Mkutano huo ulifanyika kwenye moja ya hoteli marufu jijini Dar es salaam, haikutakwa kufanywa kwenye ofisi za shirika hilo kiusalama zaidi.
Ingawa wapo hapo ni wanausalama watupu, mmoja akiwa anatoka taasisi nyingine. Haikuwa ni sababu ya kuweza kumwamini na kumfikisha zilipo ofisi zao kwa mikakati zaidi. Katiba yao inasema makao yao ni siri yao, hawakutaka kuivunja maana iliamua kulenga usalama wao zaidi. Viongozi tu wa ndani ya nchi ya Tanzania na hata Afrika ya mashariki hawakuwa wakijua ni wapi yalipo makao yao, ndiyo sembuse huyu mgeni mwenye ngozi nyeupe.
Kikao kilifunguliwa na CE MPZ ambaye alielezea kiundani juu ya mpango ulivyokuwa hadi wakafanikiwa kumnasa gaidi yule, kisha akaeleza mzungu huyo aliyepo mahala hapo ni nani. Ndipo wanausalama miongon mwao walipoweza kugundua, mtu huyo ni Afisa wa ngazi ya juu ya usalama nchini Cuba, pia mmoja wakufubnzi wa makomandoo nchini humo ambaye alimfundisha mbinu mbalimbali Gera aliyewekwa gerezan. Yeye ndiye mwenye kujua kiupana zaidi kuhusu vijana waliyotoka chini yake, alialikwa hapo ingawa tayari alishastaafu kutoa mafunzo.
"Misheni ilikuwa ni kumtia nguvun Gera hakutakiwa kuuawa, lengo ni kumbana aweze kutaja wahusika wa ugaidi uliyofanywa Amboni pamoja na
Shinyanga. Alijulikana mhusika tu, lakini kutokana na yeye kuwa ni mtumiwaji tu. Ingekuwa ni jambo baya zaidi ikiwa hajajulikana mwenye kuratibu haya na kwa lengo gani. Gera ni muuaji na mwenye kujua nini afanyacho, hakuwahi kuacha alama yeyote ile yenye kuweza kusababisha tufike mbali zaidi kujua walipo mabosi wake. Kashikiliwa kwa miezi kadhaa kwenye makazi yetu, maafa yote yakatulia lakini yeye hutumiwa na haikujulikana anayeongoza haya ni nani. Namaanisha adui yetu anatujua, ila sisi hatumjui hili ni hatari mno ndiyo maana nikamwita mwalimu wake Timothy mahala hapa aweze kutupa walau mwangaza juu ya kitendawili hiki", CE alisema kisha akamkaribisha mzungu alisimama na akatoa sabahi kwa kila mmoja.
"Nikiwa kama mwanausalama niliyestaafu, ingawa ninajali usalama ndani ya dunia hii. Sikuwa na budi kuja kujadili suala hili na wenzangu hapa, kwanza nimpongeze kijana wenu N001 hapo kwa kuweza kukamilisha ukamatwaji wa Gera", Mzungu aliongea kisha akaweka kituo na kutupa macho kwa N001 halafu akaendelea, "George Ralond au maarufu kama Gera ambaye nu ndugu wa Hulton Zedicus maarufu kama Huze. Hawa watu ni ndugu waliyochangia mama tu wakiwa na baba tofauti, watoto wa kahaba mmoja aliyekuwa akiishi Niger. Waliingia kwenye jeshi la nchi ya
Niger, ndipo wakaja kusomeshwa mafunzo ya ukomandoo nchini Cuba. Nilichojua kuhusu hawa ndugu wawili, ni wenye kushirikiana kwa kila kitu na hupenda kuwa pamoja hata kwenye mpango wao. Wote wawili ni wazuri kwenye mapigano na hata ulengaji shabaha na wana akili nyingi mno ya kufanya maamuzi kwa upesi. Vijana hawa ukiona mmoja yupo kwenye kazi fulani, tambua na mwenzake pia yumo. Hili nililijua kutokana na maafa mengi waliyowahi kuyasabaisha baada ya kuasi jeshini, hivyo kuweza kujua na kupiga hatua moja mbele kwenye suala hili. Huze apatikane popote alipo, huyu mkimshika na kuwatesa kwa pamoja ndipo mtakapoweza kumpata huyo mhusika mkuu. Udhaifu wao mkubwa, mmoja hawezi kustahimili kuona ndugu yake anateswa mbele ya macho yake. Atasema tu, mkitaka mharibu nguvu yao watu hawa basi jaribuni kuwatafuta wote wawili. Wale ni sawa na jozi ya kiatu, akiwa mmoja hana maana", Timothy aliongea kwa kirefu.
"Nadhani kwa pamoja mmesikia maneno ya Mkufunzi wao, sasa hapa tushajua kiundani nini cha kufanya tukiwa pamoja na huyu mwenye kujua udhaifu wao basi tutaweza kupiga hatua kubwa na kufika mbali", CE alisema.
Kiujumla kikao hicho kililenga kuhakikisha wahusika wakuu wa ugaidi wote ule wanapatikana, ndiyo maana akahusishwa huyo mwenye kuwajua watu wale kiundani zaidi. Kuishi nao kipindi ambacho hawakuwa na mafunzo ya hatari, kungeweza kuwa chachu ya kujua udhaifu wao mkubwa ni upi, hatimaye wamefanikiwa kuutambua na hawakuwa na la ziada zaidi ya kungia kazini.
Huze alihitajika apatikane kwa gharama yeyote ili kuweza kuujua ukweli wa yupi nyuuma ya matukio hayo. Lengo la kuendelea kuchunga usalama wa Afirka ya mashariki kwa kila namna lillenga hilo. Ndiyo maana wakaamua kuweka nguvu zao katika kusaka mhalifu wa pili.
Kutimizwa hilo aliteuliwa mwanusalama mwingine tofauti na N001, jambo hilo lilitokana na ombi la mwanausalama aliyefanikisha malengo ya shirika hilo. Alitaka akambidhiwe mtu mwngine kazi hiyo, maana alihisi baadhi ya wahalifu waliyopo pamoja naye walishajua mwenye kuitimiza kazi hiyo ni yeye. Kuingizwa mwingine kazini, kungeweza kuwafanya wasijue kama kuna kiumbe mwingine mwenye kusaka nyendo zao. Hilo likatimiwa, ingawa hakuwa mwenye cheo kikubwa mahala hapo. Mawazo yake chanya, yaliyoweza kufanikisha mipango mbalimbali pale anaposhirikishwa. Imani thabiti kwenye maneno yake, ikapelekea iwekwe kwake.
**
Benjamini Simoni Mluva, huyu ni kijana msomi aliyefanikwa kuipata shahada yake ya uhandisi wa umeme kwenye chuo kikuu cha Dar es salaam. Mmoja kati ya wanafunzi waliyofaulu kwa alama za juu mno chuoni hapo, kijana aliyehitajika kusoma na baadhi ya wahdhiri ili aje kufundisha chuoni hapo. Ila akakataa kwasababu ya kuhitaji kutafuta ajira aweze kutoka nyumbani kwao akajitegemee. Muda ambao aliotakiwa kubaki chuoni, kwake aliona ni kuendelea kusalia nyumbani mahali asipotaka kubaki asilani.
Kijana huyu alizaliwa na muuguzi mkongwe wa hospitali ya taifa ambaye aliaga dunia miaka mingi iliyopita. Akamwacha akilelewa na baba yake mzazi pekee, hapo ndipo alijikuta akiangukia kwenye maisha ya kulelewa na mama wa kambo. Alisoma kwa tabu mno, kutokana na kutopendwa na mlezi huyo. Kutozaliwa naye alijuta haswa, hadi akilala kwa marafiki zake wanaosoma naye.
Hadi anafikia kuhitimu shahada yake ya kwanza, tayari mama yule ni mwenye watoto ambao wapo shule ya msingi. Nao hawakuwa wakimheshimu kama kaka yao, zaidi ya kumdharau kutokana na sumu waliyolishwa na mama yao.
Kijana huyu nyumbani napo hakudumu alipoanza kutafuta ajira akakosa, alisimangwa hata na baba yake mzazi baada ya kupewa maneno ya uongo na mkewe. Kusikilizwa hakusikilizwa, chakula chenyewe ikawa ni wa kukosa na alikula kipindi ambcho mzazi wake karudi.
Elimu bila ya kumpa mwangaza kijana jinsi ya kujiajiri, ndiyo ilimfanya kabaki hapo nyumbani na kuhangaika ofisi kadhaa akiwa na bahasha yake ya vyeti. Laiti kama ingelimpa mwangza wa kujitegemea, yasingemkuta hayo.
Vilevile imani iliyopo kichwani mwa vijana wengi, juu ya kusoma ndiyo ilimfanya kabaki mahala hapo. Mzazi mwenyewe alimsomesha akiwa na imani hiyo, jambo ambalo lilimfanya aiweke kichwani kwa muda mrefu tangu yupo mdogo. Eti ukisoma utapata kazi na kuwa mwajiriwa, ulipwe pesa uwe na maisha mazuri. Mzazi mwenyewe alisahau kuwa na yeye alitaabika hadi kuja kupata kibarua hiko, kukaa kwake nyumbani akamwona mzigo ilihali alishaambiwa amezaa kijana mwenye kipawa kikubwa mno amuunge mkono na kumwongoza.
Benjamin nyumbani hakusalia hata, alijikuta akifukuzwa na kuanza kuhangaika mtaani pa kulala akawa hana. Marafiki waliyokuwa wakimpa hifadhi kwa siku kadhaa alale, nao walimchoka na kumfukuza kisa wao wamepata kazi na yeye hakupata.
Kipaji chake kilichooongezeka baada ya kusomea uhandisi wa umeme, ndipo alipojikuta akiingia mikononi mwa mtu mzima mmoja mwenye pesa haswa. Huyu alitaka kumpa kazi na hapo akamuahidi kumsomesha kidogo juu ya ujuzi wa dhima hiyo ndipo angeweza kumpatia ajira hiyo.
Benjamin hakuwa na ubishi juu ya hilo, ingawa moyoni alidhani angekuja kusomeshwa nchini hapahapa. Alipokuja kuletewa pasi ya kusafiria, huku akikabidhiwa kibali cha kuishi nchini Cuba kimasomo ndipo alipojua anaenda bara la Amerika kimasomo. Muda huo mzazi wake hakuwa akijua chochote, na wala hakuwa na habari naye baada ya kufanywa amchukie mwanae wa kumzaa. Kijana aliondoka nchini akiwa na furaha tele ya kwenda kupewa kazi akimaliza kusoma, alipohakikishiwa kupata ajira ilimradi tu asome kwa miaka kadhaa. Alibaki kuwa tayari ilimradi tu maisha yaende, alishachoka kudhalilika na kubezwa na wenzake ambao hawakuwa wakifanya vizuri darasani ila wana ajira zenye kuwafanya waishi mjini.
Benjamin alifanikiwa kufika mjini Havana nchini Cuba siku iliyofuata tangu aondoke jijini Dar es salaaam. Alipokewa na kijana mwenye asili ya kilatino na kuahidiwa anapelekwa chuoni huko, akiambiwa taarifa zake zishafika. Mawazo yake yakiwa yapo kwenye chuo kikubwa nchini humo, alijikuta akiingia kwenye kambi la makomandoo nchini humo baada ya wenyeji wake kumfikisha hapo. Tena kibaya zaidi, ni msituni, eneo lenye ulinzi mkali kiasi kwamba kutoroka ni kitendawili.
Alipokutana na wanajeshi wenye sura nzito alijikuta akishangaa mno, matarajio yake na jinsi alivyopakuta kukawa ni kitu kingine kabisa. Loh! Benjamini aliuliza, "Hapa ni wapi mbona mmenileta mahali sipo?"
"Huku ndiyo chuoni unapokuja kusomea, yaani chuo cha ukomandoo. Ulipoambiwa chuoni ukajua unakuja kuongezea shahada ya pili. Pole sana Benjamin, upo hapa kwa kozi maalum ili uende kufanya kazi maalum itakayohusu uhandisi, utasoma bure na kuajiriwa bure mshahara wako utakuwa mnono zaidi", Aliambiwa na mtu aliyemleta mahala hapo.
"Hey! Lakini haikuwa makubaliano yetu haya", Benjamini alisema kwa kujiamini akijiona yupo kwa watu wa kawaida tu, kauli yake hiyo alijikuta akioneshewa bastola na mtu aliyemleta hapo.
"Chagua moja, urudi nimwage ubongo wake, au uongozane na makomadnoo hapo waliyokuja kukupokea", Kauli ilimfanya mwenyewe afuatane na makomandoo wa hapo chuoni.
ITAENDELEA
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment