SEPTEMBER 1 SEHEMU YA TANO..
SEHEMU ILIOPITA...
Yaani kama ulivyosema atakuja, na kweli kaja kusikiliza na kuondoka mahala pale", Muki alijibu. "Vizuri sana vijana EASA haikukosea haswa kuwapandikiza eneo lile muishi kama mateja. Nadhani umuhimu wenyewe ndiyo huu, kazi yenu imeishia hapa, mzigo wenu ushaingia kwenye akaunti zenu, ofisi imejua kama mmetumika kwenye misheni hii kwa ghafla"
"Tunashukuru Bosi"
TUENDELEE NA

**
Watson na Huze walifanikiwa kufika zilipo ofisi za Kibolongo investment ambazo zipo Posta jijini Dar es salaam. Baada ya kufanikiwa kuingia ndani, walimwita na Benjaamin ambaye alikuwa akiendelea na kazi nyingine kama mwajiriwa wa jengo hilo. Kikao kifupi kiliwekwa, baada ya taarifa hiyo kufika eneo hilo.
Tukio zima ambapo kuna baadhi ya maeneo Benjamin hakuhusishwa, aliweza kung'amua kila kitu kama kuna sehemu ya mpango hakuwekwa kwakuwa yupo kwa ajili ya kazi nyingine tu na si kupanga namna ya kumteka mtu. Baada ya kulisikiliza kwa umakini kuanzia siku iliyopita hadi kufikia asubuhi hiyo, ndipo akaona kuna kitu ambacho wenzake walikisahau na ni hatari mno.
"Unasema uliwapigia simu na kukuahidi kuwa wapo njiani?", Aliuliza kama ni mwenye kutoelewa.
"Ndiyo maana yake", Huze alijibu.
"ah! Ah! Ah! Huze umefanya kosa kubwa sana bila ya kujielewa. Walimshika vipi na kuondoka naye, wakati uliposikia kule ni kwamba walipojaribu kumvamia tu ndiyo wakaangamizwa na hao makirikiri. Hapa kuna kachero wa TISS yupo kazini na ndiyo kacheza mchezo huu", Benjamin alisema.
"Besi umeongea jambo la muhimu mno, Huze hakuongea na mtu wetu bali ni mpelelzi huyu. Ni nani sasa?", Watson alinena
"Hilo ni jukumu lako Watson kujua, ila
Besi bado hunaniambia hatari hiyo ni ipi?", Huze aliongea.
"Kuongea naye maane yake maana yake namba yako kaiona, sasa jiulize kama kaforward call zote za kwako. Kama kadivert hiyo namba, basi ndiyo kasikiliza simu zote ulizopiga siku iliyopita hadi kufkia hivi saa. Kama uliongea na watu wetu, basi tambua amejua kila kitu. Kufowadi simu siku hizi silazima uwe na simu ya mtu, utaalamu tu wa mitambo", Besi alifafanua.
"Cheki sasa hivi kama kuna mtu kadivert", Watson alimsihi.
"Namba za kuangalia sizijui mjue, yaani upande huo mimi ni mbovu haswa", Huze alisema.
"Piga *#62# kwa line zote mbili, kama
kuna kudivert sms au voice call kwa namba yako uliyotumia kuwasiliana nao basi jua utaiona hadi namba iliyofanya hivyo", Besi alimweleza Huze ambaye kwa haraka aliingiza hizo namba kwa haraka, sekunda chache tu aliweza kuona ripoti juu ya kuingiliwa mawasiliano yake na namba nyingine.
"Aaargh! Ku****e nipo diverted, huyu kunguru ni nani anayefanya hivi?", Huze alitukana na kisha akauliza juu aliyemfanyia hivyo.
"Huna muda wa kuhangaika kujiuliza hilo wakati bado line hiyo ipo kwenye simu yako. Vunja haraka hiyo line, ubadili namba na kila mtu kwenye mtandao afanye hivyo harka sana", Besi alishauri.
Huze alifungua mfuniko wa nyuma wa simu kwa haraka, alichomoa kadi za simu kisha akaivunja papo hapo. Alishachachawa haswa akikumbuka idadi ya watu aliywasiliana nao tangu apewe taarifa mbaya ambayo Kaila ameisambaza kwa afisa wa jeshi. Loh! kama ni muda huo taarifa zake nyingi zishakamatwa, kiufupi alichelewa. ni mithili ya mtu aanzaye kuzima moto usiunguze suruali ilihali sehemu ya kiunoni ya ngio hiyo ndiyo imesalia pekee.
"Huyu ni nani anayefanya yote haya, inaonekana anajua nini atendalo", Huze alisema.
"That guy ni so brave inabidi ajulikane ni nani na tuwe naye kwa umakini zaidi. Hadi kufikia hivi sasa jua keshajua taarifa zote za watu ambao umewasiliana nao", Besi alisema.
"Iteni vijana kuanzia hivi sasa tuwe na ulinzi mkali, juu ya tu huyu tu", Watson alishauri.
Wakijadili hayo kumbe Kaila alishakamata mawasiliano yoe ya Huze. Kibaya zaidi aliongea na wataalamu wa mtandao wakachapisha namba zote alizowasiliana nazo, zikiwa na majina zilizosajiliwa kufanya kazi hiyo. Aliona hiyo ndiyo sehemu pekee am,bayo angeweza kuianza kwa kuwatafuta hao mmoja baada ya mwingine, maana kila simu aliyosikiliza ilitoa taarifa na kuibuka kwa taarifa juu ya kupotea kwa maafisa wale. Hapo alijua lao moja, ingekuwa ni jambo la maana kutowaacha na kuendelea kuwapekua zaidi. Watu aliyoambiwa ni wenye kuhusika, aliona ndiyo angeanza nao kwa siku hiyo haswa baada ya kufuatilia mawasiliano yao na kujua ni wapi walipotoa taarifa juu yake.
Baada ya kuachana na kina Rambo, hatimaye alifika kwenye duka moja kubwa la vito vya thamani lililopo maeneo ya Mwenge. Hapo aliingiza gari hadi eneo la maegesho la ghorofa lililobeba sehemu hiyo yenye kuuza mapambo mbalimbali ya madini. Alishuka akiwa ni mwenye kujiamini, akaingia upande wa vyooni mwa jengo hilo. Huko alihakikisha yupo pekee yake, ambapo kwa haraka alitazama nje na kupo salama.
Alitokeza nje ya dirisha na kusimama kwenye zege imara ya ghorofa iliyopo uswa wa bomba kubwa la kupitisha uchafu litokalo vyoo vya juu. Norbert alijaribu kulishika pitisho hilo la majitaka, alihakiki malighafi yake iliyotumika kuliunda na alipoona ni lenye asili ya chuma. Hakupoteza muda zaidi, aliliparamia mithili ya nyani, alilipanda hadi alipofika ghorofa ya pili ya jengo ambapo kuna zege lililopo usawa wa chini ya madirisha.
Hapo ndipo alipoishia na aliingia kwenye fito ya zege, alitembea nayo hadi alipofika eneo lenye dirisha la choo ndipo akaingia ndani. Alijikuta yupo ndani ya maliwato ndogo, ikionekana haswa ni kwa ajili ya ofisi moja. Mwonekano wake alibaini fika ni ofisi takamwili kwa ajili ya mtu mahsusi, haikuonekana hata kuwa ni kwa ajili ya umma kamm kule alipoingilia.
Alisimama hapo na kuingiza mkono kiunoni mwake, alitoa bastola yenye rangi ya fedha ambayo aliifunga kiwambo cha kuzuia sauti. Aliiweka tayari kwa lolote kisha akafungua mlango kwa taratibu huku akichungulia mahali alipotaka kuelekea. Norbert alitoka baada ya kizingiti kufunguka nusu tu, alitokea kwenye korido yenye upana kiasi ambapo upande wa kulia kwake kulikuwa na sinki la kunawia mikono ambalo juu yake kuna kioo. Kuwepo na ukuta upande huo ulimfanya aelekeze bastola wa haraka upande mwingine. Huko aliiona korido ikiwa na umbali wa mita moja tu, halafu ikikatika na kuonekana busati jekundu halafu kwa mbele kidogo kukionekana masofa yakiwa yamepangwa kwa ustadi mkubwa.
Nobert alipiga hatua za mnyato huku kasiba ya sailensa yake ikiwa mbele, alifika mwisho wa korido ambapo kwa upande wa kulia kulikuwa meza yenye makabrasha alianza kuiona pembe yake. Hapo alizidisha mwendo kwa haraka, alipofikia akajitokeza kwa hara na kuelekeza bastola huko lakini aliambua patupu na hakuona chochote.
Mwenye ofisi hayupo, akabaki pekee akiwa anashangaa samani za humo, Norbert alipokuta hali hiyo kwa haraka alianza kutembeza jicho iwapo kuna kamera humo ndani ila hakuiona.
"Yuko wapi?", Alijiuliza lakini akiwa amebaki na ulizo hilo, alihisi sauti ya mtu akisogelea mlango, ambao upo upande yalipo makochi. Milio ya kukanyaga ardhi ilimfanya kwa haraka arejee ajibane kwenye pembe moja ya ukuta, ambayo si rahisi kuonekana na mtu atokeaye upande wenye makochi ambao ni sebule ndogo kuelekea ilipo meza ya kazini.
Mlango ulifunguliwa, na kufungwa kwa mara nyingine kisha ukasikia uruzi pamoja na vishindo vya watu. Kaila alikaa tayari kwa lolote lile, muda mchache baadaye aliingia mtu mwenye suti ambaye alimpita na kufikia kiti chake pasipo kutazama nyuma. Alipogeuka aketi ndipo akakutana na mzee wa kazi akiwa na chombo mkononi mwake, alijikuta akishtuka na kutaka hata kupiga kelele ila aliwahiwa na kidole cha shahada kuwekewa mdomoni.
"Habari yako Mr Pwaguzi, nimekuja kukusalimia mara moja tu na rafiki huyu. Keti kitini tafadhali", Norbert aliongea huku akitabasamu, alimwashiria mwenyeji wake aketi naye akatii. Aliendelea kusema, "nyanyua mkonga wa simu hiyo umwambie sekretari wako hutohitaji mgeni kwa hivi sasa" "Nitafanyaje hivyo wakati kuna mtu muhimu hapo nje ananisubiri nitoe ruhusa aingie", Pwaguzi alisema kwa hofu, kuelekezewa silaha ya moto haikuwa jambo la mchezo.
"Nimekwambia fanya hivyo, unataka nikutandike moja ya bega sasa hivi. Hii bastola hawatosikia na kama kungekuwepo mtu aliyepo chooni naye asingeweza kusikia chochote. Epusha hatari kwako, fanya hivyo. Sitorudia tena kukusihi kuhusu hili, ukichelewa sekunde kumi zijazo nitafumua bega lako"
Maneno ya Norbert yalimfanya kwa haraka ainue mkonga wa simu na kubofya namba ya katibu muhtasi wake. Alitoa maagizo kama alivyohitajika kisha akatulia kitini akimtazama mgeni wake wa ghafla, hofu juu yake bado ilikuwepo haswa majira hayo aliyosogea karibu kabisa naye na akaketi kitini mkabala.
"Pwaguzi, kwanini ulitahadharishwa juu yangu na Josi ambaye alipokea taarifa kutoka kwa Huze? Usalama wako ni kuongea tu ndiyo nitajua namna ya kukuokoa na mdomo huu wa bastola", Aliulizwa.
"Mpango niliyopewa usije ukaharibika kwa ajili ya jambo hilo"
"Mpango gani na unahusika kwa namna gani na taarifa niliyoitoa?"
"Mpango wa kuhakikisha mheshimiwa anasaini mkataba mpya nasi juu ya mgodi wa almasi Kongwa. Wanajeshi wale wameshikiliwa kwa lengo la kumlegeza nafsi yake, kwani nchi hii hakuna vinara wa mabomu zaidi yao"
"Ili watege mabomu mapywa siyo mkishikirikiana na Huze bila uwepo wa Gera"
"Kaila unavyoona mimi maisha yangu yameelemea kwenye almasi zile. Fikiria nitaishi vipi ikiwa Mheshimiwa amegoma kuisaini na amezuia tani kumi za almasi huko bandarini kisa kuna hujuma kwetu. Lazima tufanye hivyo mzigo wetu una thamani ya mabilioni ya dola"
"Vipi maisha ya hao mnaowatoa kwa hatia, yanalingana na thamani ya huo mzigo? Uhai wa watu wasiyo na hatia kwa kutega mabomu maeneo ya mkusanyiko wa watu mnafikiri yanaweza kulingana na hicho mlikichuma kwenye ardhi yetu na mnakigombea. Si nyinyi mliyoanguka mahakamani mlipofungua kesi, sasa mmekuja na mbinu hii"
"Kaila hata wewe unaishi kwa ajili ya pesa na unafanya kazi yako ya uandishi kwa ajili ya pesa. Ina njia nyingi za kutafutwa na hii ni mojawapo, kila mtu na ngazi yake kwenye kusaka mafanikio"
"Ohoo! Pole sana kwa tamaa ya muda mfupi ukiisaliti nchi yako ilihali ni mwenye kuheshimika kupitiliza", Norbert alisema huku akiishikilia bastola vizuri,
"No! No! No! Norbert hupaswi kufanya hivi, kumbuka mimi nina watoto watabakia na nani?"
"Mliyokuwa mkiwaua huko kwenye mikusanyiko ya watu, kwani hawana watoto. Iam sorry Pwaguzi, umeingia kwenye mikono ya N001 huwezi kutoka salama"
"Oooh No kumbe ni...." Pwaguzi alitaka kutoa kauli ila hakumalizia, alitobolewa paji lake la uso na risasi. Norbert hakutaka kumbakisha yeyote yule miongoni mwa wasaliti wa nchi, alidhamiria kuwatokomeza wote.
Mahala hapo aliondoka upesi na kurejea kule maliwatoni, alitokea upande wa dirishani na kushuka na bomba lile lile hadi kwenye vyoo vya umma. Huko aliingia kwenye dirisha alilotokea na kisha akajiweka sawa na kutoka kwenye chumba cha choo ambacho aliufunga mlango muda aliyoingia. Alitoka kama vile hakuwa mwenye kufanya tukio la kihalifu humo jengoni, alipitia kizingiti alichoingilia jengoni hapo na hatimaye akafika garini ambapo alitokomea eneo hilo.
**
Majira ya alasiri ofisi ya mwanasheria maarufu jijini, mwenye jengo hilo alisalia mwenyewe tu baada ya katibu muhtasi wake kuwa ameondoka. Alibakia akimalizia kazi ndogondogo ili naye aweze kutoka, hakuwa akijua hiyo siku haikufaa hata ifike. Aliona ni moja mwendo wa wakati kuweza kutimiza majukumu yake ya hapa duniani, alipomaliza kila kitu akijiandaa kutoka nje na mkoba wake.
Mlango wa ofisi yake ulifunguliwa, aliingia mzee wa makamo mwenye suti nyeupe huku akiwa na mkoba mdogo mkononi mwake. Hakutarajia ujio wa mtu huyo mahala hapo, kitendo cha kumwona alijikuta akijenga ndita usoni mwake kwani haikuwa utaratibu kuweza kuwa na ugeni majira hayo.
"Mzee tumefunga ofisi hivi sasa, njoo kesho tafadhali", Mwanasheri alisema huko akijiandaa kutoka humo ndani, kauli yake hiyo ilipelekea mzee huyo atumbukize mkono kwenye mkoba wake kwa upesi. Aliibuka akiwa na baastola na kumwonesha, huku sailensa ikiwa imefungwa barabara.
"Wee ni nani?", Mwanasheria huyo aliuliza kwa uoga.
"Mzimu wa mauti", Mzee yule alijibu kisha akiuachia mkoba wake ukaanguka chini, mkono uliyokuwa umeushikilia ulianza kutoa kofia na kisha ukaondoa ndevu nyingi nyeupe.
"Oooh! Shit Norbert Kaila"
"Unaweza ukaniita N001 pia ukipenda, Mr Felix taaluma yako ya uwakili haikuwa tatizo wala hakuna sheria ya kukuzuia juu ya kutetea wateja wako. Ndiyo maana ukaungana na mafisadi wa almasi kwenye mgodi wa Kongwa, walishindwa kesi yao lakini ulionesha juhudi zako kama wakili. Watanzania wengi walikulaumu kwa kufanya kazi hiyo, ila ukweli utabaki palepale ni sehemu ya kazi yako na hata kulinda siri za mteja wako. Vipi kuhusika na mpango huu wa kulipua mabomu kwenye mkusanyiko wa watu nayo ni jukumu lako, hadi ukapewa taarifa na Pwaguzi juu ya kuleta habari kwangu jeshini. Magari ya mwendokasi mawili yaliyobeba abiria wengi kupitiliza, miaka mitatu iliyopita mliyalipua yote"
"Kaila hapana kijana usiwe namna hiyo, naomba tuliongee hili suala liishe. Seme nikupe kiasi gani cha fedha, najua unahitaji kutafuta uwe na maisha bora kwa ajili ya familia yako hapo baadaye. Tafadhali sana weka silaha kando na uso tuongee"" Felix alisema huku akijaribu kupiga hatua kusogea mbele, aliyatamka akibabaika akiwa na lengo la kumshawishi Kaila maana kifo hakikuwa na mwenyewe.
"Usidhani mimi ni mtu rahisi namna hiyo hadi ufikie kunihadaa kwa pesa, kama ni hiyo ninaipata nyingi kuliko unavyofikiri. Moyo wangu haupo kwenye hela bali upo kwenye uzalendo. Rushwa ni adui wa haki, mtoaji na mpokea rushwa vilevile ni adui wa haki. Lazima atokomezwe kwa gharama zozote, kwaheri Felix", Norbert alipomaliza maneno hayo, alimlamba risasi ya kichwa Mwanasheria huyo, ukawa ni mwisho wake wa kupenda kutafuta mafanikio kwa njia ya mkato.
Alishamaliza watu wawili ndani ya masaa machache tu, aliondoka humo ofisini baada ya kujivalisha ndevu zile pamoja na kuiweka kofia kichwani mwake. Alipishana na mlinzi ambapo alimwaga akiongea kwa sauti ya kizee kabisa hadi lilipo gari alilofika nalo, aliingia upande wa pili wa dereva kama vile ni mwenye kuendeshwa. Huko aliruka hadi kiti chenye usukani na kuliwasha gari, uzee wa namna hiyo kumiliki gari ya kileo tena yenye baadhi ya alama ambazo hutumiwa na vijana. Kungeweza kumtia shaka mlinzi, na kujiuliza juu ya ujio wake mahala hapo. Ndiyo maana akaamua afanye hivyo kwa usalama wake, tendo hilo halikuonekana na mlinzi ambaye hakutilia maanani hata wakati anapifika hapo alilifanya.
Norbert aliwasha motokaa yake, aliirudisha nyuma kisha akaielekeza upande lilipo geti. Aliliondoa mahala hapo na kuelekea getini ambalo alipofika usawa wa mlinzi alilitoa kwa kasi isiyo kubwa kiasi cha kumfanya asiwe makini kutazama kioo cha mbele kumuona akiwa yupo kwenye usukani. Vioo vya pembezoni ambavyo ni vya giza, wala havikumpa shaka aliamini asingeweza kuna chochote. Aliingiza gari barabarani na kuondoka hapo akiwa ameacha maafa humo ndani, pasipo kujulikana alisababisha kingine.
Walinzi walisubiri hadi ilipokaribia kuingia giza bosi wao hakuwa ametoka, jambo hilo lilifanya mmoja kwa haraka sana aingie ndani kwenda kuangalia. Haikuwa kawaida kwa mkuu wao wa kazi kukaa ofosini hadi majira hayo ilihali hutakiwa kuondoka saa kumi na moja tu. Kijana aliyefungua lango aliingia ndani kwa hima, eneo la katibu muhtasi hakukuwa na mtu yeyote hivyo alipitiliza moja kwa moja. Loh! Alimkuta Felix yupo sakafuni, sehemu ya kichwani ikionekana tobo alilopigwa risasi. Hali hii ilimchanganya lakini haikumtoa nje ya akili yake, kijana huyo pamoja na kupewa jukumu la kulinda ofisi hiyo hakuwahi kuona tukio la namna hiyo kwani siku zote huwa kazini na kumaliza bila ya kushuhudia kioja. Alipagawa mno hata jasho lilimtoka kwa ghafla, ingawa alipatwa na nguvu ya kusogea hadi ukutani na kubofya kitufe cha kengele ya hatari.
Muda mchache baadaye walinzi kutoka kampuni ambayo inahusika kulinda jengo la Felix, walifika kwa haraka na kuweka ulinzi mkali kwa nje kama kuna mhalifu yupo ndani asiweze kutoroka. Wachache waliingia ndani na kuona kilichofanya kengele ya hatari yenye kuwaita kwa dharura kubonyezwa, loh! Tajiri mkubwa mwenye kulilipa shirika lao mamilioni ili wampatia ulinzi. Ndiyo huyo hahna uhai tena, wala aliyefanya hivyo hawamtambui.
Mwenzao aliyepo zamu aliishia kuwaambia tu, juu ya aliyeingia hapo ndani kabla ya kuukuta huo mwili. Alieleza ni mzee mwenye mkoba kuukuu, aliyekuja mara moja na kuondoka hapo. Hakuwahi kumwona kabla, hadi aje kusema ni mwenye kumjua kiundani. Kibaya zaidi aliwaeleza hakuwa na miadi na Felix, na muda aliyoingia ndani ulikuwa si wa kazi kwa mujibu wa ratiba ya ofisi hiyo. Alimruhusu kwa kuingia ndani baada ya kujitambulisha kama mjomba wa mwanasheria, amekuja mara moja tu kumwangalia.
Maelezo hayo hadi jeshi la polisi liliyachukua kwa muda huo, kisha wakawasiliana na ndugu wa karibu wa Felix kujua kama kuna mjomba wa namna hiyo, majibu waliyoyapata yaliwafanya waamini aliyeingia ni muuaji hakuwa na undugu naye. Aliingia kutimiza jukumu lake tu na kutokomea eneo hilo, ikahitajika kuwepo mchoro kwa mujibu wa maelezo ya mlinzi wa Felix.
**
"Jamani inakuwa vipi watu wetu wawili wapoteze uai ndani ya siku moja tu. Huyu anayefanya haya ni nani?", Huze alisema akiwa amechachawa haswa, aliweka kikao akiwepo Watson na Besi ambao walipokea taarifa kwa pamoja juu ya tukio zima lilivyo.
"Mnajua hii ni mbaya sana yaani kuelekea siku ya siku tunachezewa mchezo na adui ambaye hatumjui", Watson alisema kisha akawatazama wote halafu akaendelea, "DG Gawaza amesema hakumtuma yeyote yule kwenye kazi hiyo, hakuna mtu wa TISS aliyepo nyuma ya mchezo huo. Sasa huyu ni nani? Mkumbuke Professa Moses hawezi kunidanganya mimi, maana ni mshauri mkubwa sana kwake kwenye masuala ya kiusalama na hata kuongoza taasisi ile". Mwanausalama huyu mstaafu alisimama kisha akanena, "Huze kuliko kuendelea kuendekeza hasira zako basi tambua tutakwama njiani kwenye mpango wetu na Alpha hatotuelewa. kabisa. Adui huyu lazima tumjue ni nani ili tupate mbinu madhubuti ya kumdhibiti, mkumbuke kumtambua adui yako ni nusu ya ushindi"
"Mzee Watson umesema kweli, nashauri kufanyike jambo moja tu ili kumtia kiwewe adui huyo mwenye kufanya haya. Naamini laini ya Huze ndiyo imesababisha yote haya, sasa basi tukubali kwanza anayehusika si TISS. Tumsake huyu kwa kumtia hasira naamini ataingia vitani akiwa anajulikana, hivi mnaonaje kama tukimuua Norbert Kaila", Besi alishauri.
"Sasa Kaila tukimuua bila kumtia nguvuni ndiyo itasaidia nini?", Watson aliuliza.
"Itasaidia haswa, naamini muuaji wa watu wetu yupo kwenye ulinzi wake. Sasa sisi tunafanya tukio moja la kummaliza, halafu tunaacha alama ya kijinga ambayo naamini itaweza kutusaidia kumpata huyo mtu. Hiyo alama itamfanya aje eneo linalohusika nayo, sisi ndiyo tutamjua hapo na kutumia shambulizi la hatari", Besi alitoa rai.
"Wewe dogo unajua ni kichwa zaidi ya vichwa, nafikiri Cuba imezaa zao lile tulilokuwa tunalihitaji siku zote. Watson hukukosea kumpata mtu kama huyu aisee, kanifumbua macho. Huyu muuaji dawa ni hiyo tu hakuna namna nyingine, kumuua tu Kaila. Sasa basi hivi, kesho kuna mkutano wa waandishi wa habari na waziri wa ulinzi Kaila ni mwandishi tena mwenye heshima kubwa, lazima awepo sehemu hiyo. Nataka kesho jua lisizame awe marehemu, Besi hiyo ni kazi yako", Huze alisema.
"Nitakachohitaji tu ni kujua nyendo zake hadi muda ambao atafika pale na si vinginevyo. Jukumu lililobaki naomba mniachie mwenyewe, nafikiri hivi sasa natakiwa niingie maabara nijue nitamwachia zawadi gani kwa ajili yake hiyo kesho. Niwage", Besi alisema huku akiinuka kuondoka sebuleni hapo, alipeana mikono na wenzake na alitoka nje na kutokomea akiwaacha watu hao wameanza kupata ahueni ya jambo linalowasumbua.
ITAENDELEA
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment