SEPTEMBER 1 SEHEMU YA SITA.

ILIPOISHIA SEHEMU YA TANO.
Nitakachohitaji tu ni kujua nyendo zake hadi muda ambao atafika pale na si vinginevyo. Jukumu lililobaki naomba mniachie mwenyewe, nafikiri hivi sasa natakiwa niingie maabara nijue nitamwachia zawadi gani kwa ajili yake hiyo kesho. Niwage", Besi alisema huku akiinuka kuondoka sebuleni hapo, alipeana mikono na wenzake na alitoka nje na kutokomea akiwaacha watu hao wameanza kupata ahueni ya jambo linalowasumbua.
TIRIRKA NAYO .....
**
Majira hayo wakijadili namna ya kumwangamiza Norbert, N001 alikuwepo nyumbani kwa mpenzi wake akiwa amekaa naye sebuleni wakiangalia runinga. Usafiri ule aliyokabidhiwa kazini wala hakuruhusu ufike hapo, aliuficha mahali anapopajua yeye akafika akiwa na gari nyingine. Muda huo wakisubiri kula chakula cha usiku, walikaa wakiangalia taarifa ya habari ambayo ilieleza juu ya kuaawa kwa tajiri wa vito vya madini na wakili wake kwa pamoja.
Habari ilivyotangazwa kwa mtu wa kawaida, angeweza kudhani ni imepangwa kuwakomoa kwani ni watanzania wanaoishi nchini na pia wamefanya mambo ambayo ni kinyume na nchi hii. Mtu mwenye fikra za kawaida, angekuwa mwepesi kusema serikali ndiyo imehusika na mpango huo ili kulipa kisasi kwa hasara iliyosababishwa na wizi wao hao. Namna hii ndiyo watu wenye kufuata itikadi tofauti ya kisiasa na ya chama tawala, huanza kuituhumu serikali pasipo kuwepo ushahidi wa kina juu ya jambo hilo. Hakika wengi wenye ushabiki huongea mambo wasiyoyajua, pasipo kutambua mengine kuna mchezo mchafu umefanyika uliyo tofauti na tuhuma inayowakabili watu wale.
"Nor najua hii ni kazi yako tu hakuna jingine", Norene alisema akiwa yupo kifuani mwa Norbert.
"Alama zangu ambazo wengi hawazijui nikifanya tukio, mwenye kuzitambua ni wewe na CE tu. Siwezi kukataa juu ya hilo, nyakati ambazo matukio yalitokea, ni alama yangu tosha ili kuwafanya watu wetu wasije kujiingiza na kuniharibia kazi", Norbert alisema.
"Ila si unajua kama hii itaichafu serikali kisiasa"
"Ni ndani ya muda mfupi ila katika muda mrefu ujao ndiyo itaongezeka imani ya wananchi kwa rais wetu. Tuvute subira tu, Pwaguzi na Felix hawakustahiki kupumua kabisa mbali na usaliti wao kuna jingine zito limenifanya niwapoteze"
"Ok nakuamini najua unafanya kile ambacho ni sahihi, pia kawaida yako kutoeleza sababu ya kufanya kitu kabla ya kukamilika kazi yako. Sitoweza kukuliza kuhusu hilo, ila nina sababu nyingine
itakayonifanya nikuulize swali tofauti"
"Uko huru malkia wa moyo wangu, waweza kuniswalika swali ulitakalo"
"Nor hivi hii pete ya uchumba hapa kidoleni huoni kama inahitajika nyingine, baba na mama wamekuwa ni watu wa kunisema kila kukicha. Mjomba tu ndiyo anajua kunitetea, kibaya zaidi huyu Jerry sasa hivi yupo primary ila wazazi wake bado hatupo kwenye ndoa" "Si kama sipendi kuwepo kwenye ndoa, ila nafikiri sana na hii kazi wakiijua familia yangu ni ipi. Huoni itakuwa ni njia pekee ya kuniweka nguvuni kupitia nyinyi, nafikiri unatambua wazi udhaifu wangu mkubwa ni familia yangu. Ndiyo maana nasita sana kuoa hadi hivi sasa una ujauzito wa pili. Si kama sipendi, tatizo nacheza kamari na kifo
"Kwakuwa ni mmoja wa watu wa ofisini, natambua sehemu ya kazi zako. Sina shaka juu ya wewe, ilimradi uzima uwepo nafikiri hata iwe siku gani ila ndoa kwetu ipo", Norene alisema huku akiinua kichwa chake, alipeleka macho yake usoni mwa Norbert ambapo walitazamana kwa sekunde kadhaa kisha wakagusanisha midomo yao.
"Nashukuru kwa kuwa mwelewa, tukale sasa nahitaji kupumzika kesho ni mchakamchaka tena nitakuwepo kwenye mkutano wa mheshimiwa na kamera zangu kufanya kazi. Blog yangu pia inahitaji ishibe habari, si unajua ninaaminika mno kuwa ni mtoaji wa habari zenye uhakika. Inabidi nipige picha nizitume kwa sekretari halafu niingie kibaruani tena. Kazi ya kuiaendesha blog ipo kwake hivi sasa"
"Na kweli maana usipozugia hiyo ukawa na fedha nyingi unafikiri watakuelewa vipi, si ndiyo mwanzo wa kukutilia shaka"
**
_Asubuhi__
Ukumbi wa Kamrijee ambao ulipangwa kufanyika mkutano wa waandishi wa habari, ulishaandaliwa mapema na meza kuu pamoja na viti vitakavyotumika kwa ajili ya kutaniko hilo vilishawekwa. Upande wa nje sehemu ya chini ya miti kulionekana waandishi wa habari mbalimbali wakiwa wamekaa wakijadiliana mambo mbalimbali. Huku baadhi ya magari ya televisheni mbalimbali yakiwa yamejipanga hapo, ulisubiriwa muda mwafaka tu kwa ajili ya kurusha matangazo pamoja na kuuliza maswali mbalimbali kwa mheshimiwa huyo kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali.
Norbert majira hayo alisimama kwenye gari lake la kazi, siku hii alivaa suruali ya rangi nyeupe, shati jeupe ambalo lina kizibao cha rangi ya kaki huku chini akiwa na kiatu cha rangu nyeupe. Mkononi alishika kamera yake yenye lensi ndefu, huku begani akiwa amening'iniza mkoba mdogo wa kuhifadhia chombo hicho cha kupiga picha. Pembeni yake kulikuwa na stendi maalum ya kamera ikiwa imekunjwa na kuwekwa chini.
Naye alijionesha alikuwa yu tayari kwa kufuatilia mahojiano hayo, pamoja na kuuliza swali kama mwandishi. Kitambulisho kilichopo shingoni mwake kilimwonesha ni mwanahabari, hivyo kustahiki kutoa maswali ni jukumu lake. Pamoja na hayo alifika hapo akijua lazima atafuatiliwa nyendo zake, maana alishatibua hali ya hewa na kuwamaliza watu sita kwa siku mbili tofauti ambao wapo kwenye mtandao wa wanyonyaji wa rasilimali za nchi.
Alijiweka tayari kwa lolote na hata ndani ya shati lake alivaa koti la kuzuia risasi, alihofia angeweza kudunguliwa muda wowote akitoka nje ya eneo hilo. Pamoja na kuwa na mafunzo makubwa ya kupambana, hakuwa na uwezo mwingine wa kujihami dhidi ya risasi zaidi ya huo tu. Kifaa kile kitakacho kwenye chombo cha moto hakikuwa na mjuaji, hadi aseme atembee kifua mbele. Tahadhari kabla ya hatari, ingawa akiwazacho si kile ambacho maadui zake wamekifikiria juu yake.
Muda wa kungia ukumbini na kuweka vifaa vyake vya kazi, aliwahi sehemu nzuri na kisha akaiweka stendi ya kamera yake pamoja na kifaa kwa juu. Majira hayo Kaila alivaa kofia aina ya 'kapelo', ambayo kwa ndani ilikuwa na malighafi yenye kuweza kuweza kuzuia risasi. Machoni mwake aliweka miwani yenye uwezo usiyo wa kawaida, yote ni kwa ajili ya usalama wake tu maana kazi iliyopo mbele ni kubwa mno.
Muda mchache baadaye alizongana na waandishi wa habari wengi, majira hayo ndiyo waziri wa ulinzi aliingia ukumbini kwa mujibu wa ratiba. Mkutano ulianza kama kawaida, Kaila aliwasha vitendea kazi vyake na kuchukua matukio yote yaliyojiri mahala hapo. Huku ni miongoni mwa watu waliyouliza maswali yenye mashiko kwa mheshimiwa yule, hadi mwisho wa kikao alishanakili vitu muhimu kwa ajili ya kazi hiyo kwenye kifaa chake cha kuandikia.
Baada ya kutawanyika wenzake, alibakia pekee akifunga vifa vyake na kisha alivinyanyua baada ya kumaliza akawa anatoka kwenda nje. Alipokuwa akitembea kuukaribia mlango, alijiwa na mtu mwenye mwili mkubwa ambaye alizuia na kumfanya aweke umakini kwake.
"Mheshimiwa anahitaji kukuona kabla hujaondoka, yupo kwenye gari lake", Aliambiwa na hakuwa na ajizi zaidi ya kuongozana naye, muda mchache alifikishwa kwa Mheshimiwa ambaye alisalimiana naye kwa bashasha na kisha akasimama naye pembezoni mwa magari ya serikali huku ulinzi ukiongezwa maradufu.
"Kaila brave boy, nimependa sana kwa kunipa changamoto kwenye mkutano ule, umeniuliza maswali yenye mashiko. Nimependa sana kwa kujua kutumia kazi yako vizuri ili upate mambo kwa uhakika", Mheshimiwa alisema.
"Nashukuru sana Mheshimwa", Kaila alpokea pongezi zake.
"Kijana wangu pamoja na hayo, natambua sana wewe ni mtu muhimu kwa jinsi ulivyotangaza ujenzi wa reli ile ambayo imefanya JWTZ iwe na heshima hivi sasa kimataifa. Ndiyo maana wakakupatia nishani kwa kazi nzuri uliyoifanya, haikuwahi kutokea mwandishi akapatiwa ila wewe ni wa kwanza. Sasa basi kijana wangu napenda utambue septemba mosi ni siku ya majeshi nchini, pia hiyo ndiyo siku maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya uzinduzi wa reli hizo. Utafanywa na Mheshimiwa Rais na atasafiri kwa treni hiyo hadi mkoani Mwanza, nikiwemo mimi, waziri wa uchukuzi na wengineo, baadhi ya waandishi wa habari ambao watachukuliwa baadhi tu kwa jili ya kushuhudia uzinduzi huo", Mheshimiwa aliweka kituo kisha akaendelea, "baadhi yao wewe umekuwa ni mmojawapo na hili limependekezwa na mheshimiwa mwenyewe, naomba usimwangushe na amenituma nikupatie kitambulisho hiki kilichotengenzwa kwa ajili ya siku hiyo"
Kauli hiyo ilimfanya Kaila ajifikirie kwa sekunde kadhaa, hakutarajia kama angeweza kupewa mwaliko muda huo. Ambao utamlazimu akae nje ya kibarua alichokabidhiwa afanye kazi nyingine, kwake hilo suala lingekuwa ni gumu mno. Baada ya sekunde kadhaa aliinua kichwa na kusema, "Mheshimiwa kwanza kabisa napenda nikuombe radhi na pia nitamwomba radhi Mheshimiwa Rais pia. Siku hiyo uliyoisema nitakuwa nipo kwenye kazi nyingine, ila sitoweza kuwaangusha nafikiri nitawapa mtu ambaye ni mbadala wangu atakayeweza kuungana nanyi kwenye siku hiyo. Huyu ataniwakilisha mimi, nadhani unamfahamu msaidizi wangu wa kazi"
"kama ni Rukia basi huyo hatuna shaka naye, maana ulishughulika naye katika kutangaza mradi ule. Sawa akiwepo kwa mbadala wako si mbaya, ilimradi utimize majukumu yako ya kimaendeleo na hata ukifanyacho kiwe ni sehemu ya kulikuza taifa. Bado tupo pamoja nawe"
"Nashukuru sana Mheshimiwa kwa kunielewa, binti yule ni mwenye kujua kuichezea kamera ipasavyo na mwenye upeo mkubwa wa kutoa changamoto akiwepo kazini. Mtakuwa naye"
Norbert hakukaa sana mahala hapo, hakuwa na mazoea ya kupiga soga na waheshimiwa labda kwa jambo muhimu. Alimuaga na kuelekea hadi lilipo gari lake, alipofika alifungua mlango wa dereva kisha akaingia kidogo halafu akafungua mlango wa nyuma wa gari wa kuwekea mizigo. Alichukua stendi ya kamera baadhi ya vitu akaenda kuviweka huko, aliporejea alikaa kwenye kiti cha dervea halafu akatoa kipakatishi chake.
Kaila aliamua kuingia mtandaoni na kutuma sehemu ya habari ile, pamoja na vitu muhimu kwa katibu muhtasi wake akimpa kazi ya kuvituma kenye blogu. Alipomaliza shughuli hiyo aliiweka tarakilishi yake ya mapakato kwenye kiti cha pembeni, Kaila aliwasha gari na akataka kufunga mkanda ila moyo ulisita na akaamua kuacha hivyo na kuondoka mahala hapo.
Aliingiza gari barabarani, aliiondoa kwa kasi kubwa hadi alipofika posta ambapo alichukua uelekeo wa mahakama ya hakimu mkazi kisutu. Alifuata njia hiyo kisha kachukua uelekeo wa ilipo wa kulia akaichana na barabara inayoenda kituo cha akiba. Aliendesha gari muda ahuo akielekea upande lilipo daraja la salenda huku akiongeza mwendo kwa kasi kubwa. kutokana na uchache wa magari.
Akiwa yu njiani hata bado kufika kituo cha polisi daraja la salenda, mlio wa simu ulisikika ambao ulitokea chini ya kiti alichokaa. Sauti hiyo ya muito ambayo ilitoka mahali asipopajua ilimfanya ajipapase mfukoni mwake na akajijua anayo simutamba yake. Alibaki kujiuliza hiyo iliyopo humo ndani ilifika vipi, ila hakuelewa. Mwishowe aliingiza mkono kwa upesi akikipasa, huku macho bado yapo mbele asije kugonga.
Hatimaye aliikamata simu hiyo, alipoitoa aliiona ni ngeni machoni mwake na wala hakuwahi kuiona. Norbert pamoja na hayo alijipa imani na kuipokea kisha akaiweka sikioni. Aliona ni bora afanye hivyo maana ililengwa kwake ndiyo maana ikawekwa humo ndani na mtu ambaye wala hakujua ameingia vipi.
"haloo........................................oooh! Jesus", alijkuta akishtuka na muda huo kengele maalum ilianza kusikika huku sehemu ya kioo cha redio cha gari lake kukaanza kuonesha dakika zikipungua, loh! Kaila moyo ulimlipuka haswa akikumbuka maneno aliyoambiwa muda mfupi uliyopita.
ILIVYOKUWA
Baada ya kupewa kazi ya kumwangamiza Norbert, Besi mtaalamu wa uhandisi wa umeme aliyepelekwa nchini Cuba kufundishwa namna ya kuunda mabmu ya aina mbalimbali na maafisa wa kirusi waliyomo nchini mule. Aliamua kuichukua dhima hiyo mapema kwa kubuni silaha yake, ambayo huweza kuendana na mfumo wa umeme wa gari husika. Gari ya Norbert na muundo wake aliipata, baada ya hapo aliunda bomu mahsusi kwa ajili yake.
Kulipopambazuka tu akawa ni mtu wa kwanza kufika viwanja vya Karimjee, akiwa na mavazi ya kawaida pamoja na kofia iliyoficha sura yake kwa kiasi kikubwa. Alijibana kwenye miti hadi pale Kaila alipofika mahala hapo, alimchunguza hadi nyendo zake na kuingia ndani ya ukumbi pale mkutano tu ulipoanza.
Kukiwa hakuna mtu ndani aliingiza mkono kwenye mkoba wake aliyokuja nao, alitoa gari ndogo ambayo huumika kwa asilimia kubwa kuchezewa na watoto. Besi aliiweka chini kisha akashika kiongozeo chake na kuanza kuiongoza hadi ilipofika kwenye uvungu wa gari la Norbert. Alipohakikisha ipo mahali alipopataka, alibonyeza kitufe kimoja kwenye kiongozeo kile. Mlio wa simu ulisikika papo hapo, hali ambayo ilimfanya aingize mkono mfukoni mwake na akatoka na simu ikiwa inaonesha kioo chenye mwanga wa bluu mpauko.
Besi aliamua kuondoka kuelekea kule ambapo gari la Norbert, akiwa ni mwenye mwendo wa hadhari alipolifikia mkononi bado ana kiongozeo cha kifani cha gari kilichopo uvunguni. Alibofya rimoti ile, na maajabu kioo cha motokaa ya N001 kilishuka, upesi aliitia ile simu chini ya kochi na kisha akakipandisha kama kilivyokuwa. Baada ya kukamilisha kazi hiyo aliondoka upesi eneo la
Karimjee, alifika nje ambapo gari dogo iliwasili papo hapo. Iliposimama tu alifungua mlango na kuingia halafu akaufunga, motokaa hiyo iliondoka kwa kasi hapo.
"Kila kitu kimeenda sawa?" Aliulizwa na mtu aliyekaa kiti cha mbele cha gari hiyo.
"Kila kitu kipo sawa kabisa, hata nikitaka
kuliongoza gari lake kuelekea ninapopataka mimi inawezekana kabisa. Tusubiri mtu wetu aliyepo pale atwambie muda ambao ataondoka, ili tumpigie simu", Besi alisema.
"Ha! Ha! Ha! Akiipokea tu ndiyo kaactivate bomu lile. Mwiisho wake utakuwa ni huo au siyo"
"Kabisaa"
Besi na mwenzake wala hawakwenda mbali, walikaa mahali kusubiri kikao kiweze kuisha ili wamfanye Norbert aliwashe bomu mwenyewe bila ya kujijua. Chombo kile mfano wa gari ambacho kipo uvunguni, kilinasishwa kwenye eneo la chini ya gari. Ndiyo kikaenda kukamata mfumo wote wa gari hilo ambao unatumia umeme, na hata kuliongoza. Laiti kama akiamua kuliwasha akiwa na kiongozeo kile anaweza, akiamua kuendesha vilevile uwezo upo. Ambacho kilishindikana kufanyika, ni kufunga na kufungua mlango tu, vingine vyote ni uwezekano upo. Milango iliweza kuweka vibanio ila mtu akijaribu kukitoa anaweza, mfumo huo wote ulienda kuunganishwa na bomu la kielektroniki lililopo kwenye gari lile. Moja ya silaha hatari ambayo kuteguliwa wala haitowezekana, na ngumu kufanya hivyo.
Walisubiri hadi pale walipoewa taarifa ya kuondoka kwa Norbert muda ambao kikao kiliisha. Wao ndiyo wakarejea tena kule kwa mwendo mdogo baada ya kupewa taarifa anaongea na waziri, walipofika lango la kutokea ndipo walipomwona akiingia barabarani na gari yake. Walimfuata hadi alipokuwa akielekea upande wa daraja la Salenda ndipo wakampigia simu. Afanalek! Laiti Norbert angejua hatari ya simu ile, wala asingejaribu kuipokea. Kuipokea kwake ndiyo akawa ameliwasha bomu, Besi ndiyo akamweleza kila kitu kuhusu silaha hiyo ya mlipuko. Kumbe alitakiwa kutosimama, akijaribu tu linalipuka, akishusha kioo linalipuka. Alitakiwa abakie kwenye mwendo vilevile, jambo ambalo haliwezekani.
"Ha! Ha! Ha! Ha! Kwisha habari yake huyu", Besi alisema baada ya kumpa taarifa Norbert halafu wakampita kwa kasi kubwa wakijua hawezi kupona yule.
BAADA YA KUJIJUA YUPO NA BOMU
Jambo ambalo Besi hakulijua, Norbert ni mtu mwenye akili nyingi na ubongo wake hufanya kazi kwa haraka kunapotokea tatizo. Ndiyo huwa na maamuzi ya haraka, ila huwa na faida kwa upande wake. Kumwacha namna ile wakitarajia ni kifo kinamkuta, walikosea haswa baada ya kumpa maelezo yale ndipo akajua kuna udhaifu kwenye bomu lake la kutega. Uoga ulimtawala Kaila kwa sekunde kadhaa ila akili ilipomkaa sawa, alichukua mkoba wake na kuweka kipakatishi huku akitazam mbele kwa umakini. Alipomaliza aliitwa kamera na kuingiza ndani, baada ya hapo aliufungua mlango akauacha na uwazi kidogo isijibane tu.
Udhaifu wa kuweza kufunga vioo na kusahau upande wa milango, ndiyo ulimpa nafasi ya kuweza kutoka.
Norbert alilikumbatia begi lake, kwa mkono mmoja huku mwingine ukiwa kwenye usukani. Alipokaribia daraja la salenda kwa haraka, alichukua hadi ile simu na kisha akafungua mlango na kujitupa nje akielekea upande ambao kuna matofali ya katikati ya barabara kwenye majani yenye kutenganisha njia mbili za Ali Hassan Mwinyi. Alijikuta akianguka na hata upande wa pili wa barabara, aliendelea kubimbirika ana kajikuta akienda kujigonga kwenye njia ya upande wa pili njia irudiyo mjini. Begi tu ndiyo lilimsaidia asiumie kifuani baada ya kugonga pale, ila kote alipopigiza mgongo maumivu aliyapata sehemu za kando.
Hatimaye alitoka nje ya lami pasipo kuguswa na gari, aliendelea kubimbirika kuelekea kwenye kilima kinachoenda upande ambao kuna ufukwe wa bahari. Hadi akafika eneo ambalo mto Msimbazi unaingia baharini. Hapo ndipo aliposita eneo ambalo lina takataka nyingi, aliijinua wima na muda huohuo alisikia sauti ya mlipuko mzito ambayo haikumfanya asimame hapo. Alilivaa begi lakekwa haraka kisha akakimbia kuelekea upande wa kaskazini mwa eneo hilo. maji ya mto ambayo hayakuwa mengi aliyavuka pasipo kujali harufu iliyopo eneo hilo. Aliendelea na mwendo ule hadi alipofika eneo lenye mikoko, ndipo alipojikeza na kurejea barabarani ambapo alikimbia zaidi hakutaka kusimama.
Mbele akiwa anakaribia kuifikia njia iendayo ufukwe wa Coco, alikutana na bajaji ambayo alisimamisha upesi akaingia. Aliagizwa apelekwe mahali anapopahitaji, huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio. Akiwa njiani aliifungua simu aliyoikuta kwa maadui zake, akachomoa kadi yake pamoja na chipu ndogo aliyoikuta humo ndani halafu akaitupa ile.
**
Kicheko kilikuwa upande wa kina Besi baada ya kusikia mlipuko, aligonganisha kiganja chake na mtu aliyekuja kumchukua huku akijitapa kwa kuweza kuitimiza kazi hiyo. Waliamini Norbert ndiyo habari yake imeisha, akili ipo kumuwaza huyo ambaye anamlinda. Loh! Hawakujua kama Kaila ni mzima, huyo wanayemhofia kafanya uharibifu kwao ndiyo yuleyule. Ama kweli usilolijua, ni usiku wa giza.
"Ebwanaeh! Yule mwandishi wa habari na umbea wake, ni kwisha kazi kabisa", Mtu aliyepo kwenye usukani alisema.
"Mtoto akilia wembe we mpe tu, sasa kapewa kweli na umemkata. Yaani hata nafasi ya kujuta kwa kujiingiza kwenye mambo yaliyomzidi uweozo hatokuwa nao. Ndiyo kwisha habari yake, mpumbavu sana yule jamaa. Sasa tunamtoa sadaka halafu tuone huyo mwenye kumlinda hadi kamwacha akalipukiwa na gari atafanya nini", Besi alijitapa baada ya kukamilisha kazi yake haramu.
ITAENDELEA
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment