Tuesday, 18 March

Ads Right Header

Buy template blogger

SUKARI YAZIDI KUADIMIKA NCHINI, WANANCHI WAISAKA KILA KONA

SUKARI YAZIDI KUADIMIKA NCHINI, WANANCHI WAISAKA KILA KONA

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KILIO cha kuadimika kwa sukari nchini kimeendelea kushika kasi kutokana na uhaba mkubwa uliopo na wananchi wanapobahatisha kuipata bei yake ni kubwa kwani kilo moja ya sukari inauzwa hadi Sh.4,000 badala ya Sh.2,600.

Kutokana na kuadimika huko wananchi wa maeno mbalimbali nchini wameendelea kupaza sauti zao kwa Serikali kuona hatua inayoweza kuchukua kuhakikisha sukari inapatikana na kwa bei ambayo itakuwa rahisi kuimudu.

Katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na majiji mengine nchini sukari imegeuka kuwa bidhaa adimu na wakati mwingine hata wafanyabiashara waliokuwa nayo wanaiuza kwa kificho utadhani wanauza bangi.

Michuzi Blog na Michuzi TV kwa nyakati tofauti limefanya uchunguzi na kubaini sukari imeendelea kuadimika madukani kwani kati ya maduka matano unaweza kuibahatisha kwenye duka moja tu na bei yake ni kati ya Sh.3700 hadi Sh.4000.

Baadhi ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wamesema kwa sasa sukari imekuwa changamoto kubwa kuipata kwake,hivyo wameiomba Serikali kuchukua hatua.

Mwanahawa Mkwinde ambaye ni mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam anasema sukari hasa kwa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan mahitaji yake huwa ni makubwa lakini kwa bahati mbaya haipatikani madukani na hata inapopatikana bei yake huwa juu sana.

Kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Dodoma na hasa wa Wilaya ya Chamwino ambao wamezungumza kwa njia simu nao wamelalamikia bei ya sukari kuwa juu ambapo nako wanainunua kwa Sh. 4,000 kwa kilo moja.

Mkazi wa Chamwino  Nasibu Ramadhan maarufu kwa jina la Kamanda amesema bei kubwa ya sukari imesababisha wananchi walio wengi kushindwa kuimudu kuinunua,hivyo kusababisha malalamiko.

"Ndugu Mwandishi huku kwetu Chamwino hali ni mbaya sana ya Sukari kwani bei ziko juu , tunaomba mtusaidie kufikisha taarifa hizi serikalini angalau viongozi waje kutusaidia na zaidi Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa,"amesema Ramadhan.

Mmoja ya  mfanyabishara mdogo Ester Mwaruko kutoka Chamwino amesema  kutokana na bei ya sukari kuwa juu wao kama wafanyabiashara wadogo wanalazimika kuuza kikombe kidogo cha chai shilingi 400  badala ya 200 kama ilivyokuwa awali kutokana na sukari kuwa juu ambapo hata hivyo wanapata wakati mgumu Sana.

"Hapa kwangu kikombe kidogo cha chai nauza sukari kwa Sh. 400 lakini awali nilikuwa nauza Sh.200 lakini kwasababu bei ya sukari ipo juu , hivyo naamua kupandisha kidogo lakini wananchi wanalalamika sana.Tunaomba Serikali itusaidie kufuatilia upandaji huu wa sukari,"amesema Mwaruka.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya hiyo ya Chamwino Vumilia Nyamoga amesema anazo taarifa za kupanda kwa bei ya sukari na kwamba wanafanyia kazi."Tumefanya uchunguzi sukari inauzwa shilingi 3, 500 na tunaendelea kufuatilia kuhusu sukari kuendelea kuwa bei ya juu."

Wakati huo huo Mkazi wa Ngaramtoni jijinj Arusha Jonathan Titto amesema nao wanachangamoto kubwa sana ya kuipata sukari na kwamba hata madukani imeadimika." Huku kwetu Arusha nako sukari imekuwa ni kilio cha mmoja wetu, tunaomba Serikali itusaidie na kama kuna watu wameficha sukari basi wenye mamlaka wachukue hatua kwani tunaopata shida ni wananchi."

Wakati malalamiko ya kuadimika kwa sukari yakiwa katika kila kona ya nchi, tayari Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa alishatoa maelekezo kwa wafanyabiashara ya sukari ikiwemo ya kutopandisha bei lakini bado imeendelea kuwa juu.

Leave Comments

Post a Comment

Ads Post 4