SERIKALI IMEKABIDHIWA VIFAA VYA MAABARA VYA UCHUNGUZI NA UTAMBUZI WA MAGONJWA YA MIFUGO
SERIKALI IMEKABIDHIWA VIFAA VYA MAABARA VYA UCHUNGUZI NA UTAMBUZI WA MAGONJWA YA MIFUGO





SERIKALI imekabidhiwa vifaa vya maabara vya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo ambavyo vitasaidia kufanikisha juhudi za kupambana na magonjwa yakiwemo yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Vifaa hivyo vimetolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) chini ya programu ya Ajenda ya Usalama wa Afya Ulimwenguni (GHSA-ZDAH).
Lengo ni kukuza uwezo wa dunia wa kujilinda dhidi ya hatari za magonjwa ya maambukizi.
Akipokea vifaa hivyo jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema vifaa hivyo vitawezesha Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Amesema matokeo ya utafiti wa kitaifa uliofanyika mwaka 2012/13 yalionesha kuwa nyingi ya kaya zinategemea mifugo kwa ajili ya kujikimu kimaisha hivyo mazao ya wanyama ni vyanzo vya moja kwa moja vya vyakula kama vile nyama, maziwa, na mayai.
“Pia wanyama kazi ni nyenzo muhimu katika uzalishaji, vile vile mifugo ni chanzo muhimu cha mboji inayotumika katika kilimo na uzalishaji wa gesi asilia kwa ajili ya kuzalisha umeme au kupikia na hivyo kuzuia au kupunguza kabisa tatizo la uharibifu wa mazingira,” alisema na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitaboresha zaidi sekta hiyo.
Hata hivyo alisema kutokana na unyeti wa sekta hiyo kwa uchumi wa nchi, Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha ufugaji wa mifugo unaboreshwa ili kuweza kutoa mazao na bidhaa bora zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na hivyo kuinua hali za uchumi za wafugaji na wananchi kwa ujumla.
Ulega alisema moja ya hatua muhimu zinazochukuliwa kufikia adhma hiyo ni ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ambayo huchangia katika kuharibu ubora wa mazao na bidhaa zitokanazo na mifugo.
Alisema pia mwongozo ya chanjo na uchanjaji wa mwaka 2020 umeshatolewa ambao unalenga kuhakikisha kwamba kila mfugo unachanjwa magonjwa ya kimkakati 13 ambayo yameainishwa na Wizara.
Kuhusu vifaa hivyo alisema vitasaidia kuwezesha uzalishaji wa nyma ulio mzuri ambao utasaidia kusafirishwa kwenda nje ya nchi pamoja na kuzalisha chanjo bora za mifugo.
“Vifaa hivi vitaimarisha maabara ya Taifa ya Veterinari na kuwa ya mafno ikitoa huduma kitaifa na hata kimataifa kwa ujumla,” alisema Ulega na kuongeza kuwa hatua hiyo itadhibiti uwepo wa dawa feki kwa wafugaji.
Aliwataka watumishi wa Maabara hiyo kufanya kazi kwa uadilifu wakitumia vyema vifaa hivyo ili viweze kuleta tija kwa sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka FAO ambaye ni Mkuu wa Mradi wa Ajenda ya Dunia ya Usalama wa Afya (GHSA),Folorunso Fasina alisema vifaa hivyo vya maabara pamoja na dawa mbalimbali vimegharimu jumla y ash milioni 500 ambavyo vitatumika kwa uchunguzi wa vimelea vya magonjwa kutoka kwa wanyama w amajumbani, mifugo, wanyamapori na magonjwa ya kipaumbele yanayoambukizwa.
Alisema vifaa vitachangia katika kutoa mafunzo kw anguvu kazi kwa ajili ya kusimamia mifumo ya afya Tanzania na kukuza uwezo wa maabara mpya ambazo zinajengwa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega katikati akipoka vifaa vya maabara vya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo ambavyo vitasaidia kufanikisha juhudi za kupambana na magonjwa kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akisoma hotuba yake katika hafla ya kupokea vifaa mbalimbali vya maabara vya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo ambavyo vitasaidia kufanikisha juhudi za kupambana na magonjwa leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akivikagua vifaa mbalimbali vya maabara vya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo alivyo vipokea kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)
Mwakilishi kutoka FAO ambaye ni Mkuu wa Mradi wa Ajenda ya Dunia ya Usalama wa Afya (GHSA), Folorunso Fasina akisoma hotuba yake katika hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali vya maabara vya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania, Profesa Hezron Nonga akifafanua jambo katika hafla hiyo.
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment