TAKUKURU yaanza kuwahenyesha viongozi na watendaji wa vijiji wadokozi, DC apigilia msumari
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa(TAKUKURU) mkoani Lindi imesema hivi karibu itaanza kufuatilia mali za vijiji na mitaa ambazo zimehujumiwa na kuibiwa na viongozi na watendaji wa mitaa na vijiji.
Hayo yameelezwa leo na mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Lindi, Steven Chami kijijini Chikonji alipokuwa anakabidhi kwa mkuu wa wilaya ya Lindi shilingi 3.7 milioni ambazo zimerejeshwa na waliokuwa wanakamati wa mradi wa trekta la kijiji ambazo walitumia kinyume na taratibu.
Chami ambaye licha ya kukabidhi kiasi hicho cha fedha kilichokwapuliwa, alikabidhi nyaraka za viwanja viwili vilivyoporwa alisema katika kuhakikisha mali za vijiji na mitaa na fedha zilizoibwa zinarejeshwa wataanza kufuatilia ili waliopora warejeshe.
Alisema taasisi hiyo imebaini kuna mali nyingi na fedha za vijiji zimeporwa na viongozi na watendaji. Kwahiyo itaanza zoezi la kuwasaka waliopora fedha na mali hizo.
Katika hali iliyoonesha taasisi hiyo imedhamiria kuwashughulikia kikamilifu viongozi na watendaji wasio waaminifu alitoa wito kwa viongozi na watendaji wanaojijua kama wamepora mali au fedha za vijiji na mitaa warejeshe haraka kabla taasisi hiyo haijawafikia na kuwaadabisha kwa mujibu wa sheria.
Alisema baadhi ya watendaji na viongozi wamediriki kuuza hata maeneo ya vijiji na mitaa. Huku wengine wamejinufaisha binafsi na fedha zilizotokana na miradi mbalimbali ya mitaa na vijiji.
'' Viongozi na watendaji mnatakiwa kuepuka tamaa na ubinafsi. Haiwezekani mnakusanya shilingi milioni tatu na laki saba halafu mnagawana wakati mnajua ni fedha za umma. Hiyo haikubaliki,'' Chami alionya na kusisitiza.
Alibainisha kwamba licha ya watendaji kulipwa mishahara ili wahudumie wananchi lakini taasisi hiyo imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba baadhi ya watendaji wanaomba rushwa ili wahudumiwe.
Aidha Chami alitahadharisha kwamba watendaji wa kata wasithubutu kuiba mali na fedha katika kipindi ambacho kutakuwa hakuna madiwani. Kwani taasisi hiyo itawafuatilia kwakaribu ili wasitumie vibaya nafasi hiyo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ambaye alikabidhi nyaraka za viwanja na fedha hizo kwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, aliiagiza taasisi hiyo ichukue hatua zaidi kwa wanaorejesha mali na fedha.
Alisema kurejesha hakutoshi kukomesha tabia hiyo. Bali wakirejesha wafunguliwe mashtaka ili wengine wanaotamani kuiba waone na wajue kwamba wakiiba watalipa na kushtakiwa.
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Leave Comments
Post a Comment