RITA YATOA PUNGUZO LA BEI YA VYETI, WANANCHI WAJITOKEZA KWA WINGI
RITA YATOA PUNGUZO LA BEI YA VYETI, WANANCHI WAJITOKEZA KWA WINGI
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika banda lao ndani ya Viwanja vya maonesho ya 44 ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam
Akizungumza na Michuzi Blog, Msajili wa Rita Hamida Thabit amesema kuwa zoezi la usajili linaendelea vizuri na wananchi wengi wamejitokeza kupata huduma hiyo.
Amesema, katika banda lao wanatoa huduma za usajili wa vizazi, vifo, ndoa, mirathi, kusajili bozi za wadhamini na hata kutoa ushauri kwa wananchi watakaohitaji.
Hamida amesema, kwa mwaka huu ndani ya Viwanja vya Sabasaba RITA wameendelea kutoa huduma hizo na kuwataka wananchi waendelee kuja kwa wingi kupata huduma za usajili kwani hata gharama zimepunguzwa.
"Kwa mwaka huu gharama zimepunguzwa tofauti na ukija ofisini kwetu, hapa usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa wakubwa na watoto vyote vinapatikana kwa bei sawa ya 10,000,"
Aidha, amessma wameweka kiwango hicho ili kila mwananchi apate cheti kwa njia rahisi na huduma hiyo itaendelea kupatikana hadi kufungwa kwa maonesho hayo Julai 13.
Hamida ameongezea kuwa, kwa cheti cha mtoto mzazi anahitajika aje na kadi la Klinik au tangazo la kuzaliwa, na kwa mtu mzima atahitajika aje na kitambulisho cha kupigia kura au cha Taifa, barua za serikali za mitaa na kwa wengine waje na cheti cha shule.
RITA wameendelea kutoa huduma hiyo ambapo wananchi wengi wameonesha kufurahishwa na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya na kurahisisha upatikanaji wa vyeti.
Msajili wa RITA Hamida Thabit akitoa huduma kwa mwananchi aliyefika katika banda lao ndani ya maonesho ya 44 ya Sabasaba yanayoendelea ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam
Wananchi wakiendelea kupata huduma ndani ya banda la RITA katika maonesho ya 44 ya Sabasaba ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment