BEFORE I DIE SEHEMU YA 3
“Ndugu wageni waalikwa mabibi na mabwana ,nakosa neno la kuweza kuelezea furaha yangu kwa makaribisho haya makubwa.Sikutegemea kama ningeweza kupata makaribisho makubwa kama haya.Kitu kimoja ninachoweza kukisema toka moyoni mwangu ni Ahsanteni sana kwa kuja katika sherehe hii.Kuna msemo usemao nyumbani ni nyumbani na mkataa kwako mtumwa.Ni kwa kuzingatia misemo hii ndiyo maana nikachagua kurudi na kuishi nyumbani Tanzania badala ya kuishi na kufanya kazi katika nchi za kigeni.Nimerudi nyumbani kusaidiana na watanzania wenzangu katika kuijenga nchi yetu,kuinua uchumi wetu.Nitatumia ujuzi na maarifa yote niliyoyapata katika kuhakikisha tunapiga hatua kimaendeleo. Japokuwa hapa si mahala pake kulisema hili lakini kwa wale ndugu zangu wa kampuni nitakayokuja kuisimamia,naomba niseme kuwa muwe na amani na ninaahidi kushirikiana nanyi kwa moyo mmoja kwa manufaa ya kampuni yetu,jamii na nchi yetu kwa ujumla.Mabibi na mabwana sina cha kuongezea zaidi ya kuwashukuru sana kwa kuja kwenu .Naomba tuendelee na sherehe hizi kwa amani na utulivu.Ahsanteni sana”
Makofi na vigele gele vikasikika katika kila kona ya ukumbi.Watu waimshangilia Innocent kwa maneno machache aliyoyatoa.Sherehe zikaendelea hadi usiku mwingi halafu watu wakatawanyika na kurudi majumbani kwao.
ENDELEA…………………………………….
Ni jumapili siku iliyofuata baada ya kuhudhuria ibada ya misa Innocent akarejea nyumbani.Sebuleni akakutana na dada yake Sarah ambaye alikuwa na macho yaliyojaa uchovu.
“Pole sana” Innocent akamwambia Sarah huku akicheka
“Du! sherehe ya jana ilikuwa si mchezo.Hapa nahisi kizungu zungu kwa pombe nilizokunywa.” Saraha akasema
“jana ulikunywa sana pombe”
“Du! Jana nilikuwa na kampani yangu tulikunywa pombe kupita maelezo.Si unajua nafasi kama ile kupatikana huwa ni mara chache sana.Hapa nyumbani baba haruhusu mtu kuja amelewa.Nahitaji kunywa supu naomba uniitie hawa wasichana wakanitengenezee supu” Sarah akasema huku akikilaza kichwa chake sofani.
Innocent akamwangalia na kutabasamu.
“Sabrinaa…!! Sabrinaa..!! “
Saraha akaita kwa sauti kubwa.
“Beeee dada !! “ Sabrina akaitika toka nje,akaja mbio.
“Unafanya kazi gani? Sarah akauliza
“Ninafua dada” Sabrina akajibu kwa adabu
“acha kufua,nenda kwanza kaniandalie supu mara moja” Sarah akaamrisha
“Sawa dada” Sabrina akaitikia.
“No ! Sabrina nenda kaendelee na kazi zako.Nitamtengenezea hiyo supu mimi” Innocent akasema.Sabrina akamtazama Innocent kwa uoga.
“Nimekwambia nenda kaendelee na kazi uliyokuwa ukiifanya.Nitakwenda mimi kumtengenezea supu” Akasema tena Inno na Sabrina akaondoka
“Nashindwa kukuelewa Inno.Toka umekuja unawapa kiburi sana hawa wasichana.” Sarah akalalamika
“Si kweli kwamba ninawapa kiburi,bali siridhishwi kwa jinsi mnavyowatendea.Hawa nao ni binadamu kama sisi na tuna kila sababu ya kuwapenda na kuwaheshimu kama sehemu ya familia yetu.” Innocent akajibu
“Shauri lako kama hutaki kutusikia tunavyokwambia.Hawa ni wagonjwa kaa nao mbali kabisa.”
Innocent hakujibu kitu akaondoka na kuelekea jikoni kumuandalia dada yake supu.Supu ilipokuwa tayari akampelekea dada yake halafu akatoka nje Sabrina alikokuwa anafua.
“Sabrina, mtaarifu na Grace kuwa leo mmalize kazi zenu mapema tutatoka kwa matembezi baadae”
Sabrina akaacha kufua akamtazama Innocent kwa macho ya mshangao halafu akatabasamu na kusema.
“kaka Innocent ,nimefurahi sana kusikia unataka kutoka na sisi kwa sababu haijawahi kutokea hata siku moja tukaenda matembezi.Lakini naona utaenda na Grace kwa sababu leo ni zamu yangu kuwa jikoni na siku kama hii ya leo ambayo mama huwa anashinda nyumbani huwa anataka chakula kisichelewe Iwapo nitaondoka na kuchelewa kurudi nitasababisha ugomvi mkubwa na mama.”
“Sawa Sabrina kama ndiyo hivyo usijali tutakwenda siku nyingine,mtaarifu Grace ajiandae“
Saa tisa za alasiri Innocent akaazima gari la dada yake akamchukua mbwa wake Pura pamoja na Grace wakaingia garini na kuondoka kwenda kutembea.
“Umependeza sana Grace.Sikujua kama u mrembo namna hiyo”Innocent akasema na kumfanya Grace atabasamu na kusema
“Ahsante kaka Innocent.”
“Unafaa kabisa kuwa mrembo wa Taifa” Innocent akatania na kumfanya Grace acheke kwa nguvu.
“Sio utani Grace leo umependeza sana.”
“kaka Innocent unapenda sana utani.Mimi niwe mrembo wa Taifa? Grace akasema na kuendelea kucheka kwa nguvu
“Ndiyo unaweza ukawa mrembo wa Taifa.Una vigezo vyote vya kukufanya uwe mrembo wa juu .Una umbo zuri la uanamitindo,urefu unaotakiwa,tabasamu zuri la kiafrika tatizo ninaloliona mimi ni kwamba bado hujiamini”
“Si kwamba sijiamini kaka Innocent.mambo kama hayo tumeshayaacha kwa watu wenye uwezo wao mkubwa na elimu ya kutosha.Mtu kama mimi maisha yangu yameshakuwa hivi,sifikirii chochote katika maisha yaliyobakia”
“Kwani Grace una elimu gani?”
“Elimu yangu mimi ni darasa la saba.Kwa elimu yangu mimi siwezi kuwa kama hivyo unavyosema.”
Innocent akamtazama Grace ambaye kwa sasa alikuwa ameinama,macho yake yalionyesha majonzi makubwa.
“Grace nakuomba ukirudi nyumbani leo hebu kaa katika kioo na ujitazame jinsi ulivyo mrembo.Nina kuhakikishia kuwa unaweza ukafanya mambo makubwa hadi watu wakabaki wakishangaa” Innocent akajaribu kumpa moyo grace.
“kaka Innocent,mimi nimekwisha kata tamaa na maisha yangu.Sifikirii kufanya jambo lolote lile na ndio maana unaona pamoja na kwamba mama ni mkali lakini ninajitahidi kumvumilia kwa sababu sina tena tumaini lolote katika maisha haya.Sina mahala pa kwenda,sina wazazi na wala sina kipato ninachoweza kusema ninaweza kufanya hata biashara ya kukaanga samaki”
Kimya kikapita.Innocent akageuka na kumtazama mbwa wake Pura aliyemuweka sehemu ya nyuma ya gari ,akakanyaga mafuta na kuyapita magari mawili yaliyokuwa mbele yao halafu akamgeukia Grace.
“Grace kama hutajali unaweza kunielezea historia ya maisha yako japo kwa ufupi?”
Grace akainama akafuta machozi.
“Hapana sijasema ulie Grace.nyamaza kulia na unieleze historia ya maisha yako kama utakuwa tayari”Innocent akasisitiza
“kaka inocent,historia ya maisha yangu ni ndefu na yenye kusikitisha sana.”Grace akasema
“Naomba unieleze tafadhali” Innocent akasema
“Nilizaliwa mkoani Iringa katika kijiji cha Nyororo.Sikumjua mama yangu.Nilielezwa kwamba mama yangu alifariki nikiwa mtoto wa miezi mitatu hivyo ikamlazimu baba kuoa mwanamke mwingine wa kunilea..Nikiwa darasa la tatu baba yangu alipata ajali ya kugongwa na nyoka akiwa shambani,akafariki dunia .Toka hapo maisha yangu yalibadilika ghafla baada ya kubaki nikilelewa na mama wa kambo.Ni kipindi cha mateso makubwa niliyoyapata toka kwa mama wa kambo.Nilipata mateso makubwa ambayo nashindwa hata kuyaelezea.Nilivumilia yote hadi nilipomaliza darasa la saba.Sikuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari.Nilibaki nikifanya kazi za nyumbani na vibarua vya kupalilia mashamba ya watu na hela yote mama akachukua.Sikuwa hata na nguo za kuvaa.Pamoja na hayo yote bado nilimpenda mama yangu na kumheshimu kwani ndiye mama pekee aliyenilea..
Siku moja alikuja mama mmoja ambaye alikuwa akitafuta mtumishi wa ndani.Mama akaniuza kwa shilingi laki tano.Japokuwa nilitoa machozi kwa kufanywa kama bidhaa lakini kwa upande mwingine nilishukuru Mungu kwani niliamini ule ungekuwa ni mwanzo wangu wa kuondokana na dhiki ile kubwa ya nyumbani kwetu.Nililetwa Dar es salaam na kuanza kufanya kazi za ndani kwa mama yule aliyenitoa Iringa.Baada ya wiki mbili mama yule akaniuza tena kwa mama mmoja wa kihindi.Nikawa nafanya kazi pale.Nilipata manyayaso makubwa sana katika familia ile.Baba mwenye ile nyumba alikuwa akija na kunilazimisha kufanya naye mapenzi kila siku kwa kigezo kwamba nikikataa atanifukuza kazi.Sikuwa na mwenyeji wala ndugu yeyote hapa dar hivyo ikanilazimu kukubali kufanya naye uchafu ule.Nilipoona sintaweza kuvumilia tena nikatoroka na kuingia mtaani.Sikuwa na mahala pa kula wala kulala.Nikiwa njiani usiku wa saa tatu nikakoswa kugongwa na gari.Mzee yule aliyetaka kunigonga alinitazama akagundua kuwa nilikuwa na matatizo.Baada ya kunihoji nikamuelezea historia nzima ya maisha yangu,akanionea huruma akanichukua hadi nyumbani kwake.Mzee huyu ni baba yako.Nilianza kuishi pale kwenu na kusaidia kazi za nyumbani.Siku moja mmoja kati ya walinzi wa baba alinibaka,nikamsemea kwa baba akamfukuza kazi.Nililia sana baada ya kusikia kuwa mlinzi yule alikuwa ameathirika na virusi vya ukimwi.Baadae nilianza kusumbuliwa na maradhi ya mara kwa mara.Nilikuwa naumwa,nakohoa na kutapika Mama akasema nilikuwa nimeambukizwa ukimwi tayari.Toka wakati huo nimekata tama na maisha yangu ninasubiri siku ya kufa kwangu……………..” Grace akashindwa kuendelea akaanza kulia.
“Nyamaza kulia Grace.Tutaongea zaidi nikisha egesha gari” Innocent akasema huku akikata kona kuingia Salama beach resort..
Salama beach resort ni moja kati sehemu tulivu kandoni mwa bahari ya hindi .Pamoja na usalama na utulivu uliokuwapo mahala hapa,kilichowavutia watu zaidi ni kuwa na ufukwe mzuri na msafi.Mamia ya wakazi wa Dar es salaam walikuwa wakija hapa kila mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kupumzika na kupata hewa safi.Siku hii ya jumapili idadi ya watu ilikuwa kubwa kama kawaida.
Innocent akapaki gari akafungua mlango akashuka halafu akazunguka akafungua mlango wa upande aliokaa Grace akashuka.Macho yake yalikuwa mekundu kwa machozi.Innocent akamwangalia bila kusema kitu halafu akazunguka gari na kumfungulia mbwa wake Pura akamshika mkanda akamshusha garini.
“Beba huu mfuko wa vinywaji tukakae katika jiwe lile kulee” Innocent akamwambia Grace
Wakaanza kutembea taratibu kuelekea katika moja ya jiwe ambalo Inno alichagua wakakae.Wakalifikia jiwe lile wakakaa na kuifurahia mandhari nzuri na upepo mwanana wa bahari.
“Sijawahi kufika sehemu kama hii.Toka nimefika hapa Dar es salaam nimekuwa nikiisikia bahari au kuiona kwenye runinga lakini sijawahi kuiona kwa macho.” Grace akasema na kumfanya Innocent atabasamu.
“Unajua kuogelea? Innocent akauliza.na kumfanya Grace acheke kwa nguvu
“kaka Innocent,kwetu Iringa hakuna bahari.Ningejua vipi kuogelea na isitoshe hata kama tungejaaliwa kuwa na bahari au ziwa nisingekuwa na huo muda wa kwenda kuogelea.Nilipokuwa nyumbani muda wote ilikuwa ni kazi tu.”
“Umenifurahisha sana Grace.Kujua kuogelea si lazima kuwe na bahari au ziwa.Unaweza ukajifunza hata katika mito ya msimu inayoletwa na mvua.Ningekufundisha kuogelea lakini kuanzia kesho nitaanza kazi kwa hiyo sintakuwa na muda wa kutosha.Ila siku nikipata nafasi nitawafundisha kuogelea wewe na Sabrina.”akasema Innocent
“kaka Innocent ina maana kuanzia kesho hautakuwa ukishinda nyumbani?
“Ndiyo Grace.Nitaanza kazi rasmi kesho kwa hiyo tutakuwa tukionana mida ya usiku tu.Nita wamiss sana wewe na Sabrina”
Grace hakujibu kitu akainua kopo lake la Juice ya maembe akanywa kidogo.Alipoliweka chini Innocent akasema.
“Grace ulinielezea historia yako nikasikia uchungu sana.Dunia hii ina watu mabaradhuli kupita maelezo.Pole sana kwa yote yaliyotokea.Hiyo ndiyo mikiki mikiki ya maisha ambayo sote ni lazima tuipitie.Unachotakiwa kufanya kwa sasa hebu jaribu kuyafuta yote yaliyotokea na ufungue ukurasa mpya wa maisha yako.Amini kwamba hiyo yote iliyotokea ni mitihani ya maisha ambayo inatusaidia kuufahamu vizuri ulimwengu huu .Vile vile mitihani hii inatufanya tuwe karibu na mwenyezi Mungu na kumtumaini yeye tu.Ni yeye pekee ambaye anaweza akayabadili maisha yetu na kuwa mapya.Ni yeye anayeweza akatusahaulisha yote yaliyopita na kutuweka juu ya mataifa.Kumbuka Daudi alikuwa mchunga Kondoo lakini kwa uweza wake Mungu akawa mfalme.Mpokee na kumuamini Yesu kristo kuwa bwana na mwokozi wa maisha yako naye atakujaza uzima,atakupa amani ,atakuosha kwa damu yake na utakuwa mpya tena” Innocent akasema kwa hisia kali.Kila anapokumbuka mambo yaliyomtokea katika maisha yake Grace huwa anashindwa kujizuia kutokwa na machozi.
“kaka Innocent,sijui hata nisema nini lakini wewe ni mtu wa kwanza ambaye Mungu amekutuma uje unipe moyo wa kuendelea kupambana na mitihani ya ulimwengu huu.Toka umekuja ninajihisi kama mtu mpya.Umekuwa unanipa moyo kila siku na kunisihi nisikate tamaa.Kaka Innocent pamoja na kunifanya nijisikie amani na furaha moyoni lakini napenda nikiri kuwa kila nikifikiria juu ya hali yangu hii nakata tamaa kabisa.Kuwa muathirika wa ukimwi ninaona kama maisha yangu yote hayana thamani tena.” Machozi yakaendelea kumtoka.Innocent akamwamgalia kwa macho yake ya huruma na kusema
“Grace naomba nikuulize kitu kimoja.Katika maongezi yako yote sijasikia hata mara moja ukinitajia suala la hospitali.Je umekwisha kutana na wataalamu wa ushauri ukapatiwa ushauri nasaha na jinsi ya kuishi na virusi vya ukimwi? Ninavyofahamu mimi kuwa na virusi vya ukimwi si mwisho wa maisha yako au mwisho wa ndoto zako.Iwapo utafuata ushauri wa wataalamu unaweza ukaishi maisha marefu sana na ukatimiza ndoto zako zote maishani .”
“Kaka Iinocent kusema ukweli sijakwenda hospitali yoyote” Grace akasema kwa sauti ya chini
“Kwani siku ulipopima na ukakutwa umeathirika walikupa ushauri gani.Hawakukwambia kitu chochote? Innocent akadadisi
“Kusema ukweli kaka Innocent mimi sijakwenda hospitali yoyote kupima “
“Whaaat!!!….” Innocent akauliza kwa mshangao
“Unasema hujakwenda hospitali yoyote kupima ? Inno akauliza
“Ndiyo Kaka Innocent”
Jibu lile linamfanya Innocent avute pumzi ndefu.
“sasa umejuaje kama umeathirika ?
“baada ya kubakwa na yule mlinzi, kilipita kipindi cha kama mwaka mmoja na miezi mitatu hivi nikaanza kuumwa ,nikawa natapika na kuharisha.Nikaenda hospitali nikapewa dawa nikapona.Baada ya mwezi nikaanza kuumwa tena.Toka hapo homa za mara kwa mara zikawa hazikatiki,nikadhoofu na kukonda sana.Mama akaniambia tayari nilikuwa nimeshaathirika.Sikutaka hata kwenda hospitali kupima kwa sababu sikuona haja.Kama nilibakwa na mtu mwenye ukimwi basi ni wazi na mimi nitakuwa nina ukimwi
TUKUTANE SEHEMU IJAYO………
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment