Sunday, 16 March

Ads Right Header

Buy template blogger

BEFORE I DIE SEHEMU YA 5


LOVE ME NOW BEFORE I DIE!!! - iaspireBlogILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Grace akakosa neno la kusema akakaa kitandani huku bado akilia.Innocent akakaa karibu yake akatoa kitambaa na kumfuta machozi.
“usilie Grace.hebu nieleze kuna tatizo gani?
“nashindwa hata niseme kitu gani kaka Innocent ” Grace akasema
“Kaza moyo.Nieleze.Niko hapa kukusaidia.Niambie tafadhali nini kimetokea? Majibu yanasemaje?
Grace akafungua mkoba wake na kutoa karatasi za majibu akampa Innocent.
“Soma mwenyewe,mimi sijui kiingereza.”
Innocent akaanza kuzipitia karatasi zile moja baada ya nyingine ghafla akajikuta akiachia tabasamu pana ,moyo ukaanza kumwenda mbio na machozi ya furaha yakimchuruzika.
“You are HIV negative…you are negative…ooh My God you are negative…” akasema Innocent
ENDELEA………………………………
Akamkumbatia Gace kwa nguvu huku naye machozi ya furaha yakimtoka.
“Grace huna ukimwi..huna ukimwi…Thank you God..thank you Jesus”
Innocent akasema kwa furaha huku amesimama na kumshukuru Mungu.
“Mungu baba wa mbinguni,ambaye kwako hakuna jambo lolote linaloshindikana,wewe unayeweza kutamka neno na kitu kikawa.Uliumba dunia na kila kilichomo ndani yake kwa kauli yako moja tu.Baba ninakushukuru sana kwa muujiza uliotuonyesha hapa leo.Umedhihirisha wewe ni mtukufu wewe ni mwenye enzi.Baba mwanao amekuwa akiteseka kwa muda mrefu akidhani ana maradhi haya ya ukimwi kumbe hana,baba ninashukuru kwa kutupa mwanga huu na kwa sasa baba wa majeshi ingia ndani yake na umfanye upya tena.Anapoenda kuyaanza maisha yake mapya baba mtume roho wako akae naye na kumuongoza katika njia zote njema na umbariki aweze kuwa na maisha mazuri yenye kukupendeza wewe peke yako bwana wa majeshi unayestahili kusifiwa na kuabudiwa,katika jina la Yesu ..Amen.
Baada ya maombi yale mafupi akatoa kitambaa akafuta machozi halafu akamwendea Grace aliyekuwa amekaa kitandani.
“Dada yangu ,bwana amekufungua na kukufanya mpya tena.Mwili wako ni safi na roho wake ataendelea kukuongoza.Hongera sana dada Grace.” Inno akasema huku akimpiga piga Grace mgongoni.
“kaka Innocent nadhani ni Mungu alikurudisha ili uweze kuyarejesha maisha yangu katika tumaini .Nimeteseka vya kutosha na nilikwisha kata tamaa ya kuendelea kuishi tena.Sijui hata nitakulipa kitu gani kaka Innocent kwa sababu wewe ndiye mtu wa kwanza kunipa ushauri wa kuja kuangalia afya yangu…” Grace akaendelea kulia.
“Nyamaza kulia Grace.hutakiwi kulia tena.Unatakiwa uyaanze maisha mapya ya furaha na amani.Leo umekuwa kiumbe mpya.”
Innocent akaenda kuonana na daktari na kumuuliza kama anaweza akaruhusiwa kuondoka na dada yake.Daktari akamruhusu,wakaingia garini na kuondoka.Wakiwa ndani ya gari Innocent akapiga simu nyumbani kwao iliyopokelewa na Sabrina.
“Hallo Sabrina nataka leo jioni uandae chakula safi.Chinja kuku andaa chakula kitamu kuna jambo kubwa na zuri la kusherehekea jioni ya leo kama famila.”
Mchana huo Innocent akawa akizunguka katika maduka mbali mbali yanayouza nguo na urembo,akawanunulia Grace na Sabrina nguo pamoja na kumpeleka Grace saluni ambako alipambwa ,akapambika,kiasi kwamba kama ulimuona asubuhi basi ungempotea katika muonekano huu mpya.
“wow ! I knew it you are so pretty.I knew it” Innocent akaongea kwa mshangao mara tu baada ya kumuona katika muonekano mpya.Grace hakusema kitu akabaki akitabasamu.
“Umependeza sana Grace.”
“ahsante kaka Innocent. “
saa kumi na mbili za jioni wakawasili nyumbani.Innocent akamfungulia mlango Grace akashuka.wa kwanza kumuona alikuwa ni Sabrina,akastuka sana.
“ouh Grace ni wewe kweli? Umebadilika ,umependeza sana.Sukujua kama ni wewe.”
Kabla Grace hajajibu kitu mama yake Innocent akatokea akiwa amefura kwa hasira.
“Na wewe umekuwa bosi siku hizi mpaka unarudi saa hizi? Unategemea kazi za nyumbani akufanyie nani? ….
“Mama nilikuwa nimekwe……….”
Kabla Grace hajamaliza kujibu Innocent akadakia.
“Alikuwa na mimi mama.Nilimpeleka hospitali na baadae nikampitishia saluni.Grace nendeni ndani”
mama yake akamwangalia Inno kwa hasira akasema
“Nakwambia unachokitafuta kwa huyo Malaya utakipata.Kila siku ninakuonya usiwe karibu na huyo chokoraa hutaki kusikia”
maneno yale yanamuudhi Innocent akajibu.
“mama tafadhali usimuite Grace Malaya.Huyu ni sawa na mwanao.Amekukosea kitu gani mama? Au anavyokaa hapa anakunyima kitu gani?
“Usinijibu hivyo Innocent.Naona huko Ulaya ulikotoka wamekufundisha vibaya sana.Wewe si wa kusimama na kuanza kujibizana na mimi.” Mama yake Inno akasema kwa hasira
“Sijibizani nawe mama yangu,ila ninajaribu kukuelewesha kuwa hawa Grace na Sabrina ni sehemu ya familia yetu…. Kabla hajamaliza kaka yake Edson anatokea.
“Wow brother” akasema Inno kisha wakakumbatiana kwa furaha.
“naona mzungu umerudi nyumbani” Edson akatania wote wakacheka.
“Vipi mbona nasikia makelele huku nje? Edson akauliza
“Huyu mdogo wako toka amekuja amekuwa akiwapa kiburi sana hawa wasichana.Toka Inno amerudi wasichana hawa wamekuwa na kiburi hawataki kunisikia hata kidogo.Muonye mdogo wako akae mbali na hawa wasichana” mama yake Inno akasema kwa ukali
“Inno mbona unamkorofisha mama namna hiyo? Edson akauliza
“Si hivyo brother ,tatizo ni kwamba hawa wasichana wanakaa humu,wanasaidia kazi za ndani lakini hakuna mtu yeyote anayewajali.Wamekuwa wakinyanyaswa na kubaguliwa kitu ambacho mimi, sikipendi”
Edson na Innocent wakaingia ndani na kumuacha mama yao pale nje amefura kwa hasira.
Saa mbili za usiku tayari meza ilikwisha andaliwa.Kila mmoja alikuwa akijiuliza nini ilikuwa sababu ya furaha ile ya Innocent. Innocent akaleta shampeni akaweka mezani halafu familia yote ikakusanyika mezani kwa ajili ya chakula cha usiku isipokuwa Grace na Sabrina ambao wao hulia chakula chao jikoni.kabla hawajaanza kula Innocent akasema
“jamani kabla hatujaanza kula chakula hiki,napenda niwafahamishe kwamba chakula hiki ni mahsusi kwa ajili ya kusherehekea mwanzo wa siku mpya na maisha mapya ya mmoja wa wanafamilia hii.”
Kila mmoja akamkazia macho Inno bila kuelewa alikuwa akimaanisha kitu gani.
Innocent akaenda jikoni na kuwaleta Grace na Sabrina akawakaribisha mezani.
“baba na mama,kaka Eddy na dada sarah,leo mmoja kati ya dada zetu hawa ameyaanza maisha mapya .Grace leo amepima afya na amekutwa hana maambukizi ya virusi vya ukimwi.Yuko mzima kabisa na ushahidi huu hapa”
Innocent akasema na kuweka mezani karatasi za majibu ya vipimo toka hospitali .Kila mmoja akapigwa na butwaa.
“Napenda tokea sasa mtambue kwamba Grace si muathirika wa virusi vya ukimwi na kwa maana hiyo basi anaanza maisha mapya na ningeomba watu wote humu ndani tumpe ushirikiano katika maisha mapya atakayoyaanza.Ni mapema bado kusema ni maisha ya namna gani atayaanza kwa sababu bado naangalia ni kitu gani cha kumsaidia ili aweze kuyaendesha maisha yake.”
Innocent akafungua shampeni wakashangilia na kumpongeza Grace isipokuwa mama yake Inno aliyekuwa amefura kwa hasira.
* * * *
Siku nne zimepita toka Grace alipopima afya yake na kujikuta hana maambukizi ya virusi vya ukimwi.Maisha yake yaliendelea kuwa ya furaha japokuwa bado alikuwa akikumbana na vikwazo vingi toka kwa mama yake Innocent.Kwa kufuata ushauri wa Innocent aliendelea kuwa mtulivu na mvumilivu wa manyanyaso yote aliyofanyiwa.
Ni siku ya alhamisi asubuhi na mapema,Innocent akijiandaa kupanda gari tayari kwa kuwahi ofisini,Grace akamfuata mbio.
“Kaka Innocent samahani kwa kukusumbua.Unajua toka umeanza kazi umekuwa haupatikani sana hapa nyumbani.Wiki yote hii nimekuwa nikitafuta nafasi ya kukuona na kukwambia kuwa nina maongezi na wewe pindi upatapo nafasi.Naomba kaka Innocent ukipata nafasi hata muda wa jioni uniambie nina maongezi na wewe ya muhimu” Grace akasema huku akitazama chini.Innocent akamshika bega na kumwambia.
“Usijali Grace.Kwa sasa nina kazi nyingi sana ofisini lakini nitajitahidi kutafuta muda ili tukae tuongee.Vipi lakini maisha yanakwendaje hapa nyumbani?
Huku akijitahidi kuuficha uso wake Grace akajibu
“Hapa nyumbani maisha ni kama kawaida.Nimeshayazoea”
“Sawa , Grace ngoja mimi niwahi ofisini halafu nikipata muda tutakaa tutaongea.”
“Ahsante kaka Innocent.Kazi njema”
Innocent akaingia katika gari lake na kuondoka kuelekea kazini.
“Nimeanza kuyaona mabadiliko kwa Grace.Kwa siku hizi chache toka apate majibu ya vipimo vyake amebadilika sana.Ninaiona nuru ya matumaini katika macho yake.Ninaona ni jinsi gani alivyo na shauku ya kuyaanza maisha yake mapya niliyomuahidi.Ni lazima nimsaidie binti yule ili aweze kutimiza ndoto zake maishani.” Innocent akawaza akiwa ndani ya gari kuelekea kazini.
Kwa siku chache toka Innocent alipokamata uongozi katika kampuni hii ya kutengeneza maji ya kunywa,hali ya kiutendaji imebadilika sana.Wafanyakazi wamekuwa na mwamko mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii wakiwa na matumaini makubwa ya kuboreshewa mishahara yao ahadi waliyopewa na na kiongozi wao mpya.Mabadiliko haya ya utendaji kazi miongoni mwa wafanyakazi yalimpa moyo sana Innocent na kumfanya aamini kuwa muda si mrefu uzalishaji utaongezeka na hivyo kuboresha zaidi hali za maisha ya wafanyakazi.
Asubuhi hii wafanyakazi wote walikwisha wahi katika sehemu zao za kazi na kazi iliendelea kufanyika.Innocent akasalimiana na baadhi ya wafanyakazi halafu akaingia ofisini kwake akaendelea na kazi zake.Akiwa ofisini kwake mara kwa mbali akasikia kama kuna mabishano katika ofisi ya katibu muhtasi wake,akaacha alichokuwa akikifanya akafungua mlango na kumkuta katibu wake akibishana na mama mtu mzima ambaye ni mmoja kati ya wafanyakazi wa kampuni hiyo.
“Kuna nini hapa Devotha? Innocent akauliza.
“Bosi kuna huyu mama hapa amekuja analazimisha kutaka kukuona nikamuuliza kama ana miadi na wewe akasema hana nikamuuliza ana shida gani akasema ni shida binafsi,basi ndiyo nikawa najaribu kumuelewesha utaratibu ulivyo wa kukuona lakini yeye bado hanielewi.” Devotha katibu muhtasi wa Innocent akasema.
“Basi mruhusu mama aingie ofisini.halafu Devotha usimzuie mfanyakazi yeyote kuja kuonana na mimi.Awe na shida yoyote ya kiofisi au binafsi.Kama nipo mruhusu kila mtu anione.Sawa?
“Sawa bosi” Devotha akasema huku akionyesha kuchukizwa na kitendo cha mama yule kubishana naye hadi akakutwa na bosi wake.
“Mama shikamoo.” Akasema Innocent huku akimuelekeza mama yule aketi kitini.
“Marahaba baba.habari za kazi”
“Habari za kazi nzuri mama yangu..Karibu sana sijui una tatizo gani?
“Baba mimi naitwa Mama Sophia.Ni mfanyakazi wa kampuni hii,sisi ndio tunaosafisha chupa za kuwekea maji.Mimi ni mjane na nina watoto wanne.Tatizo nililonalo baba yangu ni kwamba mwanangu wa kwanza ameshindwa kwenda shule kutokana na ukosefu wa fedha.Amechaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano katika shule ya bweni lakini mpaka sasa hivi ninavyokueleza ni kwamba hajafanikiwa kwenda shule kutokana na kukosekana kwa fedha ya kulipia huko shuleni.Nimekuja hapa kwako baba uone ni jinsi gani unaweza ukanisaidia ili mwanangu aweze kwenda shule kuendelea na masomo.Ikiwezekana naomba nikopeshwe fedha halafu nikatwe katika mshahara wa mwisho wa mwezi.Naomba unisaidie baba kwa sababu hapa nilipo niko mwenyewe sina msaada toka sehemu yoyote ile.Kazi hii niifanyayo hapa ndiyo kila kitu kwangu.”
Mama Sophia akajieleza kwa upole.Innocent akamsikiliza mama yule kwa makini na aliyoyasema yakamuingia moyoni,akamuonea huruma sana mama yule mjane.
“mama nimekusikia.Kwanza pole sana kwa matatizo na vile vile nikupe hongera kwa kuweza kumudu kulea na kuwasomesha watoto wako wote wanne wewe mwenyewe.Nakupongeza kwa sababu elimu ndiyo msingi bora wa maisha yao.Mama kwa kweli suala lako limenigusa sana.lakini pamoja na kuguswa huko mama yangu napenda nikufahamishe kuwa kwa sasa hali ya kampuni si nzuri kifedha kama nilivyowaeleza siku chache zilizopita.Nina imani kuwa kwa siku chache zijazo uzalishaji ukiongezeka basi tutakuwa sehemu nzuri kifedha.Pamoja na hayo mama yangu hebu niachie suala hili ili nione ni jinsi gani ninaweza kukusaidia.Naomba unipe siku ya leo nishughulike na suala lako.Hata kama nikikosa nitajitahidi kutafuta sehemu yoyote ile ili tufanikishe mwanao aende shule.Mama fedha hizo zitakuwa si mkopo bali nitakusaidia kama mama yangu .”Innocent akasema
“baba nashukuru sana kwa msaada wako.Sijui hata nikushukuruje lakini nakuombea kwa Mungu akubariki na kukuzidishia kwa moyo wako wa huruma.” Akasema mama Sophia huku akisimama na kuondoka.
“Kuna kila sababu ya kuboresha maisha ya wafanyakazi.Huyu mama amekuwa jasiri kuja kunieleza tatizo lake,lakini nina imani kuwa wapo wengine ambao hawana ujasiri wa kunieleza matatizo yao.Nitajitahidi kwa kila niwezavyo kuboresha mishahara na stahili zao nyingine ili maisha yao yaweze kuboreka.” Innocent akawaza. Halafu akaendelea na kazi .
TUKUTANE SEHEMU IJAYO……



  NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇

Leave Comments

Post a Comment

Ads Post 4