Sunday, 16 March

Ads Right Header

Buy template blogger

BEFORE I DIE SEHEMU YA 6


LOVE ME NOW BEFORE I DIE!!! - iaspireBlogILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“mama nimekusikia.Kwanza pole sana kwa matatizo na vile vile nikupe hongera kwa kuweza kumudu kulea na kuwasomesha watoto wako wote wanne wewe mwenyewe.Nakupongeza kwa sababu elimu ndiyo msingi bora wa maisha yao.Mama kwa kweli suala lako limenigusa sana.lakini pamoja na kuguswa huko mama yangu napenda nikufahamishe kuwa kwa sasa hali ya kampuni si nzuri kifedha kama nilivyowaeleza siku chache zilizopita.Nina imani kuwa kwa siku chache zijazo uzalishaji ukiongezeka basi tutakuwa sehemu nzuri kifedha.Pamoja na hayo mama yangu hebu niachie suala hili ili nione ni jinsi gani ninaweza kukusaidia.Naomba unipe siku ya leo nishughulike na suala lako.Hata kama nikikosa nitajitahidi kutafuta sehemu yoyote ile ili tufanikishe mwanao aende shule.Mama fedha hizo zitakuwa si mkopo bali nitakusaidia kama mama yangu .”Innocent akasema
“baba nashukuru sana kwa msaada wako.Sijui hata nikushukuruje lakini nakuombea kwa Mungu akubariki na kukuzidishia kwa moyo wako wa huruma.” Akasema mama Sophia huku akisimama na kuondoka.
“Kuna kila sababu ya kuboresha maisha ya wafanyakazi.Huyu mama amekuwa jasiri kuja kunieleza tatizo lake,lakini nina imani kuwa wapo wengine ambao hawana ujasiri wa kunieleza matatizo yao.Nitajitahidi kwa kila niwezavyo kuboresha mishahara na stahili zao nyingine ili maisha yao yaweze kuboreka.” Innocent akawaza. Halafu akaendelea na kazi .
ENDELEA…………………………………..
Masaa mawili baadae akaja meneja mwajiri wa kampuni,na moja kwa moja akaingia ofisini kwa Innocent..
“Bosi kuna tatizo limetokea.”
“Tatizo gani tena Godson?
“Kuna fundi umeme mmoja anaitwa Joshua amekutwa amelewa chakari kiasi kwamba hawezi hata kufanya kazi .Kama kutatokea hitilafu yoyote ya kiufundi kwa sasa sielewi tutafanya nini.Hili ni kosa na si mara yake ya kwanza kufanya hivi.Nimekwisha muonya mara tatu sasa na kwa mujibu wa sheria za kazi ni kwamba kwa sasa kinachofuata ni kufukuzwa kazi.Kampuni haiwezi kuwavumilia watu wa namna hii ambao wanachangia kurudisha nyuma kampuni.Barua yake hii hapa imekwisha andaliwa nimekuletea utie saini yako.”
Innocent akainama akakuna kichwa akawaza na kuuliza.
“Huyu bwana amefanya kazi hapa kampuni kwa muda gani mpaka sasa?
“Huu ni mwaka wa kumi “
“Ana familia? Innocent akaulza tena
“Ndiyo.Ana familia ya mke na watoto watatu”
Innocent akakaa kimya halafu akasema
“Godson pamoja na kwamba amefanya kosa kisheria na adhabu yake ni kufukuzwa kazi hebu naomba tuiweke pembeni adhabu hii na tumpe tena nafasi nyingine.We cant afford to loose him now.We still need him.Naomba apelekwe dispensary akapumzishwe kule halafu akipata nafuu msimruhusu aondoke mpaka aonane na mimi”
“Sawa bosi.Wewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho lakini ukumbuke kuwa kuzidi kuwavumilia watu kama hawa tunazidi kulea uzembe hapa kazini”
“nakubaliana nawe Godson,lakini naomba tumpe tena nafasi ya mwisho.Kama atarudia tena kosa lake basi hatutakuwa na msaada tena.Jitahidi apumzike na asiondoke bila kuonana na mimi.” Innocent akasisitiza,Godson akaondoka lakini ni dhahiri alionyesha kutoridhishwa na maamuzi yale ya mkuu wake.
“Uongozi ni mgumu sana lakini kuna nyakati ambazo ni lazima utumie busara na ubinadamu katika maamuzi .Toka ndani ya moyo wangu siwezi kumfukuza kazi Joshua wakati ana familia inayomtegemea.Nitaongea naye halafu nione nini cha kufanya” Innocent akawaza akaendelea na kazi zake.
* * * *
Saa kumi na moja za jioni wakati wafanyakazi walioingia zamu ya asubuhi wamekwisha toka na kuwapisha wale wanaoingia zamu ya usiku,Joshua bado aliendelea kuwapo pale ofisini akimsubiri bosi wake amalize kazi zake kama alivyokuwa ameelekezwa.Alikuwa mwingi wa mawazo na alikuwa amejikunyata pembeni kama mgonjwa.Alifahamu kuwa ni lazima atafukuzwa kazi kutokana na kosa la kuwa mlevi kazini hivyo akawa akijipanga jinsi ya kuomba msamaha.
Saa kumi na mbili za jioni Innocent akatoka ofisini kwake tayari kuelekea nyumbani.Joshua aliyekuwa amekaa katika mti mkubwa wa maua alipomuona bosi wake akitoka akamkimbilia.
“Mzee samahani” Joshua akaita bada ya kumfikia Innocent
“Bila samahani” Innocent akageuka
“Mzee mimi naitwa Joshua nilipewa maagizo yako na afisa maslahi kwamba nisiondoke bali nikusubiri hadi ukimaliza kazi zako unahitaji kuonana na mimi.”
“Ouh nimekumbuka.Wewe ndiye Joshua?
“Ndiyo mimi mzee” Joshua akajibu huku ameibana mikono yake kwa nyuma.
“Ok bwana Joshua nataka unipeleke nikapaone nyumbani kwako”
Joshua akastuka ,akapatwa na baridi ya ghafla.
“Mzee nyumbani kwangu?
“Ndiyo nyumbani kwako.Nahitaji kujua mahala unapoishi” Innocent akasisitiza huku akipiga hatua kueleka liliko gari lake.Wakaingia garini na safari ya kuelekea kwa Joshua ikaanza.Njiani Joshua alikuwa ni mkimya na alionekana kuwa na mawazo mengi.hakufahamu nini dhamira ya mkuu wake wa kazi kutaka kwenda kupajua nyumbani kwake.Zaidi ya maelekezo ya njia Joshua aliyokuwa akimpa Innocent hawakuongea kitu kingine chochote.Innocent alitambua dhahiri uoga aliokuwa nao Joshua.
Hatimaye wakafika katika nyumba anayoishi Joshua.Wakashuka na kuelekea ndani
“karibu ndani bosi” Joshua akamkaribisha ndani Innocent kwa sauti ambayo ilikuwa ikitetema.
Innocent akakaribia ndani sebuleni kulikokuwa na kiza na kwa msaada wa tochi ya simu ya Joshua akaonyeshwa mahala pa kukaa.Lilikuwa ni kochi lisichokuwa na mito ya kukalia .Joshua akamwita mkewe alete taa ya chemli aliyokuwa akiitumia chumbani.Mkewe alipokuja sebuleni haraka haraka Joshua akamtambulisha kwa Innocent.
“Mama Deo leo nimekuja na mgeni.Huyu ndiye meneja wangu mpya pale kazini kwangu.” Baada ya utambulisho ule ambao ulimfanya mke wa Joshua abaki mdomo wazi Joshua akamgeukia Innocent
“Bosi huyu ndiye mke wangu,tuna watoto watatu ambao nadhani bado wanacheza huko nje.”
Innocent akasimama na kusalimiana na mke wa Joshua.
“ Nafurahi sana kukufahamu mama Deo” Innocent akasema.
“Sijui utakunywa kinywaji gani bosi? Joshua akauliza
“Nashukuru Joshua.Nitakunywa siku nyingine.Kwa vile nimekwisha pafahamu nyumbani nitakuwa nikipita hapa mara kwa mara.Mama Deo Nashukuru sana nimepafahamu nyumbani.Siku nyingine nikipata nafasi nitafika kuwasalimia.” I nnocent akasema huku akiinuka na kutoka.Joshua akamsindikiza hadi garini.
“Joshua nashukuru nimepafahamu kwako ila naomba kesho nikuone asubuhi ofisini kwangu.Kwa leo hebu chukua hizi uwanunulie watoto soda” Innocent akasema huku akiitoa pochi yake na kuhesabu noti nne za elfu kumi kumi akampatia Joshua ambaye aliona ni kama muujiza .Hakuwa ametegemea kupata kiasi kile cha fedha kwa usiku ule. Innocent akamuaga na kuondoa gari lake.
“Kwa kweli bado nina kazi kubwa ya kufanya ili kuboresha maisha ya wafanyakazi wangu.Mtu kama Joshua si kwamba anapenda kulewa lakini inambidi kutokana na maisha aliyonayo.Maisha yake yanaonekana magumu sana licha ya kwamba ana kazi inayomuingizia kipato.Ni lazima nimsaidie aondokane na maisha haya anayoyaishi.”
* * * *
Saa mbili na nusu Innocent akawasili nyumbani kwao.Akasalimiana na kila mmoja halafu akaenda bafuni kujimwagia maji.Baada ya kuoga akamwita Grace wakaelekea bustanini huku akiwa na mbwa wake Pura.
“Grace ulisema una jambo la kunieleza.”
“Kweli kaka Innocent nina jambo nilitaka nikueleze.”
“Jambo gani hilo Grace”
“Kaka Innocent baada ya kupima na kugundua hali yangu nimejikuta ninapata mwanga mpya wa kuyatengeza upya maisha yangu yaliyokwisha haribika.Kwa kuwa umri wangu bado ni mdogo na nina nguvu za kutosha sidhani kama litakuwa ni jambo la busara kuendelea kufanya kazi za ndani huku nikimtegemea mama kwa kila kitu.Kaka Innocent shida yangu kubwa ni kukuomba unitafutie japo kikazi chochote katika kampuni yako au hata kokote kule unakoweza kupata ili niweze kufanya na kujipatia kipato changu mimi mwenyewe.Kwa kuwa sina elimu ya kutosha kazi yoyote itakayopatikana mimi nitaifanya.Iwe ni kufagia,kudeki vyoo,usafi nakadhalika.Siwezi kuchagua kazi kaka Innocent naomba tafadhali unisaidie ili niweze kuyaendesha maisha yangu kwa kujtegemea” Grace akasema huku akitazama chini.Innocent akakaa kimya akatafakari.Akaziangalia nyota angani na baada ya muda aksema
“Grace wazo lako ni zuri sana.lakini ukumbuke kuwa nilikwisha kuahidi kukusaidia kuyajenga maisha yako upya wewe na sabrina.Sijaisahau ahadi yangu.Hata nikiwatafutia kazi ya kufanya kwa sasa itakuwa ni kazi ambayo haitakuwa na maslahi yoyote kutokana na elimu yenu ndogo.Kwa maana hiyo lengo langu ni kwanza kuwapeleka shule mkaendelee na masomo halafu baada ya kusoma ndipo niwatafutie kazi.Nataka muanze elimu ya sekondari haraka iwezekanavyo mara tu shule zitakapofunguliwa.kwa sasa niko katika mchakato wa kutafuta shule na pindi nitakapoipata shule nzuri itakayoniridhisha nitakutaarifuni.Tafadhali msiwe na papara na haya maisha.Bado hamjachelewa.Umri wenu una ruhusu kabisa kuyatengeneza upya maisha yenu.Naahidi kuwasaidia kwa kila hali ili muweze kufanikisha malengo yenuo na kuwa na maisha mazuri siku za usoni.”
Innocent akasema na kumfanya Grace atabasamu kwa furaha huku sura yake nzuri ikizungukwa na nuru ya matumaini ya maisha mapya.
TUKUTANE SEHEMU IJAYO…………



  NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇

Leave Comments

Post a Comment

Ads Post 4