SEPTEMBER 1 SEHEMU YA KUMI NA NNE.
:max_bytes(150000):strip_icc()/iStock-637126086-5978d78f0d327a0011b429d4.jpg)
TULIPOISHIA JANA..
Wanachi wasiyopanda walibaki wakishuhudia kwenye runinga zao, namna ambavyo Mheshimiwa ameketi kwenye behewa la hadhi huku kiyoyozi kikiwa kila mahali. Pia waliweza kuona wananchi wengine wakiwepo kwenye upande wenye ubora zaidi, hakika lilikuwa ni tukio lenye kufurahisha na kila mmoja akatoa pongezi kwa serikali kuweza kutimiza hilo suala ambalo lilikuwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu. Wabunge ambao hapo awali waliusema vibaya huo mpango wa ujenzi wa reli yenye kasi, walijikuta wakipanda nao kutokana na mwaliko maalum waliyopatiwa kwenye safari hiyo.
ENDELEA NAYO SASA..
**
Upande wa dereva majira hayo yupo makini akitazama mbele huku kaka kwenye kiti. Mikono yake ipo kwenye mitambo ya kuongozea chombo hicho, alitawaliwa na sehemu yenye vitufe vingi pamoja na dashibodi yenye kuonesha mwendokasi wa chombo hiko. Pembeni kulikuwa na simu ya mawimbi ya mezani, ambayo hutumiwa kuwasiliana na vituo vya treni kama wakiwa karibu kufikia. Loh! Mtaalamu huyu hakujua kama safari hiyo ingeweza kuingia doa ndani ya siku hiyo, kwake ni furaha kwa kupewa ajira mpya kupitia taaluma yake.
Akiwa anakaribia Ruvu ndipo mambo yalipobumburuka juu ya safari hiyo, simu yake ye mezani iliyopo mbele yake ilianza kukoroma muda ambao anapiga honi kukaribia kituo cha ruvu. Ilitajwa namba ya chombo hiko, alisikia vyema na kukubali ndiyo ni chenyewe pasipo kujua huyo anayewasiliana naye ni nani.
"Landforce TZ, sikilizeni kwa umakini. Mwendo huohuo unaoutumia hutakiwi kuupunguza wala kuuongeza zaidi. Utembee namna hiyo ndiyo itakuwa usalama wako", Sauti hiyo ilipotoka sehemu ya kioo maalum chenye kuonesha ramani ya reli ilivyo, kulibadilika na kuwa chekundu kisha kikaweka saa ya kidigitali yenye kupungua dakika. Sauti iliendelea kusema, "treni yote hivi sasa na kila behewa mfumo wake wa elektroniki umeunganishwa kwa bomu zito. Ukipunguza mwendo linalipuka, ukiongeza pia linalipuka, kioo chochote kile kikifunguka ikaingia hewa ya nje jua hatopona mtu pia, lina masaa arobaini na nane toka hivi sasa hadi kufikia kulipuka kwake. Tunamuhitaji mheshimiwa Rais hivi sasa aje kwenye kichwa huko tuweze kuongea naye"
Maneno hayo yalimfanya dereva pamoja na wasaidizi wake waanza kutetemeka, wanausalama waliyopo chumba hicho waliposikia hilo walitoka kwa haraka hadi kwenye behewa ambalo viongozi wapo. Mmoja alimuuma sikio DG wake, ambaye alimchukua Rais Zuber na kufika hadi kwenye chumba cha dereva na kuikuta hali halisi inayoendea. Kiongozi mkuu wa nchi mwenye aliingiwa na uoga, alipobaini kuna bomu zito ambalo limeunganishwa na mengine madogo yaliyopo kila behewa na yana uwezo wa kuangamiza kila mtu aliyepo humu ndani.
"Unaongea na Rais Zuber hivi sasa, nimefika kuitikia wito wenu. Nyinyi ni wakina nani na mna shida gani hadi kufikia kufanya haya, hamuoni kama mtapoteza maelfu ya watanzania wasiyo na hatia. Sema mnataka nini nyinyi", Rais Zuber alisema.
"Mheshimiwa nadhani ulipocheza na moto ukasahau wenye jukumu la kufanya hivyo ni maji tu ila si wewe, tuna masharti machache ndiyo kila mmoja ataweza kusalimika. Najua kikosi cha uteguaji mabomu chote tumekiteka na kipo mafichoni mwetu, hivyo hakuna wa kuwasaidia unachopaswa ni kutusikiliza kwa umakini. Ndiyo utakuwa usalama wenu, tunza ahadi na sisi tukutunzie uhai wako na hata watanzania wote kwa ujumla", Aliambiwa.
"Ndiyo nawasikiliza"
"Shati la kwanza, mzigo wote wa almasi uliyoukamata unatakiwa upandishwe kwenye ndege binafasi itakayokuja Airport muda si mrefu, yote unatakiwa kuyafanya kabla ya muda wa bomu kulipuka uliyowekwa. Ukichelewa utakuwa umejipa hasara mwenyewe na kuweka tukio la kihistoria nchini kwako. La pili Lile gereza kubwa kabisa nchi hii mmemshikilia kaka yangu mule ndani, ndani ya muda huo anatakiwa aachiwe huru haraka iwezekanavyo apewe helikopta yenye rubani tu pekee aondoke gereza la nyumba ya giza haraka sana. Vilevile dhahabu zote zitakazotolea mgodi wa Geita zitiwe kwenye ndege binafsi itakayofika kule kama ukiwa tayari kutumiza hilo. Nakwachia saa 48 kutimiza hilo la si hivyo utakuwa umepata hasara na nchi nzima iwe na hasara"
"Hilo la tatu unajua wazi ni gumu mno kutimia, hivi sasa Mgodi ule haupo chini ya serikali upo mikononi mwa wawekezaji ambao ninapambana nao kila kukicha nirurejeshe mikononi mwa serikali. Tawala zilizopita zimeniachia magumu ambayo ninapambana
nayo, ila hilo moja halijafikia tamati"
"Ukiwa kama rais tumia nguvu yako ya dola kufanikisha hilo, tunakupa muda wa kujadiliana na wenzako kuweza kukamilisha hilo", Sauti hiyo ilipofikia tamati kuliambatana na kukatika kwa mawasiliano baina yao ndani humo na kwa maadui zao waliyofanyia mchezo mchafu. Rais Zuber alijikuta akiingia na ubaridi moyoni mwake, alihitajika kufanya mambo ambayo yapo kwenye nje ya uwezo wake hadi kufikia muda huo.
"Waitwe CDF na Mnadhimu mkuu humu ndani, CGP na IGP wote nawahitaji mahali hapa. Hawa ndiyo wawe wa kwanza kupewa taarifa hiii kabla ya kufikia wengine, hali ni mbaya sana inabidi tujadiliane nao upesi sana ili tujue ni namna tunaweza kutoa maamuzi. Kuitoa habari hii kwa umma mapema hii nadhani itakuwa ni mbaya sana. Dereva hakikisha stesheni zote za treni hazijui hili lililotokea humu ndani, waambie tu wahakikishe raia hawachezi jirani na reli hii spidi si mchezo. Jamani na kila mwenye simu mahala hapa, akabidhi kwa maofisa hawa asije kuvujisha habari hii.", Rais
Zuber alitoa maagizo huku akiketi kwenye kiti kimojawapo, mwili ulimtetemeka haswa alipofikiria anasafiri na bomu la hatari.
Dakika mbili baadaye wakubwa wote wa majeshi ya ulinzi na usalama walifika kwenye chumba hicho cha dereva, waliambiwa kila kitu juu ya kilichojiri humo. Taarifa huyo ilileta mshtuko kidogo kwao ila walirejewa na hali ya kawaida, kwakuwa ni wenye mafunzo makubwa ya kijeshi. Kila njia ambayo ingesaidia kutorosha watu ndani ya chombo hicho haikuwepo, jambo ambalo ni gumu mno kuokoka. Maelezo hayo yalifanya kila mmoja akune kichwa ili aweze kutoa ushauri kwa Rais, waweze kuokoka humo ndani.
"Nadhani nyote mnatambua humu ndani kuna watu muhimu mno kwenye jeshi letu kuna maelfu ya wananchi, wa kwanza kuitwa ni nyinyi kwakuwa mna mioyo thabiti iliyojengwa na mafunzo imara ya kijeshi. Siwezi kuita mawaziri au wabunge mahala hapa wawe wa kwanza kupewa taarifa hii, wale ni wanasiasa tu hawana jingine lolote lile. Kuwashirikisha kabla yenu nyinyi ni kufanya kosa kubwa, habari hizi zitavuja. Mkumbuke wengine ni wapinzani wangu kisiasa. Sasa basi niambieni tuchukueni hatua gani juu ya hili", Rais aliwaambia.
"Mheshimiwa masharti yote yanawezekanika hapo isipokuwa hilo la kumwachia Ralond aliyepo nyumba ya giza, tukumbuke hilo ni suala gumu mno kutimia waliyomuweka kule ni EASA na sheria iliyopelekea kuundwa kwao imeeleza wazi wale ni ogani inayojitegemea na rais yeyote nchi ya afrika ya mashariki hana mamlaka nao", Mkuu wa jeshi la magereza nchini CG Mwambe alieleza.
"Asemacho Mwambe ni kweli kabisa, wakati tukiangalia mustakabali wa masharti mengine hebu kwanza tuwasiliane na EASA hivi sasa. Wao wawe ni watu wanaofuatia kutambua kuhusu hili baada ya sisi. Wakae huko wajue wamefikia uamuzi gani kuweza kutimiza hili", Jenerali Marwa alisema.
"Mheshimiwa hata mimi ninaungana na CG Mwambe pamoja na Afande Marwa juu ya hili. Tuanze kwanza kuongea na AE wa EASA juu ya hili", IGP Mbwambo alisema.
"Ni vyema huo ni uamuzi stahiki hata mimi nauunga mkono, mujadiliane na hao watu kwanza huku General unahakikisha makao mkuu wanajua kuhusu hili. Taarifa hii iwahusishe wanausalama pekee na maafisa wakubwa wa kijeshi kwanza, Ngome wapate taarifa juu ya hili", DG Moses Gawaza alitoa wazo
"Ok sasa na mimi ninaenda sawa na mawazo yenu, DG Gawaza hakikisha unawasiliana na AE wa EASA. CDF ni wajibu wako kuhakikisha kamandi zilizobaki zinajua nini cha kufanya, toa taarifa kwa aliyepo Ngome muda huu nadhani ni muda mwafaka wa maamuzi. Tuhakikishe tunapata ya busara yenye tija kwenu, bila kuingiwa na hasara yeyote ile", Rais Zuber alihitimisha.
*
Hatimaye simu ya upepo iliyopo ofisini kwa Brigadia Mkunga ilivuma na kutoa mkoromo kisha ikasikika sauti ya Luteni Jenerali Belinda. Ilijitambulisha na kutaja eneo alipo kisha akataja jina la mtu anayeongea naye, alifanya hivyo huku akiuliza kama anasikiwa.
"Nakusikia ni Mkunga hapa afande"
"Landforce TZ yote hivi sasa imetegwa elektroniki bombs, hatutakiwi kuongeza wala kupunguza mwendo pia hatuhitajiki kufungua hata kioo wala mlango. Tukifanya hivyo hakuna hata mmoja atakayesalia, umenielewa! Ongea na Kamandi ya ngerengere tunahitaji msaada"
"Afande!", Brigadia Mkunga aliitikia kisha akakata mawasiliano na kunyanyua mkonga wa simu ya mezani akijiandaa kubonyeza namba atimize agizo alilopewa.
Loh! Alipotaka kufanya hivyo mlango wa ofisi ulifunguliwa ghafla, waliingia maofisa wawili kila mmoja akiwa na silaha mkononi mwake. Wote walielekeza kwake wakiwa na nyuso ambazo hazina mzaha hata kidogo, Brigadia Mkunga hata yeye mwenye alishangaa juu ya jambo hilo. Hakutaraji kama kungeweza kutokea kitu kama hicho, maafisa wawili mmoja akiwa na cheo sawa na yeye mwingine ni mdogo kwake
"Seba! Gabi! Nini mnafanya hiki, kwanini mnielekezee silaha?", Brigadia Mkunga aliuliza kwa mshangao kwa kutoegemea jambo kama hilo
"Kama unajitaka basi usitoe taarifa Ngerengere juu ya hilo, hii ni amri kwako wewe senior", Kanali Seba alisema.
"Siwezi kuamini nyinyi ndiyo wasaliti wa nchi hii, mnahusika pia na tukio hili"
"Hukukosea tunahusika ndiyo na tukio hili, lakini jiulize hivi sasa umejua utafanya nini wewe. Ninachokwambia hivi sasa ni kutoa taarifa ka Navy wapeleke meli sasa hivi kisiwa cha Mafia. Wanajeshi wote wanaofanya doria mpaka wa baharini wa nchi hii waondoke mara moja, ukifanya hivyo ndiyo itakuwa pona yako. Uzalendo mwachie baba wa taifa, kizazi hiki ni pesa tu tuone wewe na huyo Rais wenu uzalendo utawasaidia nini?", Brigaia Gabi alisema huku akiondoa usalama wa silaha yake ambayo ina kiwambo cha kuzuia sauti.
"Ok sasa sikieni, sijawahi kutishwa na bastola inapaswa mjiulize nyinyi mtatoka vipi hapa ilihali
huko chumba cha kuongozea kamera wanawaona mnachokifanya. Sipo tayari kutii maagizo hata mnitoe moyo wangu nikiwa mzima, kwa ajili ya nchi yangu napiga simu na kutoa maagizo ambayo Afande Belinda kanituma si kufuata matakwa yenu nyinyi wasaliti wa nchi hii", Brigadia Mkunga alisema huku akibonyeza vitufe vya simu ya mezani.
"Nasikitika kukwambia chumba cha kamera kuna mizoga mitupu tu, hivi sasa hakuna anayetuona hiki tunachokifanya isipokuwa wewe. Tumezima kamera za jengo zima hili", Kanali Seba alisema kwa kujiamini.
"Yupo anayewaona ni mimi tu", Sauti ilisikika kutoka nyuma yao, kina Kanali Seba walipogeuka tu kila mmoja alipigwa risasi ya kiganja cha mkono silaha ikamwanguka, walikutana na kasiba mbili za bastola zenye kiwambo cha kuzuia sauti kila moja ikimwelekea mhusika.
"Ooooh! No Norbert Kaila tena", Brigadia Gabi alisema.
"Wakati wenu wa kufanya uhaini ndani ya nchi hii ushaisha hivi sasa, nyinyi ndiyo mnahusika na utekwaji nyara wa kikosi cha kutegua mabomu ili mkafanye ujinga ambao mmeufanya leo hii. Wasaliti wakubwa nyinyi hatopona mtu leo hii", Norbert alisema akiwa hana mzaha, uso wake ule wenye tabasamu ulimwondoka,
"No Kaila usiwaue hawa wahusika nataka wafikishwe kwenye vyombo vya sheria wapewe adhabu", Brigadia Mkunga alisema.
"Haitokuwa na maana hawa kuhukumiwa, hata wakipewa hukumu ya kifo bado mwenye mamlaka ya kutia saini hukumu ya kifo ni Mheshimiwa Rais. Amekuwa hafanyi hivyo siku hizi, huoni hawa wataenda kula dona la bure kwenye gereza wakisubiri hukumu isiyotimizwa. Lazima wafe hawa Afande Mkunga, wameshanijua mimi ni jasusi pia", Kaila alisema.
"Kaila hapana"
"Mkunga nimekwambia piga simu kutoa taarifa kamandi ya anga juu ya suala hili, pia taarifa ifike kwa Belinda juu ya wasaliti wa jeshi. Hawastahiki kubaki wazima kabisa hawa ni hatari wanajua siri nyingi na pia ni wasaliti, unafikiri wakiwa huko gerezani wanashindwaje kuvujisha taarifa ilihali hawatoenda nyumba ya giza maana hukumu yao itakuwa ni kifo tu kwa maafa waliyosababisha. Kumbuka gereza lile ndiyo pekee mtu hawezi kutoa siri lakini haya yaliyobaki jueni kila kitu kitavuja na itakuwa hatari kwa nchi yetu", Kaila alipotoa maelezo hayo bila ya kukawia alimpiga risasi ya kichwani Kanali Seba akafa papo hapo, alielekeza bastola mbili kwa pamoja kwa Brigadia Gabi
"Brigadia Mkunga hapa naongea, hakikisha kamandi ya anga wanatoa msaada Landforce TZ aliyopo mheshimiwa ina bomu. Hii ni amri kutoka kwa
Three star general", Afande mzalendo alisema, kisha akashusha mkonga wa simu chini halafua akamtazama Kaila. Kuiona sura ya kijana huyo aliyemkomboa kulimfanya hata aendelee kuwa jasiri na kutoa taarifa kwa Belinda juu ya kitu kinachoendelea huko na pia kumweleza juu ya wasaliti na namna Kail alivyoweza kumwangamiza mmoja.
"Afande Belinda kakupa go ahead, fanya kazi yako Kaila", Amri hiyo ilimfanya Norbert amwangamize Gabi palepale.
"Hawa watu huwezi hata kuwahoji Mkunga, hawapo tayari kufumbua mdomo wao, zawadi yao ni kifo tu na si kingine", Norbert alisema huku akichomeka silaha zake kiunoni halafu akaendelea, "anyway tuachane na hayo, kilichonileta mahali hapa ni kujua katika ushughulikaji wa kuweka mabehewa kwenye reli na pia kushusha kichwa na kuunganisha mfumo mzima wa umeme. Kazi hii aliifanya nani?"
"Ameifanya injinia wa Kiborongo investment anayeitwa Benjamini Mluva"
"Oooh! No! No! Mkunga huyo mtu anatakiwa apatikane upesi, kazi ile ya kuunga bomu la namna ile anaweza kuifanya injinia wa umeme tu na si mwingine. Kama yeye ndiyo kaja kuhakikisha umeme upo sawa kwenye treni yetu, basi jua huyo ndiyo mhusika mkuu. Benjamin ni wa kukamatwa mara moja na kuwekwa chini ya ulinzi. Huyu ndiye atasaidia serikali isifuate matakwa ya wenzake, kama ni yeye ndiye aliyeunda lile bomu basi ndiyo atajua namna ya kulitegua ni mtu muhimu sana yule"
"Kaila kumbuka mimi nipo uande wa mipaka ya nchi na ninahitajika mahali hapa pia kwa ajili ya kuwasiliana na wengine wote. Kiufupi mimi ndiye mtoa amri kwa sasa hivi ofisini. Hiyo kazi naiacha chini yako hivi sasa, wewe nishajua ni mwanausalama ingawa bado sijamaizi upo chini ya kina nani kuweza kutenda yote haya"
"Mimi ni EASA napenda utambue hilo, hivi sasa kwa maelezo niliyoyapata kutoka kwa wakuu, hawapo tayari kumwachia yule mhalifu. Ndiyo maana nimeamua kufanya haya, watu hawa waliyotega bomu tusije tukawaamini cha kufanya ni sisi tutegue bomu hilo hakuna namna nyingine. Benjamini nitamsaka mwenyewe"
"Ok nikutakie kila la heri kwenye mpango wako, tutawasiliana zaidi"
Kaila na Mkunga waliagana hapo, watu wenye kuipigania nchi yao kila mmoja alichukua njia yake ili kutimiza majukumu ambayo yalipaswa yatekelezwe kwa haraka ili kuweza kunusuru maelfu ya wa tu waliyopo kwenye treni ya kisasa.
Kufikia majira hayo hakuna mtu aliyeweza kufahamu hilo mbali na wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama pamoja na wanausalama wachache. Kutoa taarifa kwa ghafla ingeweza kupoteza maisha ya ndugu wengi waliyopo uraiani ambao jamaa zao walikuwa ndani ya chombo kile cha mwendokasi.
**
"Mheshimiwa AE wa EASA amegoma kutimiza sharti hilo, kasema kuamua hivyo ni sawa na kuachia hatari kwa dunia hii. Gera ni mtu hatari sana, yeye na jopo lake wameweka msimamo huo. Wapo tayari kutusaidia kuweza kulitegua hilo bomu ila si kumwachia Gera", DG Moses alisema.
"Oooh! God hivi anafikiri ni rahisi kuishi na bomu lililotegwa saa 48 huyu hajui ni namna gani ninavyotaabika. Haya huo msaada watatupa upi mkumbuke wale watu wanasubiria majibu yetu, hebu tusiangalie maisha yetu mkumbuke sisi ndiyo wenye dhamana ya maisha ya maelfu ya watanzania waliyopo humu ndani itakuwaje kama wakijua kuna jambo kama hili limetokea. Inabidi izimwe hii ishu haraka iwezekanavyo kabla haijajulikana, yaani hata hawa wabunge wenye kupenda kuonekana kwenye ishu kama hizi ingawa tukitoka hapa wanatupinga, wasijue", Rais Zuber alisema.
"Mheshimiwa tuachie hili suala kwenye mikono yetu tulifanyie kazi, nakwomba rejea kwenye behewa la viongozi. Tarajia makubwa kutoka kwetu", Belinda alisema.
"Mheshimiwa tafadhali msikilize Belinda, tuachie hili suala lipo kwetu hivi sasa. Mimi, CGP, IGP na DG tutashughulika. Nakuomba uwe na kifua cha kutunza siri na pia uwe na subira, tupo kwa ajili ya roho za maelfu ya watanzania waliyopo humu ambao ni jukumu letu kuhakikisha hawadhuriki", Jenerali Marwa alisema, Rais Zuber hakuwa na hiyana alitoka mwenyewe nje ya chumba hicho cha dereva wa treni. Alirejea kule walipo viongozi wengine wa kisiasa na kiserikali, alikaa kama vile hakuwa akijua kinachoendelea humo na hata alivaa tabasamu la bandia usoni mwake.
ITAENDELEA
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment