SEPTEMBER 1 SEHEMU YA KUMI NA TANO.
:max_bytes(150000):strip_icc()/iStock-637126086-5978d78f0d327a0011b429d4.jpg)
Mheshimiwa tafadhali msikilize Belinda, tuachie hili suala lipo kwetu hivi sasa. Mimi, CGP, IGP na DG tutashughulika. Nakuomba uwe na kifua cha kutunza siri na pia uwe na subira, tupo kwa ajili ya roho za maelfu ya watanzania waliyopo humu ambao ni jukumu letu kuhakikisha hawadhuriki", Jenerali Marwa alisema, Rais Zuber hakuwa na hiyana alitoka mwenyewe nje ya chumba hicho cha dereva wa treni. Alirejea kule walipo viongozi wengine wa kisiasa na kiserikali, alikaa kama vile hakuwa akijua kinachoendelea humo na hata alivaa tabasamu la bandia usoni mwake.
ENDELEA NAYO.
**
Mzee wa kazi aliamua kuifanya dhima kinamna yake, kutokana na muda wa masaa 48 waliyopewa ikimaanisha Septemba tatu ndiyo mwisho wa kuishi kila mmoja aliyepo ndani ya chombo kile. Aliamua kuingia kwenye msako wake, Besi alihitajika kupatikana kwa gharama zozote zile. Akiwa kwenye mwendo wa kasi alifika nyumbani kwa mshukiwa wake, ulinzi ulikuwa mkali mno kukiwa na walinzi wenye sare sawa na wale waliyomshambulia kule darajani.
Norbert akiwa na silaha zake kiunoni, aliegesha gari kwenye miti mingi kisha akashuka akiwa amevaa glovu nyeusi mkononi. Mbali na bastola mbili, alichukua visu vinne vikali na aliweka kiunoni vyote vikiwa kwenye ala zake. Uso wake haukuwa na mzaha kila alipofikiria ni roho za watu waliyopo kwenye treni ile.
Uzio wa nyumba ya Besi aliuruka kwa sarakasi moja na alipotua ndani alibimbrika chinii. Kitendo cha yeye kuingia walinzi wawili waliyopo jirani na uzio walimwona, ila aliwahi kuwamaliza kwa kumpiga mmoja karate mbili za haraka. Ya kwanza ikipangua silaha na nyingne ikimpiga shingoni akapoteza fahamu. Aliyesalia alipojaribu kuinua silaha kwa hima, alikutana na pigo la judo ambalo lilimpeleka chini huku akiwa amepigwa kabali ya miguu. Alibanwa hivyo hadi alipotulia ndipo akaachiwa, Kaila alijilaza vilevile pamoja na kuwamaliza huku akitalii mazingira ya hapo ndani.
Upande wa getini aliona walinzi wawili wakiwa hawajui kinachoendelea, upande mwingine kuelekea nyuma ya nyumba aliona ni kweupe hakuna kiumbe yeyote. Bila kuchelewa alitoa bastola zake mbili kiunoni. Aliwalenga kichwani kila mmoja, kutokuwa mlio kulimpa wasaa wa kutenda jambo la upesi bila kugundulika. Aliwalamba risasi za kichwani kila mmoja, tendo hilo alipolifanya alichukua bunduki moja ya walinzi wale kisha akapiga sarakasi upesi na alipotua alimbimbrika hadi akafikia kwenye ukuta wa nyumba akajibanza. Tukio alijua wazi kungejitokeza walinzi wenye kutazama eneo la langoni kama wapo
Kweli kulisikika vishindo vikija hapo, Norbert alijiandaa vyema kwa kuweka bastola zake kiunoni kisha akachukua bunduki ya kivita aliyoitwaa humo ndani. Walindaji waliyotoka huko nyuma walifika wakiwa hawana mahesabu yeyote, kitendo cha wao kujitokeza aliamua kuchungulia tu akawamiminia risasi. Wanne kati yao wakaanguka papo hapo, wawili wakasalia wakawa wakimimina risasi upande aliyopo. Norbert alirudi nyuma kwa kasi, hadi usawa ambao kuna bomba la kutolea harufu chooni usawa wa madirisha mdogo ya choo. Bila kukawia aliruka juu akashika kingoa za madirisha madogo, alijivuta juu kwa haraka akafika batini ambapo alitulia kimya kama vile hayupo.
Loh! Magadi wale walikosea hesabu haswa, walikuja upande uleule kichwa kichwa huku wakimimina risasi wakidhani watampata mtu wao. Hadi walipofika sehemu ile hakumkuta, wakiwa wanashangaa ndipo mwenzao akawamaliza kwa pamoja akiwa amejishikiza kwenye paa la nyumba hiyo.
Norbert alipoteketeza sehemu kubwa ya walindaji, alishuka huko juu alipokuwa huku silaha aliyoichukua humo ikiwa ipo tayari kwa lolote. Alitembea hadi mlango wa mbele wa jengo hilo, huo alijaribu kuufungua ila haukutii amri. Hii ni ishara tosha ya kuwa humo ndani hakuna kiumbe wa aina yeyote ile au yupo hajatoka nje. Aliamua kuufungua kwa funguo malaya, akaingia ndani ambapo alitokea kwenye sebule ya kisasa kulipokuwa kuna picha za Besi zikiwa ukutani.
Upendezaji wa kikaribisha wageni kwake haikuwa na maana, zaidi ya kupekua ndani humo kumtafuta mhusika lakini hakukuwa na mtu. Pia hakuona cha maana kilichopo ambacho kingeweza kumsaidia walau kumpata mhusika wake.
Aliamua kutoka nje hadi alipo mlinzi yule ambaye alimzimisha tu, alimfikia na kumtoa kila kitu cha hatari mwilini mwake kisha akamburuza hadi eneo ambalo kuna bomba la maji linalotumika kumwagilia maua yaliyopo bustanini humo ndani. Norbert alimwinamisha kwenye koki ya maji, alifungua na kumlowanisha kichwa chake hadi pale alipozinduka na kuanza kuleta kukurukakara zake. Kufikia hapo alimwondoa bombani kwa nguvu kisha akamsukuma kwenye majani, mlinzi yule aliangukia chali na alipoinua uso kumtazama aliyemfanyia hivyo alikutana na mdomo wa bunduki.
"Mwenye nyumba yupo wapi?", Aliulizwa swali na kisha risasi takribani tatu zikapigwa jirani na miguu, haikumpata hata moja ila uoga aliyokuwa nao alishtuka haswa na kuanza kusota kurudi nyuma.
"Siulizi swali mara mbili, unanipotezea muda", Alipotoa kauli hiyo alimtandika risasi moja ya gotini na kupelekea damu zianze kumvuja, mlinzi yule aliona hakuna ulazima wa kuficha tena kwa jinsi alivyojeruhiwa na pia adui yake bado ana silaha. Alibaki kimya huku akiendelea kujitazama nguo yake ya ndani baada ya kuvuliwa koti la juu, hapo ndipo alijiona hana ujanja na amefika pabaya.
"Inaonekana nyinyi ni zaidi ya walinzi ndiyo maana hadi kola zenu zinawekwa sumu mlambe mkizidiwa. Si kampuni ya ulinzi ya kawaida, nyinyi. Sikia wewe usinipotezee muda hapa kama ni hiyo nguo tayari nimekuvua huna namna ya kulamba sumu ufe", Kaila aliongea huku akimlenga na mdomo wa mdomo wa bunduki kwenye goti jingine.
"Mkuu Besi hayupo hapa, anaondoka usiku wa leo kuelekea Komoro. Hapa kahama na kila kitu chake"
"Swali nililokuuliza ni yupo wapi, sijakuuliza anaenda wapi"
"Sijui hivi sasa alipo, naomba usiniue ninahitajika na familia yangu"
"Ili ukatoe taarifa kuwa umevamiwa wazidi kujificha nisiwafikie siyo, umechelewa", Norbert a;liposema maneno hayo alimmiminia risasi za kifuani na kumpiga moja ya kichwani.
Alipotimiza hayo aliamua kwenda hadi kwenye kibanda cha ulinzi kwenye nyumba hiyo, hakukubali kuwa amewakosa hivihivi wabaya wa nchi wakiwa wameweka masharti magumu kutimizika. Huko alikutana na kitabu cha wageni, pia kukiwa na simu ya mezani pamoja na kitabu kingine chenye namba za simu. Hapo alijikuta akiachia tabasamu, kwa kuona amepata namna ya kuanzia, kuwepo kwa kitu kama hicho kwake ni ushindi tosha ambao alihitaji kutafuta namna ya kuupata tu na si vinginevyo.
Mawasiliano ya 'fax' hatimaye yalitumika, yalitoka kwenye treni hadi ofisi ya mkuu wa gereza la nyumba ya giza. Taarifa ya kile kilichowakuta wakuu wa nchi pamoja na wa kijeshi, zilifika kwa Kamishna Nkongo. Karatasi yenye kutoa maelezo hayo aliipata kupitia mashine hiyo, aliyasoma na kuelewa sehemu ya masharti yaliyopo ili watu wote waweze kukombolewa kwa haraka.
Hayo ndiyo mambo magumu kwake, yaani kumwachia mtu hatari kama yule pamoja na kupatiwa chombo cha kutorokea kama ikiidhinishwa juu ya jmbo hilo. Kwake ni mtihani haswa, akifikiria jinsi alivyomfungia kiumbe hatari mule ndani. Hali ilivyo aliona ingekuwa ni mbaya zaidi kama angeendelea kumuweka kwenye chumba chenye mateso. Aliamuru atolewe na kurejeshwa magereza ya kawaida, huku akitafakari itakuwaje kama ingetolewa amri kama hiyo huko EASA.
Ofisini muda huo alikuwepo mkewe wake ambaye pia ni askari, tena akiwa mmoja wa wasaidizi mahala hapo.
Habari hiyo naye aliisikia akaone ugumu wake, kama ingeweza kutimizwa kwa kufuata matakwa ya magaidi.
"Unajua huyu mtu ni gaidi kabisa fikiria tukimwacha awe huru nini itakuwa kwa nchi hii. Tukumbuke hakukuwahi kuwa na makubaliano yenye usawa kati ya serikali na magaidi, maadui hawakubaliani lazima kutakuwa na usaliti", Mkewe alisema.
"Hilo suala nalielewa Teddy lakini fikiri kwa umakini itakuwaje sasa, wakuu ndiyo waamuzi wake yaani hapa huyu mjinga nitamani hata nimwangamize unajua baba yupo kwenye treni ile ni hatari hii. Hii fax katuma yeye hivi sasa", CP Nkongo alisema.
"Hebu tuwe na subira na suala hili tulifikisha kwa wenzetu wote, huyu gaidi hastahiki hata kuwepo humu. Hukumu yake ni kifo tu na si kingine"
"Nahitaji tukae kikao cha dharura na wengine mahala hapa"
**
Baada ya kufanikiwa kutuma pesa kwenye akanti ya baba yake, alisahau kumkumbusha juu ya msaada aliyowapatia. Ndipo akiwa na wenzake kwenye maficho yao aliamua kupiga simu na kumpa taarifa ya kumtuma pesa. Besi hapo ndipo akajikuta akipokea habari mbaya, mzazi wake naye yupo ndani ya treni ileile ambayo kaweka bomu kwa ajili ya kulipua maelfu ya raia wa nchi ya Tanzania wakiwemo viongozi wa nchi na hata wakuu wa majeshi.
Loh! Kumfanyia mtu ubaya ni kitu chepesi sana ila ukikurudia wewe ni jambo jingine zito sana kukabilika. Besi alijikuta akijiwa na uchungu moyoni mwake, anaenda kumwangamiza mzazi wake aliyemlea kwa muda mrefu kisa tu tamaa zake za muda mfupi. Kama ni kutafuta pesa ila si kukaribia kutoa uhai wa wengine, alijikuta akieleza hilo kwa Watson ambaye alimshangaa sana akiona anaweza kuwasaliti ndani ya muda wowote ule.
Alidhani mzee huyo ndiye ambaye angeweza kumsaidia kwa jinsi alivyompigania hadi akawa hapo. Kumbe anampa habari mtu mwenye roho ya paka, ambaye aliamua kumpa pole kinafiki na kuahidi kumsaidia tu huku kichwani akiwa na lake. Alipofanikiwa kumweleza hilo simu iliingia kupewa taarifa ambayo ilifanya wengi washangilie mahala hapo. Eti Norbert Kaila ameshikwa nyumbani kwa Besi, baada ya kupigwa kitako cha bunduki akapoteza fahamu.
"Habari njema hii jamani, aliingia kikondoo tu akakutana na wazee wa kazi. Nasikia aliruka ukuta ile katua ndiyo jamaa akamuwahi na kitako cha bunduki. Sasa huyu nataka akauawe mara moja", Huze alisema kwa furaha.
"Besi kwakuwa wewe hapa hauna kazi nyingine, basi hili jukumu nakwachia wewe, nenda kamhoji huyo mjinga kama ana chochote cha kusema utuletee tumia mbinu za kijasusi kumbana asema. Akisema mmalize, asiposema asipone vilevile", Watson alisema, huku akimgeukia Huze akamuuliza, "kuna habari yeyote ile kutoka kwa kina Kanali na Brigadia?"
"Hadi sasa sijawapata na simu zao hazipo hewani, nahisi ndiyo wapo kazini kumbukeni walisema wakiingia shughulini hawatoshika simu", Huze alijibu, muda huo tayari Besi alishatoka kwenda alipoambiwa akiwaacha wenyewe humo ndani
"Hivi Watson kwanini hii kazi kwa haraka umempa Besi, kama itatokea tatizo lolote hapa la kimitambo nani wa kuja kulitatua. Nimekaa kimya tu sikupinga, lakini nadhani kuna jingine umeliwaza", Alpha alisema.
"He is stupid, anaendeshwa na emotion kuliko akili. Kwenye treni yupo baba yake mule kajua hilo, eti ananiambia nimsaidie aokoke. Maana yake tusilipue bomu kisa kuna mzazi wake, unafikiri ana umuhimu gani huyu. Huze toa taarifa kwa walinzi akifika huko wammalize yeye na Kaila hakuna namna, nimempeleka huko ili wakamuue tu", Watson alisema.
"Wooow! Umecheza kama pele Watson, angeweza kuwa kikwazo kwetu huyu tena ningemwachia aweke password yeye angeweza hata kuirukia system ya bomu kwa kutumia PC nyingine atufelishe", Huze alisema huku akiinua mkonga wa simu akabonyeza namba kadhaa kisha akaweka sikioni, alisubiri simu ilipoita hadi ikapokelewa. Aliongea, "Guard sikilizeni kwa umakini Besi anakuja yupo njiani tumempa kazi moja tu ya kumwangamiza Kaila, ila haikuwa lengo hilo bali tumemleta huko mumwangamize. Hakikisheni Kaila na Besi wote kwa pamoja wanaangamia hii amri"
"Watson wewe una akili sana, huyu mjinga umemuweza haswa kwa kitu hicho ulichokifanya", Alpha alisema.
"Huyu ni magugu hivi sasa, mwache akakutane na mafuta ya taa huko, afe bila hata ya kuwashiwa kibiriti", Watson alijitapa.
**
Besi akiwa yupo ndani ya gari lake aliendesha ka kasi kubwa, akiwa hana lengo la kummaliza Kaila isipokuwa ni kuweka mkakati mwingine. Tayari alishafanya kitu ambacho ni pigo kwa akina Huze, wao hawakujua waliona ni wanaenda kumaliza mchezo. Alifanikiwa kufika hadi nyumbani kwake, akafunguliwa geti akaingiza gari ambapo alisimamia eneo la jirani na kibanda cha mlinzi. Alishuka huku geti likijifunga lenye kwa mtambo maalum, alipiga hatua zake ndefu akielekea upande wa mlango wa banda hilo, huko alikutana na ukimya ambao siyo wa kawaida.
Ilimbidi afungue na alipofanya hivyo, alikutana uso kwa uso na mdomo wa bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti. Hakutarajia suala hilo, akataka kufanya ujanja, alijikuta akitulia baada ya mkono wa pili kuongezwa ukiwa na silaha vilevile. Mwenyewe aliweka mikono juu huku akirudi nyuma na Kaila akaonekana akitoka kwenye kibanda cha ulinzi.
"Umekuja kumuua Kaila siyo, hongera sana kwa mtego wangu umejileta mwenyewe mahala hapa", Norbert alisema.
"No! No! Kaila sipo kwa lengo hilo, baba yangu yupo kwenye treni Kaila. Wale wajinga wamejua hilo ndiyo maana wakaniagiza haya ili walinzi wa huku waje kuniua. Nimesikia mipango yote baada ya kutoka ndani ya control room, nikabana mlangoni. Sipo kwa lanego hilo, nahitaji mzazi wangu aokoke", Besi alisema.
"Kama isingekuwa mzazi wako kuwa kule ungefanyaje? Yaani upo radhi kabisa kupoteza maisha ya watanzania wengine kisa uwepo kwenye maisha mazuri"
"Kaila ondoa silaha usoni kwa Benjamin, huyo si adui yetu kwa sasa ameweza kuwa msaada kwetu", Sauti nyingine ilisikika na hatimaye akajitokeza mtu aliyevaa gwanda la kijeshi ambalo limeweka weusi kwa uchafu.
"Luteni Mfuruki ni wewe kweli?", Norbert aliuliza akiwa haamini.
"Ndiyo mimi, huyu bwana baada ya kujua kama yupo upande mbaya wenye kutaka kutoa uhai wake. Aliamua moja kwa moja kuja hadi tulipofungiwa baada ya kutekwa, hivi ninavyoongea ameikomboa bomb squad yote na amekuja nayo kwenye gari alilofika nalo. Anatakiwa atusaide hivi sasa", Luteni Mfuruki alisema, Kail alishusha silaha chini kisha akamtazama Besi.
"Benjamin umefanya kosa kubwa pia ingawa umeweza kuwakomboa maafisa hawa wote, wakijua kama umeondoka nao basi jua watahamisha kambi haraka iwezekanavyo. Maana unajua walipo na walituma kukuua, mpango wao umefeli kuchomeshwa ndiyo kunafuata", Norbert alilalamika.
"Unafikiri ningefanyaje Norbert, hawa wangeuawa wote leo leo. Alpha kafika kwa ajili ya kuondoka na timu yake na kuua wote hawa", Besi alisema.
"Alpha ndiyo nani?"
"Mkufunzi wa zamani wa Cuba kwenye kikosi cha komadnoo, anaitwa Timothy. Yeye ndiyo alifadhili hadi nikaweza kupata ujuzi wote huu niliyonao, ni mtu hatari sana huyo", Besi alieleza, hapo ndipo Norbert akajua mtu ambaye walimwamini na kufanya naye kikao juu ya kutafutwa kina Huze ndiye anayewatuma kufanya kazi hizo. Doh! Waliuza mpango wote kwa adui bila ya kujijua, aliweka mkono usoni huku akijuta kwa maafisa wa shirika lao kufanya yale. Norbert alisema, "Ooh! No! No! No! Huyu mtu tumeshauza sehemu ya siri zetu, kikao cha kuwatafuta hao watu alihusika".
"Jamani hapa cha maana ni kujua jinsi gani tunaweza kuwakomboa waliyopo kule hebu hayo mengine tuache. Msifikiri kuna makubaliano na ambayo yatawekwa, jueni hata masharti yalitolewa yakitimizwa treni inalipuliwa. Yasipitimizwa ni vilevile. Muhimu ni kutegua hilo bomu kuliko kitu kingine, tusiangalie masharti yao. Mimi ndiye niliyetumia miezi kuliunda lile bomu, password ameweka Huze mwenyewe siwezi kulitegua pia. Haliteguliwi kwa nyaya zaidi ya password tu na si kingine, najuta kutumiwa na washenzi wale", Besi alisema.
"Sasa sikilizeni kwa umakini, mimi nimepata wazo hivi saa. Mfuruki na Benjamin nyinyi nendeni kambini mjue mtalitatua namna gani. Mimi ninaelekea makao yangu ya kikazi hivi sasa, mjigawe hakikisheni wengine wanafika kule kwenye makao ya kina Huze tubahatishe kama wapo au lah. Tusidharau kitu, kukiwa na jipya mimi nitajua ni namna gani tunaweza kulitimiza", Kaila alisema huku akitoka kwa haraka, wengine nao walimfuata kwa nyuma huku wakiwa hima kuokoa maisha ya wasiyo na hatia.
ITAENDELEA
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment