SEPTEMBER 1 SEHEMU YA KUMI NA TATU.
:max_bytes(150000):strip_icc()/iStock-637126086-5978d78f0d327a0011b429d4.jpg)
TULIPOISHIA..
Norbert alifika hadi kwenye soko la mitumba la Karume, hapo alinunua kofia nyingine kisha akaondoka kurejea katikati ya jiji mahali ambapo aliliegesha gari lake kabla hajaamua kumvamia Huze. Mpango wake wa kumteka nyara tajiri yule, ulishindikana hapo kwa jinsi alivyovamiwa na walinzi.
ENDELEA NAYO ...
**
Baadaye Huze alirejewa na fahamu alijikuta akiwa yupo kwneye wodi ambayo ina ulinzi mkali, akili yake iliporejea sawasawa ndipo maafisa wa jeshi la polisi walifika mahali hapo na kumuhoji juu ya tukio lile lililomkuta. Kutokana na jinsi ilivyokuwa ilimbidi atumie uongo mwingi kwa kuunda kisa chenyewe hadi anafanikiwa kupoteza fahamu. Walinzi nao waliungana naye kwenye maelezo, walieleza kinamna ambayo walishabihiana na bosi wao na hakuna kitu kilienda kinyume. Askari wakaamini Huze alivamiwa na mhalifu ambaye hamfahamu, wakajaza maelezo hayo kuanza upelelezi wao. Ukosefu wa kamera za usalama barabarani, uliwafanya wasigundue kilichokuwepo pale, pia namna ambavyo tukio lilivyo hakuna raia wa kawaida aliyethubutu kutia macho yake na baadaye aje kuwaeleza maafisa hali halisi.
Majira ya jioni ya siku hiyo, aliruhusiwa na alirejea nyumbani kwake ambapo ulinzi uliimarishwa na walinzi wa kampuni yake baada ya kukataa kuchukua maafisa wa TPF akisema walindaji wao wanaweza kumwokoa. Watson alikuja kumwona akiwa na Kanali pamoja na Brigadia wenye kuhusika nao kwenye usaliti wa nchi.
"Unajua sisi tumesikia maelezo ya upande wa jeshi la polisi tu, ila hatukufanikiwa kujua kuhusu huyo mshenzi, hata walinzi hawakumwona. Uliyemwona ni wewe tu ambaye umepoteza fahamu pekee, sasa tunataka kusikia kutoka kwako Huze. Ni nani huyo mwenye kufanya hayo", Watson alisema.
"Jamani! Jamani mjue kuna mjusi mmoja hatari sana yupo nyuma yetu na keshanusa kila kitu", Huze alisema.
"Mafumbo si mahali pake Huze, weka kila kitu wazi", Brigadia alisema.
"Ok ni hivi, ushenzi wote huo kaufanya Norbert Kaila. He still alive hakufa na bomu lile, sasa jamani tujue huyu mtu ni nani? Kwa nilivyosikia alivyotoroka tayari ni komandoo, yupo nyuma ya nani jamani. Brigadia na mwenzio Kanali, upande wa MI mnaujua vilivyo, Watson upande wa TISS unaufahamu, kuna rekodi za huyu mtu kwneye ufanyaji kazi?"
"Norbert Kaila si mwanajeshi wa JWTZ na hakuna special force mwenye jina kama lake. Tukianza kazi hii, nilipitia rekodi ya kila special force wa MI ila sikuwahi kuona jina hilo", Brigadia alisema
"Anayoyasema Brigadia ni kweli kabisa, rekodi yake ipo tu kwa kuwahi kupitia mafunzo ya kijeshi ya JKT na alitakiwa kuajiriwa kama angeenda Monduli ila mzazi wake marehemu Brigadia Alphonce Kaila alipinga hilo ndipo akaenda kusomea uandishi huyu. Kuwahi kupitia kwake mafunzo tunajua wachache tu, hakuna mwingine anayefahamu miongoni mwa raia", Kanali alisema.
"Pia kiupande wangu rekodi zote za TISS nazifahamu fika, Norbert Kaila si mtu wa kwenye system labda awe informer wa mtu aliyepo kwenye system na si vinginevyo", Watson alisema.
"Sasa huyu mtu yupo upande wa nani? Au EASA hawa, na wameingia vipi kazini hawa washenzi. Mkumbuke hawa ndiyo chanzo cha kukamatwa kwa kaka yangu, inabidi tuwe nao makini zaidi"
"Hilo la muhimu zaidi, mimi natoka hapa na kwenda nyumbani kwa DG wa TISS naenda kumchokonoa zaidi maana tulipanga niende kuchukua kitambulisho kesho cha kusafiri na treni. Ninaweza kupata kitu, maana Moses na Kaila ni marafiki", Watson alisema.
"Watson unaelewa plan yetu ilivyo umekubali vipi kuchukua tiketi ya lile kopo lao. Are you out of your mind?"
"Huze cool down, wewe hakikisha helikopta zetu za kutoroka nchi hii ipo ok. Njia ya kuondokea ni mashariki kwa bahari ya Hindi tu, meli ya Alpha ipo jirani na visiwa vya komoro. Hapo ndiyo tutaenda kuweka kituo chetu cha safari, Gera naye ataondoka na rubani tu, akifika angani anamuua kisha anakamata chombo kuufata mwenyewe", Watson alisema.
"Nilitaka nishangae ujue, yaani Watson huyuhuyu akubali kupanda kopo lile, jamani kwanza hapa tugawane majukumu. Alpha anaingia leo hii saa tatu usiku huu, naomba Brigadia ukamchukue na kumpeleka mahali stahiki. Watson unaweza kuendelea na mpango wako wa kumchimba DG. Tena wakikubali masharti yetu nafikiri mnaju nini cha kufanya"
"Kazi ya bomu ni kulipua, hakuna ambaye atashughulika kulizima. Bomu kalitengeneza Besi password ukaweka wewe, kuactivate unafanya wewe. Unafikiri nani ataweza kulitegua, bomb squad wote wauawe kwa bomu tukimaliza kila kitu chetu Besi keshaseti mambo kule na mteguaji ni yeye tu hakuna mwingine mwenye kuliweza hilo", Kanali alisema
"Tuanzeni majukumu mara moja jamani, mimi napumzika hadi saa sita usiku kisha nitakuja kuonana na Alpha", Huze alihitimisha kikao hicho, baada ya kukubaliana kila mmoja kuchukua jukumu aliloagizwa. **
Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere
Eneo la kutokea abiria wanaowasili, alionekana mzungu aliyevaa kofia ambayo ilifunika uso wake kwa kiasi kikubwa. Huyu alishuka akiwa na mkoba wa begani, huku akiwa ameshika kitoroli chenye sanduku kubwa la nguo. Alitembea kwa taratibu hadi akafika usawa ambao kuna mwanaume wa makamo mwenye suti nadhifu akiwa amekaa, alipomfikia aliipeleka kofia yake chini zaidi kisha akampita na kutoka kuelekea nje.
Mtu yule alimtazama tu na alipompita alianza kutoka na kumfuata kwa nyuma, mzungu alifika kwenye mlango wa gari kisha akasimama. Muda huohuo ilisikika kengele maalum na taa za pembeni kuwakaa kuashiria milango imefunguliwa kwa rimoti maalum. Alifungua mlango wa pembeni ya dereva akaingia na begi lake, kisha akaufunga na kuacha kitoroli mahali hapo. Naye a;liyekuwa ameketi kule ndani alifika na kuingia upande wa dereva.
"Brigadia fanya hima twondoke mahali hapa, kabla hawajajua aliyekuja kunipokea ni nani?", Mzungu yule alisema.
"Sawa Alpha usihofu kwa hilo, ila mbona umekuja na mkoba mkubwa hivyo wakati hukai kwa muda mrefu huku", Brigadia alismea huku akiwasha gari.
"Mimi ni komandoo na pia ni mzee wa kazi, fikiri nikija mikono mitupu wakati EASA wananijua fika si ndiyo mwanzo wa kuanza kufuatiliwa shaka. Wapo airport nimewaona wa kawaida, pia kuna makachero kadhaa wamepandikizwa na wanafanya kazi mahali hapo. Wakiona na begi hili hawatodhani kama nimekuja kikazi, watajua ni kutalii ndiyo maana nikabeba mzigo huo wa nguo maana kama nimekuja kivingine nikibeba hili itakuwa ngumu kutoroka"
"Ok nimekuelewa hivi sasa, sasa humo ndani kuna nini?"
"Matambara tu nimeyakunja kama nguo, tukifika mbele nitatupa hili begi halina maana. Mkoba huu niliyoupakata ndiyo kila kitu aise"
**
Nyumbani kwa Moses majira hayo, Beatrice na mtoto wapo chumbani na sebuleni yupo Watson na mwenyeji wake wakizungumza. Majukumu waliyepeana ndiyo tayari muda huo wameanza kupatiana hapo Mzee huyu msaliti wa nchi ambaye anaheshimika kutokana na kuifanyia mengi idara ya usalama wa taifa. Alitaka kujua kile kinachoendelea kuhusu Kaila hadi akafikia kule, alitaka kumfahamu kwa namna ya kumchimbua maana anaamini Gawaza hakuwa na ubavu wa kumficha chochote kile kwa jinsi alivyo mshauri kwenye mambo mengi yenye manufaa kwa taifa.
"Kijana kwanza nikupe pole sana, nimesikia rafiki yako amefariki na mwili wake upo mikononi mwa EASA kiuchunguzi. Mungu amlaze mahala pema Kaila, mpiganaji na mwanaharakati wa taifa hili", Watson alianza kumchokonoa Moses.
"Pole ya nini mzee wangu, Norbert yupo hai. Watu waliyofanya kazi ile walichanganya magari, hawakujua siku ile kulikuwa na magari mawili ya aina moja kule Karimjee. Wamemuua mtu asiye na hatia, wakimlenga yeye ambaye anaonekana wazi ni chukizo kwao",
"Ohoo! Asante Mungu kwa kumuokoa mpiganaji wako, ila kijana wangu nilitaka nikwambie kuwa kesho sitofika stesheni kule Pugu. Mama yangu ni mgonjwa nimepigiwa simu muda si mrefu, kesho nitaelekea Dodoma kwa ndege binafsi kwenda kumwona"
"Mr Mbilinyi yaani tumepewa usafiri bora kabisa na unafika huko, kwanini usingetumia hii treni tu hadi huko. Ingawa haiweki kituo hapo Dodoma, ila kwa heshima yako unaweza kushushwa kama tukimshaiwshi mheshimiwa. Huoni ni nafasi hiyo na itaokoa nauli"
"Hapana, natakiwa nifike kule saa kumi na mbili. Ili nifanye mipamgo ya kumleta jijini hapa mapema apelekwe hospitali moja kwa moja. Unajua wazi huduma bora ipo hapa jijini kutokana na jinsi sehemu zingine zilivyotupwa kimaendeleo na kutazamwa Dar tu"
"Kwahilo siwezi kukuzua kwakweli, nafikiri ungeenda tu kupumzika mzee wangu. Uwahi kuamka na kufika mapema airport, nikutakie usiku mwema"
"Nawe pia kijana wangu", Moses na Watson walipenea mikono halafu mgeni akasindikizwa hadi kwenye maegesho ya nyumbani hapo ambapo gari la Watson lilikuwepo.
**
SAA SITA USIKU,
SEPTEMBA MOSI KUISHA KWA AGOSTI 31
Mitambo yenye kuongoza kila kitu kilichopangwa nao, ilishawekwa sehemu ya maficho kwa akina Huze. Majira hayo vioo vingi vya tarakilishi vilikuwa vikitazamana na meza yenye kitambaachi pamoja na 'keyboard'. Kitini Huze ndiyo alikuwepo huku wengine wakiwa wamesimama kutazama mandhari ya sehemu tofauti ndani ya treni ya kisasa ambayo ndiyo inazinduliwa kwa safari za mbali nchini Tanzania. Mandhari ya ndani ilipendeza haswa, kukiwa ni kutupu huku baadhi ya wanausalama wa idara ya usalama wa taifa wakionekana wakihakikisha usalama unakuwepo pasipo wao kubaini ulishakuwa hatarini eneo hilo.
Kufikia mpango huo ulivyo, kila mmoja hapo aliendelea kutoa pongezi kwa Besi ambaye alisimama nyuma ya Huze akiwa wengine wakitazama jinsi hali ilivyo. Tayari majira hayo Alpha ambaye ni kiongozi wao, alishaweka kiasi kikubwa cha pesa kwenye akaunti yake ya benki kwa kuweza kufanikisha hilo. Kwa jinsi alivyo na hela nyingi, mwenyewe aliamua kutumia kiasi kwenye akaunti ya baba yake mzazi kuweza kusaidia matibabu ya mdogo wake. Chuki ile aliyokuwa nayo awali ilimwondoka kutokana na kuzidiwa na furaha kupita kiasi. aliamua kusaidia kabla hajaamua kuondoka nchini na kuelekea mbali baada ya kukamilisha jukumu lake zito.
**
ASUBUHI
Mzee Mluva aliamka na kujiandaa akiwa na kila kitu chake kuhusu safari hiyo ya kwenda Mwanza, mapambazuko yalimkuta akiwa yupo kwenye lango la kuingia ndani kwenye treni. Alishajiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea jijini humo, majira ya saa moja asubuhi ndipo kukafanyika uzinduzi huku mawaziri na sehemu kubwa ya wakubwa wa majeshi wakiwepo eneo la tukio. Rais Zuber alikata utepe kuzindua safari hiyo na akawa wa kwanza kupanda ndani, huku mawaziri na viongozi wengine wa taifa la Tanzani wakifuatia kwa nyuma.
Wananchi nao bila ya kukawia waliingia kwenye mabehewa yao kwa ajili ya safari hiyo, muda mchache baadaye wanausalama nao walipanda kwa kujichanganya na abiria huku wengine wakiwepo behewa la mbele ambalo lipo jirani na kichwa cha treni ambapo ndipo viongozi walikuwepo huko pamoja na waandishi wa habari ambao walifuatilia kwa kina juu ya tukio hilo linavyoendelea.
Hatimaye safari ya Septemba mosi, siku ya kusherekewa kuundwa kwa JWTZ. Iliyosubiriwa kwa hamu, ilianza kwa treni hilo kwenda mwendo mdogo huku milango na vioo vyote vikiwa vimefungwa kwa usalama zaidi. Hatimaye lilichanganya na kuwa na mwendokasi mkubwa, wengi waliongea kupitisha muda huku behewa kuu ndiyo Mheshimiwa akawa anasifia zaidi kwa jinsi safari hiyo ilivyokuwa nzuri pia ubora wa vifaa hivyo.
Wanachi wasiyopanda walibaki wakishuhudia kwenye runinga zao, namna ambavyo Mheshimiwa ameketi kwenye behewa la hadhi huku kiyoyozi kikiwa kila mahali. Pia waliweza kuona wananchi wengine wakiwepo kwenye upande wenye ubora zaidi, hakika lilikuwa ni tukio lenye kufurahisha na kila mmoja akatoa pongezi kwa serikali kuweza kutimiza hilo suala ambalo lilikuwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu. Wabunge ambao hapo awali waliusema vibaya huo mpango wa ujenzi wa reli yenye kasi, walijikuta wakipanda nao kutokana na mwaliko maalum waliyopatiwa kwenye safari hiyo.
ITAENDELEA
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment