WANAFUNZI 722 WA KIDATO CHA SITA WAFANYA MITIHANI ARUSHA
Na Woinde Shizza, michuzi Tv Arusha
JUMLA ya wanafunzi 722, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, wameanza mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita na vyuo, iliyoanza tarehe 29.06.2020 kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa -'NECTA'.
Akizungumza na mwandishi wa habari, Afisa Elimu Sekondari, Menard Lupenza amefafanua kuwa, jumla ya wanafunzi 722 wanafanya mitihani ya kidato cha sita, mithani itakayofanyiaka kuanzia tarehe 29.06.2020 na kumalizika tarehe 15.07.2020.
Ameongeza kuwa idadi hiyo ya wanafunzi 722, inajumumuisha wanafunzi 689 wa kidato cha sita ikiwa wasichana ni 381 na wavulana 342 pamoja na wanafunzi 33 wa vyuo vya Ualimu, ambapo wavulana ni 11 na wasichana 22.
Hata hivyo Afisa Elimu huyo amesema kuwa, maandalizi yote ya mtihani huo tayari yamekamilika kufuatia ratiba ya Baraza la Mitihani la Taifa na wanafunzi wameandaliwa vema na wako tayari kwa kufanya mitihani hiyo.
"Maandalizi ya mitihani yamekamilika, kufuatia atiba ya mitihani iliyotolewa na NECTA, na wanafunzi wameandaliwa vema tayari kwa mitihani hiyo" amesema Afisa Elimu Lupenza.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Mringa, mwalimu Salum Magaka, amethibitisha kukamilika kwa maandalizi ya watahiniwa shuleni kwake, na kuongeza kuwa jumla ya watahiniwa 145 wanategemea kufanya mitihani ya kidato cha sita, huku wanafunzi wote wakiwa tayari kwa mitihani hiyo kwa mujibu wa ratiba ya Baraza la Mitihani.
"Licha ya wanafunzi kukaa nyumbani kwa muda mrefu kutokana na ugonjwa wa Corona, lakini walimu wa masomo walikamilisha mada zote walizotakiwa kusoma, na wanafunzi wameandaliwa vizuri kisaikolojia na kitaaluma na wako tayari kufanya mitihani inayoanza kesho, na nina hakika watafanya vizuri na kupata ufaulu wa juu". Amesema Mkuu wa shule ya Sekondari Mringa
Awali Katibu Mkuu Baraza la Mitihani la Taifa Dkt. Charles Msonda amewataka wasimamizi wa mithani kuepuka vitendo vya udanganyifu na kufuata kanuni, sheria na taratibu za mitihani ya Taifa na kuwaonya wamiliki wa shule binafsi, kutowaingilia wasimamizi wa mitihani hiyo.
Halmashauri ya Arusha, inawatakia kila la kheri wanafunzi wote wa halmashauri Arusha, pamoja na watahiniwa wote Tanzania, katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita, wafaulu vizuri ikiwa ni mandalizi ya kuelekea vyuo vya elimu ya juu.
Previous article
Leave Comments
Post a Comment