SEPTEMBER 1 SEHEMU YA KUMI NA MOJA.
:max_bytes(150000):strip_icc()/iStock-637126086-5978d78f0d327a0011b429d4.jpg)
SEPTEMBER 1
SEHEMU YA KUMI NA MOJA.
TULIPOISHIA SEHEMU YA KUMI...
"Basi kaa hapo utaweza kuona kile nitakachokifanya, natumai tutacheka wote kama ilivyokuwa muda si mrefu. Najua wewe ni bingwa wa kucheka, naenda kwa wapumbavu wenzako kisha nitarejea kwako pia usihofu tutacheka sana. Napenda sana mtu mwenye kufurahi kama wewe"
"(Akicheka) Acha kunipiga mikwara Kaila, you are loser"
"Hata mimi naona pia"
TUENDELEE...
Majira hayo ofisini kwa Besi, mlango ulifunguliwa kwa fujo. Aliingia mwanamke huku nyuma kukiwa na katibu muhtasi wake, ujio wake ulionesha wazi mwanamama huyo aliingia kwa lazima bila ya ruhusa ya msaidizi wake. Hali hiyo na pia kumwona mahala hapo mtu huyo, mwenye ofisi alijikuta akisimama wima huku akimtazmaa kwa mshangao.
Mwanamke yule ambaye ni mtu mzima, alifika na kupiga magoti mbele yake huku machozi yakimtoka. Hali hiyo ilimshangaza hata binti mwenye kutoa taarifa za wageni wenye kufika humo, hakujua imekuwaje hadi akafikia kuwa hapo.
"Mwanangu naomba msaada wako mdogo wako atakufa yule", Mwanamke huyo aliongea huku akijaribu kugusa miguu ya Besi ila alimkwepa kwa kurudi nyuma.
"Kama kufa tu mwache afe, mimi ndiyo yuleyule uchafu uliyosema marehemu kauacha. Jiulize takataka itaanzaje kukusaidia wewe, mahala pake si jalalani. Katafute isiyokuwa takataka ikusaidie ila siyo mimi, naomba utoke ofisini kwangu kabla sijaita security"
"mwanangu nilikosea nisamehe baba, nahitaji msaada wako hivi sasa"
"Ulipojifungua mtoto si ndiyo uliona umemaliza kila kitu, umesahau hata kesho yako huijui. Basi jeuri zako ndiyo zikulipie pesa za kumfanyia operesheni, sina mdogo ambaye ananiita mimi takataka. Uchafu ndugu yake ni uchafu, yeye siyo atawezaje kuwa ndugu yangu, ondokaa!", Besi aliposema hayo alibonyeza kitufe kilichpo ukutani humo chumbani mwake kisha akaweka mdomo kwenye spike iliyopo jirani na eneo alilobofya.
Alisema, "Security nawahitaji haraka sana". Muda mchache baadaye waliingia walinzi wenye sare maalum ambao walimtoa mwanamke yule kinguvu huku akilia. Kwake Besi haikuwa kitu chenye kumuumiza kila akikumbuka namna ambayo ameishi naye kwa kipindi kirefu tena kwa mateso makubwa mno. Moyo wake ulishaingiwa na giza, haukuona neno msamaha kwake na kila alipomwona ndiyo hasira zilimzidi zaidi.
"Na wewe kaendelee na kazi mtu kama huyo usije ukamruhusu aingie kwa namna yeyote ile", Besi alisema.
"Nimemzuia najua huu muda huhitaji mgeni bosi, ila kaingia kinguvu akisema ni mama yako"
"Ita security, nahitaji kuwa peke yangu hivi sasa. Baadaye nitaelekea Pugu kuendelea na kazi ya kiserikali"
**
Hali ya gerezani ilikuwa si shwari kwa Gera, muda mfupi alitokea kuwa mtemi wa gereza lote kwa wale wanaojifanya wababe. Mwili wake na jinsi alivyo mbabe ni vitu viwili tofauti, aliweza kuwatuliza wenye miili ya mazoezi kutokana na mafunzo hatari aliyopatiwa. Ubabe huo aliuendelea hadi ikafikia ni mwenye kupiga maaskari kila kukicha, haikupita siku basi askari mmoja akawa ni wa kulazwa hospitali ya nyumba ya giza. Hilo walimkariri, kila mmoja akimhofia, taarifa zake hatimaye zikafika kwa mkuu wa gereza wa wakati huo. Kamishna James Nkongo, huyu alipokea sifa na namna anavyowapa tabu maaskari wake.
Majira ambayo Besi anamtoa mama yake ndani, alipokea taarifa kupitia kwenye simu ya upepo afisa mwingine wa magereza anasulubiwa na Gera. Jambo hili liliamsha hasira za Afande Nkongo na kwa haraka alitoka ofisini kwake akiwa mikono mitupu hakubeba hata rungu, alikimbia kwa haraka kwenda hadi eneo ambalo mhalifu wao anafanya unyama.
Alipofika bila kuchelewa alimrukia mateke mawili ambayo yalimpata kifuani akaenda chini, tukio hilo lilifanya ukimya utande humo ndani. Wafungwa wote walimheshimu mno afande huyo, hakuna ambaye alithubutu kutoa sauti yake. Kila mmoja alitazama kile kinachoendelea kwa kuingia kwake mahala hapo, Gera kwa mara ya kwanza ndipo aliangushwa chini na alipoinuka alikuta na askari mrefu mwenye mwili wa kimazoezi.
"Kila siku unajua kuonea sana vijana wangu, sasa pambana na mimi tuone mimi na wewe nani ataingia hospitali leo. Ukiweza kunifanya nikalazwe naacha kazi hii kuanzia leo", Afande Nkongo alisema kwa kujiamini.
Kauli iliyomfanya Gera amjie kwa kutanguliza teke, mpinzani wake akalikwepa. Akiwa huko kando alipeleka ngumi mfululizo, napo zikaishia hewani. Alijitahidi kuonesha ujuzi wake kwenye mapigano lakini hakufua dafu, hapo ndipo akabaini amekutana na chupa cha pua. Akabadili upigani, alidhani angeweza kumpata napo ikawa ni bilabila.
Zamu yake ya kuanza kushambuliwa ilipofika, alijuta hata kujaribu kuwa mkorofi humo ndani. Alipigwa kama mtoto mdogo na Kamishna Nkongo, mapigo ambayo yalimchakaza hadia akafikia kutokwa na majeraha mengi mwili wake. Ilifika mahali akawa hawezi kuendelea kupigana kabisa, kweli alikutana na mwamba ilihali amezoea kuchezea mawe.
"Nilikwambia ukinipiga mimi naacha kazi, hilo huwezi. Chukueni huyu mtupeni shimo la kifo, atapasua kokoto akiwa gizani asione mwanga wowote kuanzia hii leo. Hakikisha hafi, anatakiwa kubaki hai kwa namna yeyote ile", Afande Nkongo alitoa maelekezo kisha akawagekia wafungwa waliyokuwa wakitazama mpambano. Aliwaambia, "Kila mmoja akaendelee na kazi yake sasa hivi, atakayeleta kiburi nitajua cha kumfanya mwenyewe. Tulikubaliana tuishi kwa kiadabu humu, jeuri ya mmoja kitampata kama cha yule. Sipendi kupiga mtu msinilazimishe". Alipomaliza kuongea, aliondoka hapo huku akitoa kitambaa mfukoni, alijifuta jasho huku akipandisha ngazi kurejea ofisini kwake.
**
Kutokana na mtandao mpana ambao kina Huze wanao, haikuwa jambo la ajabu kwao kuweza kupata taarifa ya kile kinachoendelea. Kwani kukitokea mabadiliko yeyote yale habari hufikishwa kwa DG wa usalama wa taifa, na pia makao makuu ya EASA. DG naye alimwamini mno Watson kutokana na ushauri wake kwenye mambo mbalimbali, akamvujishia juu ya habari hiyo.
Naye hakuiweka moyoni mwake, aliileta moja kwa moja kwa kaka wa Gera. Kumpatia taarifa ambayo ilimtia hasira kupitiliza, alitamani hata aende kuvamia kule gerezani na kumtorosha ndugu yake lakini suala hilo haliwezekani.
"Nkongo ndiyo anaamua kumtuoa ndugu yangu kwenye shimo la kifo, mahali ambapo si salama kuishi kiumbe wa aina yeyote. Haki ya Mungu nikimtoa huko ndiyo atajuta, namwambia amalize familia yake yote", Huze alisema akiuma meno.
"Yaani eneo alilomuweka ni kuna joto, kile chumba kipo chini ya mlima kabisa, kuta zimejengewa kwenye mwamba. Hakina mwanga na kina joto kupitiliza, kuna tundu la kupumulia tu, tena akiwa humo amewekewa jiwe kubwa apasue kokoto. Huyu Nkongo ni mnyama sana", Watson alisema.
"Labda nisiwe Huze ninayefahamika, Kamishna na mke wake ASP watajuta akitoka kaka yangu. Mshenzi sana, hajui kapata tabu ngapi hadi mimi nipo hapa, leo aje kumtenda tu nasema sikubali"
"Kila jambo lina wakati wake, nasi tusubiri wakati wetu tutaweza kumwonesha ni namna gani tuna nguvu. Sasa hivi cool down"
**
Majira hayo Norbert Kaila alikuwa nyumbani kwa Belinda, alihitaji mno kuonana naye na wala hakutaka kufika ofisini. Afisa huyu wa jeshi naye alifahamu fika hakufa kwenye mlipuko ule, hivyo hakushangazwana kuhitajika kwake kuzungumza naye. Alichukulia ni jambo la kawaida tu. Aliikacha ofisi na kuwasili hapo, ambapo ni salama kwao kuweka kikao kuliko hata sehemu nyingine yeyote ile.
Walifikia meza kubwa ya nyumba hiyo, ambao walikaa mkabala. Belinda akiwa na vazi la kazini, huku Kaila akiwa na mavazi yaleyale aliyotoka naye nyumbani kwa Norene.
"Nor nipe habari kuna kipi kipya kilichoweza hadi ukaniita huku?", Belnda aliuliza.
"Belinda kuna maafisa wawili wa chini yako ndiyo wasaliti wakubwa wa jeshi na sijui kwanini wanafanya hivyo", Norbert alisema
"Are you sure? Hii ni ishu nyingine kabisa"
"Hivi nisingekuwa na uhakika ningeweza kukueleza hayo, nimeamua nilifikishe kwako hii ishu wapo maafisa wawili. Mmoja ni kanali mwingine ni one star general"
"Kanali na Brigadia, hivi vyeo kuna watu zaidi ya mmoja wanavyo ni ngumu mno kuweza kumpata mhusika mkubwa ni yupi"
"Wapo kambi za hapa jijini, waliyoamua kuvunja kiapo cha utii kisa tamaa zao za muda mfupi"
"Kama ni kambi za hapa kweli wanahesabika, jumla kuna makanali kumi na brigadia wapo nane. Wengine wapo nje ya jiji kwenye kamandi kuu ya anga na nchi kavu"
" hao kumi na nane, wawili ndiyo wanaongoza huu mchezo wote. Nahitaji ujiibe kwa muda wa ziada huku mimi ninaendelea na kazi zingine"
"Hilo halina tabu.....enhee! Nimepata wazo Septemba mosi ni siku ambayo maafisa wote
tutapanda treni kwa ajili ya uzinduzi wake. Siku hiyo ndiyo nzuri kuhakikisha wote wanajulikana, tutatumia hila"
"Mimi sitokuwepo kwenye uzinduzi huo nitakuwa kazini, ila una uhakika wote watapanda?" "Wawili tu ndiyo hawatopanda, mmoja atabaki Ngome kiofisi pia kuwasiliana vikosi vingine kwa ajili ya kuendeleza jukumu la kulinda mipaka ya nchi. Mwingine atatumia helikopta kuhakikisha kila njia itakayopita treni ina usalama. Kusitokee ajali ya yeyote, ukumbuke Mheshimiwa yupo ndani pia"
"Hao wawili ni nani na nani?", Norbert aliuliza
"ooh! Sorry ni watatu ambao ni Kanali Seba ambaye anasalia, msemaji mkuu wa jeshi naye vilevile atasalia. Mwingine ni Brigadia Mkunga"
"Ok kama ni hao basi ni kuhakikisha waliyopo mule ndani kwa namna yeyote ile wanajulikana upesi. Tutatumia hila gani kuweza kufanikisha hilo"
"Nafikiri hakuna hata mmoja anayeweza kucheza na maisha yake, sasa ni kuhakikisha muda ambao treni inaenda kila kioo kimefungwa. Baada
ya hapo tutawatisha kama kuna bomu humo, ambalo halihitaji hewa ya nje linaweza kulipuka"
"Tujaribu hilo, tukiweza kuwaingiza kwenye shimo moja kwa moja basi ndiyo itakuwa mwisho wao"
"Vipi ikiwa hawa nje ndiyo wenye kuhusika na mchezo wote huo?"
"Hao ni juu yako Nor nadhani mimi niachie watakaokuwa ndani ya treni, habari hii nataka niifikishe kwa Afande"
"Hapana si muda wake huo, sitaki afahamu kama nipo hai kwa hivi sasa. Mwache aendelee kubaki na imani ileile kuwa nimekufa kama ilivyo umma wa watanzania"
"Ok, kuna la ziada au kinachofuatana ni soga"
"Toka lini nikapiga soga kipindi nipo kazini. Nikuage tu niwahi huko niendapo hivi sasa. Kwaheri", Norbert alisema huku akiinuka kwenye kti alichoketi
"Goodluck"
"you too, usalama kwa Tanzania kwanza mengine yatafuata baadaye"
**
Siku ndiyo zilikuwa zimebaki chache tu, kuweza kufika septemba mosi. Kipindi ambacho ilitarajiwa vilivyo kushuhudiwa treni ya kisasa ikianza safari yake ya mara ya kwanza ya masafa marefu tangu reli ya SGR ikamilike.
Kuendelea na maandalizi Mhandisi aliyepangwa kuja kulitazama na kuhakikisha usalama upo, aliendelea na kazi yake kama kawaida akionesha kujituma.
Besi ndiyo alichukua jukumu la kuendelea kulikagua na kurekebisha endapo kungeweza na tatizo lolote lile la kuhusu umeme. Pia alitumia njia hiyo kufanya kazi nyingine aliyotumwa, hakuna ambaye alishtuka juu ya hilo hadi alipohitimisha jukumu lake ambalo ameahidiwa mamilioni ya fedha.
Laiti kama serikali ingelimjua huyu mtu na uhalisia wake, basi wasingelimpa jukumu hilo kisa tu ana utaalamu wa umeme. Fisi hakabidhiwi bucha alilinde pasipo kutia hasara yeyote, hilo jambo hakuna aliyeweza kumaizi hadi alipokamilisha na kulipwa ujira mkubwa akarejea walipo wenzake. Ni zaidi ya kosa kubwa kwa serikali, ambalo wamelifanya bila ya wao kujijua.
Huko aliwasimulia kila kitu juu ya kinachoendelea, pongezi nyingi alipatiwa na pia kuongezwa malipo zaidi kuliko yale aliyopewa na serikali kwa kazi aliyoifanya. Watson aliyehakikisha Besi anawepo kwenye hila hiyo, alitoa donge noo ambalo kijana huyu hakuwahi kulipwa kabla ya siku hiyo. Muamala wa fedha uliingia kwenye simu kuonesha pesa hizo zimepelekwa kwenye akaunti yake, jioni ya siku hiyo ilibidi waweke sherehe kwa ajili ya kufurahia jambo hilo ambalo walilisuka kwa muda mrefu kuja kufikia tamati.
"Hivi sasa hakuna injinia hatari kwenye sehemu yeyote ila ya nchi hii, wewe ndiyo mkubwa wao
Besi. Pesa hizo bado tu Mkuu atakuongeza subiri sasa hivi tukimpa taarifa, hutojuta kuwa nasi", Watson alisema usoni akiwa na tabasamu mwanana.
"Besi wewe ni kichwa aisee, hii project yako ambayo umetumia muda mrefu kuweza kuiandaa basi tambua hakuna kiumbe ambaye anaweza kuifikia. Sijawahi kuona kitu kama hicho tangu niingie kwenye huu mchezo. Wewe ni genius", Huze naye alimpongeza huku akigonganisha mkono naye.
"Wote mnajua jinsi nilivyokuwa na hasira na serikali hii, mateso yote ya ajira na elimu kubwa kisomo changu cha maana. Sifa kedekede nilizopewa nikiwa field walitegemea niitumie elimu yangu kinamna gani, yaani unashuhudia mtu ambaye umemzidi kila kigezo anapata ajira ila mimi niliye na ufaulu mzuri sijafikia hapo walipo. Fools all of them, sijaona maana ya elimu yao zaidi ya kuiona hii mliyoniongeza nyinyi. Watajuta majuma mawili mbali, hiyo sikukuu ya majeshi itakwua ni kilio kwao na si kingine", Besi alisema huku akigonganisha bilauri na Watson.
"Rais ndani, makamu wake ndani, mawaziri ndani, mkuu wa majeshi ndani, mnadhimu mkuu ndani, IGP ndani, DIGP ndani, CG wa magereza ndani, DG wa TISS ndani na makomandoo ndani. Shetani ataizidi dua zao za ufunguzi nguvu", Huze aliongea.
"Umewasahau na wananchi wenye kiherehere cha kwenda Mwanza na Kigoma kwa muda mfupi nao itawakuta ileile. Halafu kitu chetu kilaini tunakipata, mnaonaje kwenye mpango huu watuongeze na dhahbu zote zitakazotoka Geita kusafirishwa zije kwetu", Watson alisema.
"Hilo ni wazo zuri yaani tukitoka hapa ni mwendo wa kuwa billionea, tutawaachia nchi yao na hasara ambayo hawajawahi kuipata", Huze alisema.
Waliendelea kunywa na kufurahi, kwa kukamilisha sehemu ya mpango wao ambayo itahitaji utimizwaji tu waweze kufikia kilele cha mafanikio. Watu hawa walikuwa tayari kwa lolote, ilimradi tu wafikie malengo yao waliyoyaweka.
ITAENDELEA
NAFASI MPYA ZA KAZI KWA WENYE ELIMU KUANZIA DARASA LA SABA ,KIDATO CHA NNE,CERTIFICATE,DIPLOMA,DEGREE NA KUENDELEA ZIPATE KUPITIA AJIRA FORUM APP 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇
Previous article
Next article
Leave Comments
Post a Comment